Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Usahihi wa Biblia Unathibitishwa na Maktaba ya Kale ya Urusi

Usahihi wa Biblia Unathibitishwa na Maktaba ya Kale ya Urusi

Usahihi wa Biblia Unathibitishwa na Maktaba ya Kale ya Urusi

WASOMI wawili wanatafuta hati za kale za Biblia. Kila mmoja anavuka majangwa na kuzitafuta hati hizo katika mapango, makao ya watawa, na nyumba za kale zilizojengwa kwa mawe yaliyochongwa kutoka katika miamba. Miaka mingi baadaye, wanakutana katika maktaba ya kale zaidi ya umma nchini Urusi, ambako kuna baadhi ya hati muhimu zaidi za Biblia. Wasomi hao walikuwa nani? Na hati hizo walizogundua zilifikaje Urusi?

Hati za Kale Zalitetea Neno la Mungu

Mmoja wa wasomi hao aliishi katika miaka ya mapema ya 1800, wakati wa mabadiliko makubwa ya elimu huko Ulaya. Katika kipindi hicho kulikuwa na maendeleo ya kisayansi na ya kijamii ambayo yaliwafanya watu watilie shaka mafundisho ya kale ya dini. Wachambuzi walijaribu kuwachochea watu wasiamini Biblia. Wasomi nao walitilia shaka usahihi wa maandishi ya Biblia.

Watetezi fulani wa Biblia waliokuwa wanyoofu waliamini kwamba hati za kale za Biblia ambazo hazikuwa zimegunduliwa bila shaka zingeonyesha kwamba maandishi ya Neno la Mungu hayajabadilishwa. Ikiwa hati za kale zaidi zingepatikana, bila shaka zingeonyesha waziwazi kwamba maandishi ya Biblia hayakuwa yamebadilishwa, ijapokuwa kwa muda mrefu watu wamejaribu sana kuharibu au kupotosha ujumbe wake. Hati hizo zingeonyesha pia kasoro chache ambazo ziliingizwa wakati wa kunakili Biblia.

Usahihi wa Biblia ulijadiliwa vikali hasa nchini Ujerumani. Profesa mmoja kijana aliyeishi huko aliacha maisha yake ya starehe na elimu na kufunga safari ambayo ilimwezesha kugundua hati muhimu zaidi za Biblia. Aliitwa Konstantin von Tischendorf. Yeye alikuwa msomi wa Biblia aliyepinga uchambuzi wa Biblia na hatimaye akafanikiwa kutetea usahihi wa maandishi ya Biblia. Alipata mafanikio katika safari yake ya kwanza ya kwenda kwenye jangwa la Sinai katika mwaka 1844. Alipochungulia kikapu cha takataka katika makao ya watawa, aliona Septuajinti, ambayo ni tafsiri ya kale ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania. Nakala hiyo aliyopata ndiyo iliyokuwa ya kale zaidi kuwahi kupatikana!

Tischendorf alifurahi sana na akafaulu kupata sehemu 43 za hati hizo za kale. Ijapokuwa alikuwa na hakika kwamba kulikuwa na sehemu nyingine za hati hiyo, alipata tu kipande kidogo aliporudi mwaka wa 1853. Zile sehemu nyingine zilikuwa wapi? Pesa zake zilikuwa zimekwisha na Tischendorf akamwomba tajiri fulani msaada wa kifedha na kuamua kutoka nchi yao tena ili aende akatafute hati nyingine za kale za Biblia. Hata hivyo, kabla ya kufunga safari hiyo akamwomba maliki wa Urusi msaada wa kutimiza mradi huo.

Maliki Aunga Mkono

Yamkini Tischendorf alijiuliza kama yeye aliyekuwa msomi Mprotestanti angekaribishwa nchini Urusi, kwani katika nchi hiyo kubwa watu wengi walikuwa wafuasi wa Kanisa Othodoksi la Urusi. Hata hivyo, mabadiliko makubwa yalikuwa yakitukia nchini Urusi. Elimu ilitiliwa maanani, na katika mwaka wa 1795 Malkia Katerina wa Pili (anaitwa pia Katerina Mkuu) akaanzisha Maktaba ya Milki ya St. Petersburg. Hiyo ilikuwa maktaba ya kwanza ya umma nchini Urusi na iliwawezesha watu wengi sana kusoma vitabu vingi vilivyokuwa huko.

