Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hadithi ya 7: Mtu Hodari

Hadithi ya 7: Mtu Hodari
Henoko

WATU walipoanza kuongezeka duniani, wengi wao wakafanya mabaya kama Kaini. Lakini mtu mmoja alikuwa tofauti. Ni huyu anayeitwa Henoko. Henoko alikuwa mtu hodari. Watu wote karibu yake walikuwa wakifanya mabaya, lakini Henoko aliendelea kumtumikia Mungu.

Unajua sababu wakati huo watu walifanya mabaya mengi sana? Kumbuka, Nani alifanya Adamu na Hawa wakatae kumtii Mungu kisha wakala tunda ambalo Mungu aliwakataza? Ni malaika mbaya. Biblia inamwita Shetani. Anataka kumfanya kila mtu awe mbaya.

Unyang’anyi na uuaji

Siku moja Yehova Mungu alimwagiza Henoko awaambie watu jambo fulani ambalo hawakutaka kulisikia. Ni hili: ‘Siku moja Mungu atawaharibu watu wote wabaya.’ Labda watu hao walikasirika sana kwa kusikia hayo. Labda hata walitaka kumwua Henoko. Hivyo ilimpasa Henoko awe hodari sana ili awaambie watu hao jambo ambalo Mungu alikusudia kufanya.

Mungu hakumwacha Henoko akae muda mrefu kati ya watu hao wabaya. Henoko alikaa miaka 365 tu. Kwa nini twasema “miaka 365 tu”? Kwa sababu watu wa siku hizo walikuwa wenye nguvu nyingi kuliko watu wa sasa. Nao walikaa muda mrefu zaidi. Methusela mwana wa Henoko alikaa miaka 969!

Watu wakifanya mambo mabaya

Basi, Henoko alipokufa, watu walizidi kuwa wabaya sana. Biblia yasema kwamba ‘kila jambo walilowaza lilikuwa baya wakati wote,’ na kwamba ‘dunia ikajaa jeuri.’

Unajua sababu moja kwa nini kulikuwako matata mengi sana duniani siku hizo? Shetani alipata njia mpya ya kufanya watu watende mabaya. Tutajifunza hayo katika hadithi inayofuata.

Mwanzo 5:21-24, 27; 6:5; Waebrania 11:5; Yuda 14, 15.Maswali

 • Henoko alikuwa tofauti na watu wengine kwa njia gani?
 • Kwa nini watu walioishi siku za Henoko walifanya mambo mengi mabaya?
 • Watu walifanya mambo gani mabaya? (Ona picha.)
 • Kwa nini Henoko alihitaji kuwa hodari?
 • Watu waliishi kwa muda gani siku hizo, lakini Henoko aliishi miaka mingapi?
 • Watu walizidi kufanya nini baada ya kifo cha Henoko?

Maswali ya ziada

 • Soma Mwanzo 5:21-2427.

  Henoko alikuwa na uhusiano gani pamoja na Yehova? (Mwa. 5:24)

  Kulingana na Biblia, ni nani aliyeishi kwa muda mrefu zaidi duniani kulingana na Biblia, na alikuwa na miaka mingapi alipokufa? (Mwa. 5:27)

 • Soma Mwanzo 6:5.

  Hali ikawa mbaya kadiri gani duniani baada ya Henoko kufa, na hali hiyo inafananaje na siku zetu? (2 Tim. 3:13)

 • Soma Waebrania 11:5.

  Ni sifa gani ya Henoko ‘iliyompendeza Mungu vema,’ na Mungu alifanya nini? (Mwa. 5:22)

 • Soma Yuda 14, 15.

  Wakristo leo wanawezaje kuiga uhodari wa Henoko wanapowaonya watu kuhusu vita vya Har-Magedoni vinavyokaribia? (2 Tim. 4:2; Ebr. 13:6)