Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Barua Kutoka Benin

Nimejipataje Katika Hali Hii?

Nimejipataje Katika Hali Hii?

ILIKUWA asubuhi ya kawaida huko Afrika Magharibi. Harufu nzuri ya mchuzi uliokuwa ukichemshwa na wali ilijaa hewani. Wanawake walitembea wakiwa wamebeba mizigo mizito kichwani. Sauti za vicheko zilichanganyika na mazungumzo makali kati ya wanunuzi na wauzaji. Mara moja jua likaanza kuwa kali.

Kikundi fulani cha watoto kilipoona Yovo, yaani, mtu mweupe, kilianza kuimba na kucheza kama walivyozoea kufanya. Wimbo huo ulianza kwa maneno haya, “Yovo, Yovo, bon soir” na walimalizia kwa kusema “Tafadhali tupe zawadi kwa sababu tumeimba na kucheza.” Mvulana mmoja hakuwa akiimba. Nilipoendelea kutembea njiani, alinifuata na akaanza kunionyesha ishara kwa mikono yake. Nilidhani kwamba ilikuwa lugha ya ishara. Nchini Marekani, nilikuwa nimejifunza herufi za Lugha ya Ishara ya Marekani, lakini nchini Benin watu huzungumza Kifaransa.

Nilijitahidi kutoa ishara za herufi nane za jina langu. Mvulana huyo akaanza kutabasamu kwa furaha. Alinishika mkono na kunielekeza kwenye barabara fulani nyembamba mpaka kwenye nyumba yao iliyojengwa kwa mawe. Familia yao ikajikusanya. Kila mtu alizungumza kwa ishara. Sasa ningefanya nini? Nilitoa ishara za herufi za jina langu kisha nikaandika kwenye karatasi kwamba mimi ni mmishonari anayewafundisha watu Biblia na ningewatembelea tena. Majirani wengine waliokuwa na uwezo wa kusikia walijiunga nasi, wote walitikisa vichwa na kukubaliana nami. Nikajiuliza, ‘Nimejipataje katika hali hii?’

Niliporudi nyumbani nilijiambia, ‘Lazima kuwe na mtu anayeweza kuwasaidia watu hawa wajifunze kuhusu ahadi ya Mungu: “Masikio ya viziwi yatazibuliwa.”’ (Isaya 35:5) Nilifanya utafiti fulani. Hesabu ya watu ya hivi karibuni ilionyesha kwamba nchini Benin kuna jumla ya viziwi na watu wenye tatizo la kusikia 12,000. Nilifurahi nilipotambua kwamba Lugha ya Ishara ya Marekani, ndiyo inayotumiwa katika shule za viziwi wala si Lugha ya Ishara ya Ufaransa. Lakini ilisikitisha sana kujua kwamba hakuna Shahidi hata mmoja wa Yehova huku aliyejua Lugha ya Ishara ya Marekani. Nilimwambia hivi Shahidi mmoja katika eneo letu, “Afadhali kungekuwa mtu anayejua Lugha ya Ishara ya Marekani ili atusaidie.” Akanijibu, “Lakini wewe upo.” Alisema kweli! Niliagiza DVD na kitabu cha kujifunza Lugha ya Ishara ya Marekani, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Sala zangu za kuomba msaada zilijibiwa wakati Shahidi aliyejua Lugha ya Ishara ya Marekani alipohamia Benin kutoka Kamerun.

Watu wengi wakajua kwamba nilikuwa nikijifunza lugha ya ishara. Niliambiwa nimtembelee mwanamume anayeitwa Brice ambaye ni mchoraji. Kibanda chake cha kazi kilichotengenezwa kwa matawi ya mitende yaliyosokotwa kilikuwa na hewa baridi katika eneo lenye unyevunyevu na joto. Kutokana na zoea lake la kupangusa brashi ukutani, kuta za kibanda hicho zilikuwa na rangi tofauti tofauti kama upinde wa mvua. Alipangusa vumbi kwenye viti kadhaa na kunitazama, huku akisubiri nianze. Nikaweka DVD ndani ya mashine yangu ndogo. Akavuta kiti chake karibu na mashini. “Ninaelewa! Ninaelewa!” akasema kwa ishara. Watoto wa eneo hilo wakajikusanya ili kutazama DVD hiyo. Mmoja wao akasema, “Kwa nini wanatazama sinema isiyo na sauti?”

Kila mara nilipomtembelea Brice, kikundi kilichokuja kuona DVD kilizidi kuongezeka. Baada ya muda, Brice na watu wengine wakaanza kuhudhuria mikutano yetu ya Kikristo. Nilipojitahidi kuwatafsiria nilifanya maendeleo katika kujifunza lugha ya ishara. Kikundi hicho kilipozidi kuongezeka, wengine wao hata walianza kunitafuta. Kwa mfano, siku moja nilikuwa nikiendesha polepole gari langu lililozeeka kwenye barabara yenye mashimo huku nikijaribu kuwaepuka mbuzi na nguruwe wasio na mchungaji. Kisha nikasikia sauti nyuma yangu. Nikajiambia, ‘Aah, natumai gari halijaharibika tena!’ Hapana, kuna kipofu aliyekuwa akikimbia nyuma ya gari langu huku akijaribu kunisimamisha kwa kugongagonga gari!

Vikundi vya Lugha ya Ishara ya Marekani vilianzishwa katika majiji mengine. Vipindi vya lugha ya ishara vilipoanzishwa kwenye kusanyiko letu la wilaya la kila mwaka, niliombwa kuwa mmoja wa watafsiri. Nilipoenda jukwaani na kumsubiri msemaji aanze, nilikumbuka nilipoanza mgawo wangu. Nilikuwa nikijiuliza, ‘Ni nini kingine ninachoweza kufanya nikiwa mmishonari barani Afrika?’ Nilipowatazama wasikilizaji, nilijua kwamba nilikuwa nimepata jibu, yaani, kuwa mmishonari anayewasaidia viziwi. Siku hizi sijiulizi tena, ‘Nimejipataje katika hali hii?’