Maktaba hiyo ilionwa kuwa mojawapo ya maktaba bora huko Ulaya, hata hivyo ilikosa kitu fulani. Miaka 50 baada ya kuanzishwa, maktaba hiyo ilikuwa na hati sita tu za kale za Kiebrania. Kwa kuwa watu wengi nchini Urusi walipendezwa na lugha za Biblia na tafsiri zake, hati hizo chache hazingetosheleza tamaa yao. Malkia Katerina wa Pili alikuwa amewapeleka wasomi wakajifunze Kiebrania kwenye vyuo vikuu huko Ulaya. Waliporudi, masomo ya lugha ya Kiebrania yalianzishwa katika seminari za Kanisa Othodoksi la Urusi, na kwa mara ya kwanza, wasomi Warusi wakaanza kutafsiri nakala sahihi ya Biblia katika Kirusi wakitegemea maandishi ya kale ya Kiebrania. Lakini hawakuwa na fedha za kutosha, na viongozi wa kanisa wasiotaka mabadiliko waliwapinga. Wakati wa kuielewa Biblia vizuri haukuwa umefika.

Maliki Aleksanda wa Pili, alielewa upesi umuhimu wa mradi wa Tischendorf na akaamua kumsaidia kifedha. Licha ya “wivu na upinzani” wa watu fulani, Tischendorf alienda Sinai na akarejea akiwa na zile sehemu nyingine za Septuajinti. * Bado hati hiyo ya Septuajinti, ambayo baadaye ilikuja kuitwa Kodeksi ya Sinai, ni mojawapo ya hati za kale zaidi za Biblia ambazo zimewahi kupatikana. Aliporudi St. Petersburg, Tischendorf alienda moja kwa moja kwenye Jumba la Maliki la Majira ya Baridi. Alimpendekezea maliki aunge mkono “mmojawapo wa miradi mikubwa zaidi ya kuchunguza na kujifunza maandishi ya Biblia,” yaani, kutayarisha nakala ya hati hiyo iliyopatikana karibuni na kuichapisha. Baadaye nakala hiyo iliwekwa kwenye Maktaba ya Milki. Maliki alikubali upesi na baadaye Tischendorf aliyekuwa na furaha akaandika hivi: “Kwa mapenzi ya Mungu kizazi chetu kimepewa . . . Biblia ya Sinai ambayo inathibitisha kikamili na waziwazi usahihi wa maandishi ya Neno la Mungu, na kutusaidia kutetea kweli ya Biblia kwa kuonyesha jinsi ilivyokuwa awali.”

Hati Muhimu za Biblia Kutoka Krimea

Kuna msomi mwingine aliyekuwa akitafuta hati za kale za Biblia ambaye alitajwa mapema. Yeye alikuwa nani? Miaka michache kabla Tischendorf hajarudi Urusi, Maktaba ya Milki ilipewa nafasi ya kununua hati nyingi sana, jambo lililompendeza sana maliki na kuwavutia wasomi kutoka sehemu zote za Urusi na Ulaya. Jambo hilo liliwashangaza sana. Waliletewa hati nyingi na vitabu vingine. Maandishi hayo yalikuwa na sehemu mbalimbali 2,412, kutia ndani hati na vitabu vya kukunjwa 975. Kati ya hizo kulikuwa na hati 45 za Biblia zilizoandikwa kabla ya miaka ya 900. Inastaajabisha kwamba hati zote hizo zilikuwa zimekusanywa na mtu mmoja tu aliyeitwa Abraham Firkovich, msomi Mkaraite ambaye wakati huo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 70! Lakini Wakaraite walikuwa nani? *

Hilo lilikuwa jambo muhimu sana kwa Maliki. Urusi ilikuwa imetwaa maeneo yaliyokuwa yakitawaliwa na nchi nyingine. Hivyo, watu wa asili mbalimbali waliishi katika eneo la milki hiyo. Eneo maridadi la Krimea, kwenye pwani ya Bahari Nyeusi, lilikaliwa na watu waliodhaniwa kuwa Wayahudi lakini ambao walikuwa na mila za Waturuki na lugha yao ilifanana na Kitatari. Wakaraite hao walisema kwamba walikuwa wazao wa Wayahudi waliopelekwa uhamishoni huko Babiloni baada ya uharibifu wa Yerusalemu mwaka wa 607 K.W.K. Hata hivyo, tofauti na Wayahudi waliokuwa wafuasi wa dini ya Kiyahudi, walikataa Talmud na kukazia kusoma Maandiko. Wakaraite walioishi Krimea walitaka sana kumwonyesha maliki kwamba wao ni tofauti na Wayahudi waliokuwa wafuasi wa dini ya Kiyahudi, na hivyo walitarajia kupata kibali cha kipekee. Wakaraite walifikiri kwamba kwa kumpa Maliki hati za kale walizokuwa nazo wangemthibitishia kwamba walikuwa wazao wa Wayahudi waliokuwa wamehamia Krimea baada ya kutoka uhamishoni huko Babiloni.

