Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kusafiri Mpaka Sehemu ya Mbali Zaidi ya Dunia

Kusafiri Mpaka Sehemu ya Mbali Zaidi ya Dunia

Jinsi Wakristo Walivyoishi Katika Karne ya Kwanza

Kusafiri Mpaka Sehemu ya Mbali Zaidi ya Dunia

“Siku iliyofuata akaondoka pamoja na Barnaba kwenda Derbe. Na baada ya kulitangazia jiji hilo habari njema na kufanya wanafunzi wengi, wakarudi Listra na Ikoniamu na Antiokia.”—MATENDO 14:20, 21.

MSAFIRI anavuta hewa baridi ya asubuhi. Anaingiza miguu yake iliyochoka kwenye viatu vilivyochakaa. Anatazamia kutembea siku nzima.

Huku miale ya jua la asubuhi ikimpiga mgongoni, anafuata barabara ya vumbi inayopitia kwenye shamba la mizabibu na la mizeituni, kisha anapanda kilima chenye mwinuko mkali. Barabarani, anakutana na wasafiri wengine—wakulima wanaotembea kuelekea kwenye mashamba yao, wafanya-biashara wakiwa na wanyama wao waliobeba bidhaa nyingi, na watu wanaosafiri kwenda Yerusalemu kuabudu. Msafiri huyo na wale wanaosafiri naye wanazungumza na kila mtu wanayekutana naye. Lengo lao ni nini? Ni kutimiza utume wa Yesu wa kuwa mashahidi wake “mpaka sehemu ya mbali zaidi ya dunia.”—Matendo 1:8.

Msafiri huyo anaweza kuwa mtume Paulo, au Barnaba, au yeyote kati ya wamishonari wavumilivu wa karne ya kwanza. (Matendo 14:19-26; 15:22) Walikuwa watu imara wasioyumbayumba. Haikuwa rahisi kusafiri wakati huo. Akielezea hali ngumu alizopata kwenye bahari, mtume Paulo aliandika: “Mara tatu nilivunjikiwa na meli, usiku mmoja na mchana mmoja nimekaa katika kilindi.” Haikuwa rahisi pia kusafiri kwenye nchi kavu. Paulo alisema kwamba mara nyingi alikabili “hatari za kutokana na mito” na “hatari za kutokana na wanyang’anyi wa njia kuu.”—2 Wakorintho 11:25-27.

Ungehisi namna gani kusafiri na wamishonari hao? Ungesafiri umbali gani kwa siku? Ungehitaji kubeba nini, na ungelala wapi ukiwa safarini?

Safari ya Nchi Kavu Kufikia karne ya kwanza, Waroma walikuwa wametengeneza barabara nyingi sana zilizounganisha vituo muhimu vya miliki hiyo. Barabara hizo zilijengwa kwa ufundi mkubwa na zilikuwa imara sana. Barabara nyingi zilikuwa na upana wa mita 4.5 na zilijengwa kwa mawe. Zilikuwa na vizuio ukingoni na mawe yaliyoonyesha umbali kati ya vituo mbalimbali. Kwenye barabara kama hizo, mmishonari kama Paulo angeweza kusafiri kilomita 32 hivi kwa siku.

Hata hivyo, huko Palestina, barabara nyingi zilikuwa tu vijia hatari vya vumbi. Hakukuwa na ukingo wa kutenganisha vijia hivyo na mashamba au kuzuia watu wasianguke kwenye mabonde. Msafiri angeweza kukutana na wanyama wa mwituni au wanyang’anyi; au hata apate barabara imefungwa.

Msafiri angebeba nini? Vitu muhimu alivyobeba ni fimbo ya kujilinda (1), godoro lililokunjwa (2), kibeti (3), jozi nyingine ya viatu (4), mfuko wa kubebea chakula (5), mavazi ya kubadilisha (6), ndoo ya ngozi ya kutekea maji kwenye kisima ambayo ingeweza kukunjwa (7), chupa ya maji (8), na mfuko mkubwa wa ngozi wa kubebea vitu vyake vya kibinafsi (9).

