Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hadithi ya 47: Mwivi Katika Israeli

Hadithi ya 47: Mwivi Katika Israeli
Akani akificha alichoiba

TAZAMA anachozika mwanamume huyu katika hema yake! Ni vazi zuri, dhahabu na vipande vya fedha. Amevichukua katika mji wa Yeriko. Lakini vitu hivyo Yeriko vilitakiwa vifanyiwe nini? Unakumbuka?

Viharibiwe, dhahabu na fedha zipelekwe kwenye hazina ya hema ya Yehova. Basi watu hawa hawakumtii Mungu. Wameiba mali ya Mungu. Jina la mwanamume huyo ni Akani, na walio pamoja naye ni wa jamaa yake. Ebu tuone yanayotokea.

Akani akiisha kuiba vitu hivyo, Yoshua anatuma watu wakaupige mji wa Ai. Lakini wanapigwa vitani. Wengine wanauawa, na wanaobaki wanakimbia. Yoshua anasikitika sana. Analala kifulifuli na kumwomba Yehova hivi: ‘Kwa nini umeacha haya yatupate?’

Yehova anajibu: ‘Amka! Israeli ametenda dhambi. Wamechukua vitu vilivyotakiwa kuharibiwa au vitolewe kwenye hema ya Yehova. Waliiba vazi zuri na kulificha. Sitawabariki ninyi mpaka mtakapoliharibu pamoja na mtu aliyechukua vitu hivyo.’ Yehova anasema atamwonyesha Yoshua mtu huyo mbaya.

Basi Yoshua anakusanya watu wote, naye Yehova anamtenga Akani mbaya kati yao. Akani anasema: ‘Nimefanya dhambi. Niliona vazi zuri, dhahabu na vipande vya fedha. Nilivitaka sana nikavichukua. Mtaviona vimezikwa ndani ya hema yangu.’

Vitu hivyo vinapopatikana na kupelekwa kwa Yoshua, anamwambia Akani hivi: ‘Kwa nini umetuletea taabu? Yehova atakuletea taabu wewe!’ Kisha watu wote wanapiga kwa mawe Akani na jamaa yake mpaka wanakufa. Ni onyo kwamba tusichukue vitu vya wengine, sivyo?

Baada ya hapo Israeli wanaenda tena kuupiga Ai. Wakati huu Yehova anasaidia watu wake, nao wanashinda vita.

Yoshua 7:1-26; 8:1-29.Maswali

  • Katika picha, ni nani mtu huyo anayeficha mali zilizochukuliwa Yeriko, na anasaidiwa na nani?
  • Kwa nini tendo hilo la Akani na familia yake ni baya sana?
  • Yehova anasema nini Yoshua anapomwuliza ni kwa nini Waisraeli walishindwa vitani huko Ai?
  • Baada ya Akani na familia yake kupelekwa mbele ya Yoshua, wanapatwa na nini?
  • Adhabu ambayo Akani alihukumiwa inatufundisha jambo gani muhimu?

Maswali ya ziada