Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hadithi ya 69: Msichana Anamsaidia Mwanamume Mwenye Nguvu

Hadithi ya 69: Msichana Anamsaidia Mwanamume Mwenye Nguvu

UNAJUA msichana mdogo huyu anasema nini? Anamwambia mama huyu juu ya Elisha, nabii wa Yehova, na maajabu ambayo Yehova anamsaidia kufanya.

Mama huyu ni Mshami. Mume wake ni Naamani, mkuu wa jeshi la Shamu. Washami walikuwa wamemchukua msichana mdogo huyu Mwisraeli, wakampelekea mke wa Naamani awe mtumishi wake.

Mke wa Naamani pamoja na kijakazi wake

Naamani ana ukoma. Basi msichana huyo anamwambia mke wa Naamani hivi: ‘Afadhali bwanangu angemwendea nabii wa Yehova katika Israeli. Angemponya ukoma wake.’ Baadaye mume wa mama huyu anaambiwa maneno ya msichana mdogo.

Naamani anataka sana kuponywa; hivyo anaamua kwenda Israeli. Anapofika huko, anakwenda nyumbani kwa Elisha. Elisha anamtuma mtumishi wake amwambie Naamani akaoge mara saba katika Mto Yordani. Jambo hilo lamkasirisha sana Naamani, naye anasema: ‘Mito ya kwetu ni bora kuliko mto wo wote katika Israeli!’ Baada ya kusema hivyo, Naamani anaondoka.

Lakini mmoja wa watumishi wake anamwambia hivi: ‘Bwana wee, kama Elisha angekuambia kufanya jambo gumu, ungelifanya. Basi kwa nini usijioshe kama alivyosema?’ Naamani anamsikiliza mtumishi wake, kisha aenda kujitumbukiza mara saba katika Mto Yordani. Anapofanya hivyo, nyama yake inakuwa ngumu na yenye afya!

Naamani anafurahi sana. Anarudi kwa Elisha na kumwambia: ‘Sasa najua hakika kwamba Mungu wa Israeli ndiye Mungu pekee wa kweli katika dunia yote. Basi, tafadhali, pokea zawadi hii kutoka kwangu.’ Lakini Elisha anajibu: ‘Sitaipokea.’ Lakini Gehazi mtumishi wa Elisha anataka achukue zawadi hiyo.

Basi Gehazi. anafanya hivi. Baada ya Naamani kuondoka, Gehazi anakimbia akamkute. ‘Elisha amenituma nikuambie kwamba anataka zawadi yako awape rafiki waliotembelea sasa hivi,’ Gehazi anasema. Huo ni uongo. Lakini Naamani hajui ni uongo; basi anampa Gehazi zawadi hizo.

Gehazi anaporudi nyumbani, Elisha anajua alilofanya. Yehova amemwambia. Anasema: ‘Kwa kuwa ulifanya ubaya huu, ukoma wa Naamani utakupata wewe.’ Na mara hiyo anapata ukoma!

Twaweza kujifunza nini kutokana na hayo yote? Kwanza, imetupasa tuwe kama msichana yule mdogo na kuzungumza juu ya Yehova. Inaweza kuleta matokeo mazuri. Pili, tusiwe na kiburi kama Naamani alivyokuwa kwanza, lakini tuwatii watumishi wa Mungu. Na tatu, tusiseme uongo kama Gehazi. Je! hatuwezi kujifunza mengi kwa kusoma Biblia?

2 Wafalme 5:1-27.Maswali

  • Yule msichana mdogo unayemwona katika picha anamwambia yule mama nini?
  • Mama huyo ni nani, na msichana huyo anafanya nini katika nyumba ya mama huyo?
  • Elisha anamweleza mtumishi wake amwambie Naamani nini, na kwa nini Naamani anakasirika?
  • Ni jambo gani linalotokea Naamani anapofanya kama watumishi wake wanavyopendekeza?
  • Kwa nini Elisha anakataa zawadi ya Naamani, lakini Gehazi anafanya nini?
  • Ni nini kinachompata Gehazi, na tunajifunza nini kutokana na jambo hilo?

Maswali ya ziada