Wamishonari hao walikuwa na hakika kwamba wangekutana na wafanya-biashara waliokuwa wakipelekea bidhaa zao kwenye masoko mbalimbali. Wafanya-biashara hao walitegemea punda ambaye si rahisi kujikwaa wala kuanguka. Hakuna mnyama mwingine aliyetegemeka kama punda katika barabara hizo zenye mawe na miteremko mikali. Inasemekana kwamba punda mwenye nguvu angeweza kutembea kilomita 80 kwa siku akiwa amebeba mizigo. Magari ya kukokotwa na ng’ombe au wanyama wengine yangeweza tu kusafiri umbali wa kilomita 8 hadi 20 kwa siku. Lakini ng’ombe wangeweza kubeba mizigo mizito zaidi na walifaa sana kwa safari fupifupi. Msafiri angepita msafara wa ngamia au punda—wakiwa wamebeba mizigo kutoka sehemu zote za dunia. Mjumbe aliyepanda farasi angepita haraka; akiwa amebeba barua na maagizo ya mfalme kupeleka kwenye kituo fulani katika miliki hiyo.

Usiku ulipofika, wasafiri walilala kando ya barabara kwenye kambi zilizotengenezwa haraka-haraka. Baadhi yao walilala kwenye vyumba visivyokuwa na chochote ndani, ambavyo vilikuwa vimejengwa kuzunguka ua wa katikati. Kulikuwa pia na ukuta uliozunguka vyumba hivyo. Hakukuwa na usalama wa kutosha kwenye vyumba hivyo chafu na visivyopendeza. Wasafiri wangeweza kuathiriwa na hali ya anga au vitu vyao kuibwa. Ilipowezekana, wamishonari waliokuwa safarini walilala katika nyumba za watu wa familia au waamini wenzao.—Matendo 17:7; Waroma 12:13.

Safari ya Baharini Mashua ndogo zilisafirisha mizigo na watu katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Galilaya na pia ng’ambo ya bahari hiyo. (Yohana 6:1, 2, 16, 17, 22-24) Meli nyingi kubwa za mizigo zilivuka Bahari ya Mediterania kwenda na kurudi kutoka bandari za mbali. Meli hizi zilipeleka chakula Roma na kusafirisha maofisa wa serikali. Pia zilisafirisha watu kutoka bandari moja hadi nyingine.

Mabaharia waliongozwa na ishara ambazo wangeweza kuona kwa macho. Kwa mfano, mchana walitazama alama fulani na usiku wakatazama nyota. Kwa hiyo, usafiri wa baharini ulikuwa salama kwa kadiri fulani kuanzia mwezi wa Mei (Mwezi wa 5) mpaka katikati ya mwezi wa Septemba (Mwezi wa 9), wakati ambapo yaelekea hali ya anga ingekuwa tulivu zaidi. Lilikuwa jambo la kawaida kuvunjikiwa na meli.—Matendo 27:39-44; 2 Wakorintho 11:25.

Watu hawakuchagua kusafiri kwa meli kwa sababu walifurahia zaidi kusafiri baharini kuliko kusafiri kwenye nchi kavu. Kwenye meli za mizigo zilizotumiwa sana kwa usafiri, starehe za wasafiri hazikutangulizwa. Wasafiri walikaa na kulala kwenye sitaha ya meli katika hali yoyote ile ya anga. Sehemu kavu iliyokuwa chini ya sitaha ilijazwa mizigo yenye thamani. Wasafiri walikula chakula walichobeba wenyewe. Walipewa tu maji ya kunywa. Nyakati nyingine, hali ya anga ilibadilika-badilika sana. Dhoruba na mawimbi makali yalisababisha kichefuchefu ambacho mara nyingi kiliendelea kwa muda mrefu.

Ijapokuwa watu waliosafiri baharini au kwenye nchi kavu walipatwa na matatizo mbalimbali, wamishonari kama Paulo walieneza “habari njema ya ufalme” kwa mapana katika ulimwengu uliojulikana siku zao. (Mathayo 24:14) Miaka 30 tu baada ya Yesu kuwaambia wanafunzi wake watoe ushahidi kumhusu, Paulo angeweza kuandika kwamba habari njema ilikuwa ikihubiriwa “katika uumbaji wote ulio chini ya mbingu.”—Wakolosai 1:23.