Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 53

Ujasiri wa Yehoyada

Ujasiri wa Yehoyada

Yezebeli alikuwa na binti anayeitwa Athalia, ambaye alikuwa mwovu kama mama yake tu. Athalia alikuwa mke wa mfalme wa Yuda. Mume wake alipokufa, mwana wake akaanza kutawala. Lakini mwana wake alipokufa, Athalia akajitawaza kuwa malkia wa Yuda. Kisha akajaribu kuangamiza ukoo wote wa kifalme, kwa kuua kila mtu ambaye angeweza kuwa mfalme, kutia ndani wajukuu wake mwenyewe. Kila mtu alimwogopa.

Kuhani Mkuu Yehoyada na mke wake, Yehosheba, walijua kwamba jambo ambalo Athalia alikuwa akifanya lilikuwa baya sana. Kwa hiyo, wakahatarisha uhai wao ili kumficha mjukuu wa Athalia, mtoto mchanga aliyeitwa Yehoashi. Wakamlea hekaluni.

Yehoashi alipokuwa na umri wa miaka saba, Yehoyada alikusanya wakuu na Walawi na kuwaambia hivi: ‘Ilindeni milango ya hekalu na msimruhusu mtu yeyote aingie ndani.’ Kisha Yehoyada akamfanya Yehoashi kuwa mfalme wa Yuda na kumvika taji kichwani. Watu wa Yuda wakapaaza sauti hivi: ‘Mfalme na aishi!’

Malkia Athalia aliposikia sauti za umati akakimbia kwenda hekaluni. Alipomwona mfalme mpya, akalia kwa sauti: “Ni hila! Ni hila!” Wakuu wakamkamata malkia huyo mwovu, wakamwondoa hekaluni, na kumuua. Lakini, namna gani kuhusu uvutano wake mbaya juu ya taifa hilo?

Yehoyada alilisaidia taifa lifanye agano na Yehova, nao wakaahidi kumwabudu Yehova peke yake. Yehoyada aliwaagiza wabomoe hekalu la Baali na kuvunja sanamu zote. Kisha akaweka rasmi makuhani na Walawi wafanye kazi hekaluni ili watu waabudu huko tena. Akawaweka watunza-malango walinde hekalu ili mtu yeyote asiye safi asiingie. Kisha Yehoyada na wakuu wakampeleka Yehoashi kwenye nyumba ya mfalme na kumketisha juu ya kiti cha ufalme. Watu wa Yuda wakashangilia. Hatimaye wangeweza kumtumikia Yehova bila uvutano mbaya wa Athalia mwovu na ibada ya Baali. Je, umeona jinsi ujasiri wa Yehoyada ulivyowasaidia watu wengi?

“Msiwaogope wale wanaoua mwili lakini hawawezi kuua nafsi; badala yake, mwogopeni yule anayeweza kuangamiza nafsi na mwili katika Gehena.”​—Mathayo 10:28