Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 43

Dhambi ya Mfalme Daudi

Dhambi ya Mfalme Daudi

Sauli alipokufa, Daudi akawa mfalme. Alikuwa na umri wa miaka 30. Baada ya kuwa mfalme kwa miaka kadhaa, usiku mmoja akiwa juu ya nyumba yake alimwona mwanamke mrembo. Daudi akaambiwa kwamba mwanamke huyo anaitwa Bath-sheba na kwamba alikuwa mke wa askari-jeshi anayeitwa Uria. Daudi akaagiza Bath-sheba aletwe kwenye nyumba yake ya kifalme. Akalala naye, na Bath-sheba akawa mja-mzito. Daudi alijaribu kuficha kile alichokuwa amefanya. Alimwambia mkuu wa jeshi lake amweke Uria kwenye mstari wa mbele wa vita kisha waondoke na kumwacha peke yake. Uria alipouawa vitani, Daudi akamwoa Bath-sheba.

Lakini Yehova aliona mambo yote mabaya yaliyotukia. Angefanya nini? Yehova alimtuma nabii Nathani aende kwa Daudi. Nathani akamwambia hivi: ‘Mwanamume fulani tajiri alikuwa na kondoo wengi, na mwanamume maskini alikuwa na mwana-kondoo mmoja mdogo ambaye alimpenda sana. Yule tajiri akamchukua mwana-kondoo wa yule mwanamume maskini.’ Daudi akakasirika na kusema: ‘Huyo mwanamume tajiri anastahili kufa!’ Ndipo Nathani akamwambia Daudi: ‘Wewe mwenyewe ndiye yule tajiri!’ Daudi akahuzunika sana, akamwambia Nathani waziwazi hivi: ‘Nimemtendea Yehova dhambi.’ Dhambi hiyo ilimletea Daudi na familia yake matatizo mengi sana. Yehova alimwadhibu Daudi, lakini akamwacha aendelee kuwa hai kwa sababu alikuwa mnyoofu na mnyenyekevu.

Daudi alitaka kumjengea Yehova hekalu, lakini Yehova akamchagua Sulemani mwana wa Daudi alijenge. Daudi alianza kukusanya vitu kwa ajili ya Sulemani na kusema: ‘Hekalu la Yehova linapaswa kuwa lenye utukufu. Sulemani ni mchanga, lakini nitamfanyia matayarisho.’ Daudi alichangia pesa nyingi kwa ajili ya kazi hiyo ya ujenzi. Akatafuta wafanyakazi wenye ustadi. Akakusanya dhahabu na fedha, na akaleta mierezi kutoka Tiro na Sidoni. Alipokaribia kufa, Daudi akampa Sulemani ramani ya ujenzi wa hekalu. Akamwambia hivi: ‘Yehova aliniagiza niandike mambo haya yote kwa ajili yako. Yehova atakusaidia. Usiogope. Uwe mwenye nguvu na ufanye kazi.’

“Anayefunika makosa yake hatafanikiwa, lakini yeyote anayeyaungama na kuyaacha ataonyeshwa rehema.”​—Methali 28:13