Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 99

Mlinzi wa Jela Ajifunza Kweli

Mlinzi wa Jela Ajifunza Kweli

Huko Filipi, kulikuwa na kijakazi aliyekuwa na roho mwovu. Roho huyo mwovu alimtumia msichana huyo kufanya ufundi wa kubashiri, na msichana huyo alikuwa akiwapatia mabwana zake faida nyingi kwa kufanya kazi hiyo. Paulo na Sila walipofika Filipi, msichana huyo aliendelea kuwafuata kwa siku nyingi. Roho huyo mwovu alimfanya apaaze sauti akisema: “Watu hawa ni watumwa wa Mungu Aliye Juu Zaidi.” Mwishowe, Paulo akamwambia huyo roho mwovu: ‘Katika jina la Yesu, ninakuagiza umtoke!’ Huyo roho mwovu akatoka.

Basi, mabwana zake walipoona kwamba hawawezi tena kupata pesa kutoka kwa msichana huyo, walikasirika sana. Wakawakokota Paulo na Sila mpaka kwa mahakimu wa raia, wakasema: ‘Watu hawa wanavunja sheria na wanasumbua sana jiji lote!’ Mahakimu hao wakaamuru kwamba Paulo na Sila wapigwe na kutupwa gerezani. Mlinzi wa jela akawatupa katika gereza la ndani zaidi, lenye giza zaidi, na kuifunga miguu yao katika mikatale.

Huku wafungwa wengine wakiwasikiliza, Paulo na Sila walimsifu Yehova kwa wimbo. Ghafula, katikati ya usiku, tetemeko kubwa la nchi likatukia na kutikisa misingi ya gereza hilo. Milango ya gereza ikafunguka na minyororo na mikatale waliyokuwa wamefungwa ikafunguka. Mlinzi wa jela akaingia haraka ndani ya gereza na kuona kwamba milango ya gereza ilikuwa imefunguka. Akiwazia kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka, akauchomoa upanga ili ajiue.

Wakati huohuo, Paulo akapaaza sauti kubwa, akisema: ‘Usijiumize! Sisi sote tupo hapa!’ Mlinzi huyo akaingia ndani na kuanguka chini mbele ya Paulo na Sila. Naye akawauliza: “Nifanye nini ili niokolewe?” Nao wakamwambia: ‘Wewe na watu wa nyumba yako mnahitaji kumwamini Yesu.’ Basi, Paulo na Sila wakawafundisha neno la Yehova, na mlinzi huyo wa jela pamoja na watu wa nyumba yake wakabatizwa.

“Watu watawakamata ninyi na kuwatesa na kuwakabidhi kwenye masinagogi na magereza. Mtapelekwa mbele ya wafalme na magavana kwa sababu ya jina langu. Hivyo, mtapata nafasi ya kutoa ushahidi.”​—Luka 21:12, 13