Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hadithi ya 54: Mwanamume Mwenye Nguvu Kuliko Wote

Hadithi ya 54: Mwanamume Mwenye Nguvu Kuliko Wote

UNAJUA jina la mwanamume mwenye nguvu kuliko wote? Ni mwamuzi Samsoni. Yehova anampa Samsoni nguvu hizo. Hata kabla ya Samsoni kuzaliwa, Yehova anamwambia mama yake hivi: ‘Upesi utazaa mwana. Ataongoza kuokoa Israeli kutokana na Wafilisti.’

Samsoni akipigana na simba

Wafilisti ni watu wabaya wanaoishi Kanaani. Wana wanajeshi wengi, na wanawaumiza Waisraeli sana. Wakati mmoja, Samsoni anapokwenda kwa Wafilisti, simba mkubwa anatokea akinguruma kukutana naye. Lakini Samsoni anamwua simba huyo kwa mikono yake tu. Pia anaua mamia ya Wafilisti wabaya.

Baadaye Samsoni anapendana na mwanamke, Delila. Viongozi Wafilisti wanaahidi kwamba kila mmoja wao atampa Delila vipande 1,100 vya fedha akiwaambia kinachompa Samsoni nguvu nyingi hivyo. Delila anataka fedha zote hizo. Yeye si rafiki wa kweli wa Samsoni, wala wa watu wa Mungu. Anazidi kumwuliza Samsoni kinachompa nguvu nyingi hivyo.

Delila na Samsoni

Mwishowe, Delila amshawishi Samsoni. Naye Samsoni anamwambia siri ya nguvu zake, akisema: ‘Mimi sijanyolewa nywele. Tangu kuzaliwa kwangu, Mungu alinichagua niwe mtumishi wake wa pekee, yaani, Mnadhiri. Nikinyolewa nywele, nitapoteza nguvu.’

Delila anapojua hayo, anamlaza Samsoni katika paja lake. Kisha amwita mtu aje amnyoe nywele. Samsoni anapoamka, anakuta amepoteza nguvu. Ndipo Wafilisti wanakuja kumkamata. Wanamwondoa macho yake mawili, na kumfanya mtumwa wao.

Samsoni akibomoa nguzo

Siku moja Wafilisti wanafanya karamu kubwa ili waabudu Dagoni mungu wao. Wanamtoa Samsoni gerezani ili wamcheke. Wakati huo, nywele za Samsoni zimekua tena. Samsoni anamwambia kijana anayemwongoza kwa mkono: ‘Acha nishike nguzo za jengo hili.’ Kisha Samsoni anamwomba Yehova ampe nguvu, naye anashika nguzo hizo. Anapaza sauti hivi: ‘Acha nife pamoja na Wafilisti.’ Wafilisti wanaokula karamu ni 3,000. Samsoni anapoegemea nguzo hizo, jengo laanguka na kuua watu wote hao wabaya.

Waamuzi sura ya 13 mpaka 16.Maswali

  • Mtu mwenye nguvu kuliko wote ambao wamewahi kuishi anaitwa nani, na ni nani aliyempa nguvu?
  • Kama unavyoona katika picha, Samsoni alifanya nini alipokutana na simba mkubwa?
  • Samsoni anamwambia Delila siri gani katika picha, na jambo hilo linasababishaje kwamba anakamatwa na Wafilisti?
  • Samsoni alisababishaje vifo vya maadui Wafilisti 3,000 siku aliyokufa?

Maswali ya ziada