Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SOMO LA 65

Esta Awaokoa Watu Wake

Esta Awaokoa Watu Wake

Esta alikuwa msichana Myahudi aliyeishi katika jiji la Uajemi la Shushani. Miaka mingi mapema, Nebukadneza alikuwa ameichukua familia yao kutoka Yerusalemu. Alilelewa na binamu yake Mordekai, mtumishi wa Mfalme Ahasuero wa Uajemi.

Mfalme Ahasuero alitaka malkia mpya. Watumishi wake walimletea wanawake waliokuwa warembo zaidi nchini, kutia ndani Esta. Kati ya wanawake wote hao, mfalme alimchagua Esta kuwa malkia. Mordekai alimwambia Esta asiwaambie watu kwamba yeye ni Myahudi.

Mwanamume mwenye kiburi aliyeitwa Hamani alikuwa mkuu wa wakuu wote. Alitaka kila mtu amwinamie. Mordekai alikataa kumwinamia, na Hamani alikasirika sana hivi kwamba akataka kumwua. Hamani alipogundua kuwa Mordekai alikuwa Myahudi, akapanga njama ya kuwaua Wayahudi wote nchini humo. Akamwambia hivi mfalme: ‘Wayahudi ni watu hatari; unapaswa kuwaangamiza.’ Ahasuero akasema: ‘Fanya unavyotaka,’ naye akampa mamlaka ya kutunga sheria. Hamani akatunga sheria iliyowaamuru watu wawaue Wayahudi wote siku ya 13 ya mwezi wa Adari. Yehova alikuwa akiona yote hayo.

Esta hakujua kuhusu sheria hiyo. Hivyo, Mordekai akamtumia nakala ya sheria na kumwambia hivi: ‘Nenda uzungumze na mfalme.’ Esta akasema: ‘Yeyote anayeingia kwa mfalme bila kuitwa atauawa. Mfalme hajanialika niende kwake kwa siku 30! Lakini nitaenda. Akininyooshea fimbo yake ya enzi, nitaishi. Asipofanya hivyo, basi nitakufa.’

Esta akaenda kwenye ua wa mfalme. Mfalme alipomwona, akamnyooshea fimbo yake ya enzi. Esta akaenda mbele za mfalme, naye akamwuliza hivi: ‘Ungependa nikufanyie nini, Esta?’ Akasema hivi: ‘Ningependa kukualika wewe na Hamani kwenye karamu.’ Walipokuwa kwenye karamu hiyo, Esta akawaalika kwenye karamu ya pili. Walipokuwa kwenye karamu ya pili, mfalme akauliza tena: ‘Ungependa nikufanyie nini?’ Akasema hivi: ‘Kuna mtu ambaye anataka kuniua mimi pamoja na watu wangu. Tafadhali tuokoe.’ Mfalme akauliza: ‘Ni nani anayetaka kukuua?’ Esta akajibu: ‘Ni huyu Hamani mtu mbaya.’ Ahasuero akakasirika sana hivi kwamba akaamuru Hamani auawe siku hiyohiyo.

Lakini hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kufuta sheria ya Hamani, hata mfalme mwenyewe. Kwa hiyo, mfalme akamfanya Mordekai mkuu wa wakuu na kumpatia mamlaka ya kutunga sheria mpya. Mordekai akatunga sheria ambayo iliwaruhusu Wayahudi wajilinde watakaposhambuliwa. Katika siku ya 13 ya mwezi wa Adari, Wayahudi wakawashinda adui zao. Tangu wakati huo, wamekuwa wakisherehekea ushindi huo kila mwaka.

“Mtapelekwa mbele ya magavana na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushahidi kwao na kwa mataifa.”​—Mathayo 10:18