Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 49

Malkia Mwovu Aadhibiwa

Malkia Mwovu Aadhibiwa

Mfalme Ahabu angeweza kuona shamba la mizabibu la mwanamume aliyeitwa Nabothi kupitia dirisha la nyumba yake ya kifalme. Ahabu alitaka shamba hilo la mizabibu, na akajaribu kulinunua kutoka kwa Nabothi. Lakini Nabothi akakataa kumuuzia shamba hilo kwa kuwa Sheria ya Yehova haikuwaruhusu watu kuuza shamba walilorithi. Je, Ahabu alimheshimu Nabothi kwa sababu alifanya jambo lililofaa? Hapana. Ahabu alikasirika sana. Alikasirika kiasi cha kwamba akakataa kutoka nje ya chumba chake, na hata akakataa kula.

Mke wake, Malkia Yezebeli mwovu, akamwambia Ahabu hivi: ‘Wewe ndiye mfalme wa Israeli. Unaweza kupata chochote unachotaka. Mimi nitakupa shamba hilo.’ Yezebeli akawaandikia wazee wa jiji barua, akawaambia wamshtaki Nabothi kwamba amemlaani Mungu na wampige mawe hadi afe. Wazee wakafanya kile ambacho Yezebeli aliwaambia wafanye, kisha Yezebeli akamwambia Ahabu hivi: ‘Nabothi amekufa. Shamba la mizabibu ni lako.’

Nabothi hakuwa mtu pekee asiye na hatia ambaye Yezebeli aliua. Aliwaua watu wengi waliompenda Yehova. Pia, Yezebeli aliabudu sanamu na kufanya mambo mengine mabaya. Yehova aliona mambo yote mabaya ambayo Yezebeli alifanya. Yehova angemfanya nini Yezebeli?

Ahabu alipokufa, Yehoramu, mwana wake akawa mfalme. Yehova akamtuma mwanamume anayeitwa Yehu amwadhibu Yezebeli na familia yake.

Yehu alipanda gari lake na kwenda Yezreeli, ambako Yezebeli aliishi. Yehoramu akapanda gari lake ili kukutana na Yehu na kumuuliza hivi: ‘Je, kuna amani kati yetu?’ Yehu akamjibu: ‘Hakuwezi kuwa na amani ikiwa Yezebeli mama yako anatenda maovu.’ Yehoramu akajaribu kugeuza gari lake ili akimbie. Lakini Yehu akampiga kwa mshale, naye Yehoramu akafa.

Kisha Yehu akaelekea kwenye jumba la kifalme ambapo Yezebeli aliishi. Yezebeli aliposikia kwamba Yehu anakuja, akajipamba na kutengeneza nywele, kisha akamsubiri kwenye dirisha lililokuwa kwenye orofa ya juu. Yehu alipofika, Yezebeli akamsalimu kwa dharau. Yehu akapaaza sauti na kuwaambia watumishi wa Yezebeli waliokuwa wamesimama kando yake: ‘Mtupeni chini!’ Watumishi hao wakamtupa Yezebeli kupitia dirishani, akaanguka chini na kufa.

Baada ya hapo, Yehu akawaua wana 70 wa Ahabu na kuondoa kabisa ibada ya Baali nchini kote. Je, umeona kwamba Yehova anajua kila kitu na kwamba kwa wakati unaofaa, atawaadhibu wale wanaofanya mambo mabaya?

“Urithi unaopatikana kwa pupa mwanzoni hautakuwa baraka mwishoni.”​—Methali 20:21

1 Wafalme 21:1-29; 2 Wafalme 9:1–10:30