Firkovich alianza kutafuta maandishi na hati za kale katika nyumba zilizojengwa kwa mawe yaliyochongwa katika miamba huko Chufut-Kale, Krimea. Wakaraite walikuwa wameishi na kuabudu katika nyumba hizo ndogo kwa miaka mingi. Wakaraite hawakuharibu kamwe nakala zilizochakaa za Maandiko zilizokuwa na jina la Mungu, Yehova, kwa sababu waliona hilo kuwa tendo la kufuru. Hati zilizochakaa zilihifadhiwa katika ghala ndogo kwenye sinagogi lililoitwa geniza, ambalo ni neno la Kiebrania linalomaanisha “maficho.” Wakaraite hawakuziharibu hati hizo kamwe kwa sababu waliliheshimu sana jina la Mungu.

Ingawa hati hizo zilifunikwa kwa mavumbi kwa karne nyingi, Firkovich aliyachunguza maghala hayo kwa makini. Katika ghala moja alipata hati maarufu ya mwaka wa 916 W.K. Hati hiyo inaitwa Kodeksi ya Petersburg ya Manabii wa Mwisho nayo ni mojawapo ya nakala za kale zaidi za Maandiko ya Kiebrania.

Firkovich alikusanya hati nyingi sana na mwaka wa 1859 akaamua kuiuzia Maktaba ya Milki hati hizo. Mwaka wa 1862, Aleksanda wa Pili alisaidia kununua hati hizo kwa ajili ya maktaba hiyo kwa gharama kubwa sana, yaani rubo 125,000. Wakati huo gharama ya kuendesha maktaba hiyo haikuzidi rubo 10,000 kwa mwaka! Kodeksi ya Leningrad (B 19A) inayojulikana sana ilikuwa kati ya hati hizo zilizonunuliwa. Hati hiyo iliyoandikwa mwaka wa 1008 hivi ni nakala ya kale zaidi ya Maandiko yote ya Kiebrania. Msomi mmoja alisema kwamba “huenda hiyo ndiyo hati ya Biblia iliyo muhimu kuliko hati nyingine zote kwa sababu chapa nyingi za kisasa za Biblia ya Kiebrania zenye nyongeza zinategemea hati hiyo.” (Ona sanduku.) Mwaka huohuo, yaani 1862, Kodeksi ya Sinai ya Tischendorf ilichapishwa nayo ikasifiwa sana ulimwenguni.

Elimu ya Kiroho Leo

Maktaba inayoitwa sasa Maktaba ya Kitaifa ya Urusi ni mojawapo ya maktaba zilizo na hati nyingi zaidi za kale. * Jina la maktaba hiyo limebadilishwa mara saba katika kipindi cha miaka mia mbili iliyopita kupatana na mabadiliko nchini Urusi. Jina moja linalojulikana sana ni Maktaba ya Umma ya Kitaifa ya Saltykov-Shchedrin. Ijapokuwa maktaba hiyo imeharibiwa kwa kadiri fulani katika misukosuko ya karne ya 20, hati zake hazikuharibiwa katika vile vita viwili vya ulimwengu wala wakati Leningrad lilipozingirwa. Lakini, hati hizo zinatunufaishaje?

Hati za kale ndizo msingi unaotegemeka wa tafsiri nyingi za Biblia za kisasa. Zinawawezesha watu wanaotaka kujua kweli kusoma tafsiri sahihi za Maandiko Matakatifu. Kodeksi ya Sinai na ya Leningrad zilitumiwa sana katika kazi ya kutafsiri Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Kiingereza, iliyochapishwa na kutolewa na Mashahidi wa Yehova mwaka wa 1961. Kwa mfano, Biblia Hebraica Stuttgartensia na Biblia Hebraica ya Kittel ambazo zilitumiwa na Halmashauri ya Kutafsiri Biblia ya Ulimwengu Mpya zinategemea Kodeksi ya Leningrad inayotaja jina la Mungu mara 6,828 katika maandishi ya awali.

Wasomaji wachache tu wa Biblia ndio wanaojua kwamba wanafaidika sana na maktaba ya St. Petersburg na hati zake, ambazo baadhi yake zinaitwa kwa jina la zamani la jiji hilo, Leningrad. Tunapaswa kumshukuru sana Mtungaji wa Biblia, Yehova, ambaye hutoa nuru ya kiroho. Mtunga-zaburi alimsihi hivi: “Tuma nuru yako na kweli yako. Na hivyo vyenyewe viniongoze.”—Zaburi 43:3.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Alirejea akiwa pia na nakala ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ya miaka ya 300 W.K.

^ fu. 13 Unaweza kupata habari zaidi kuwahusu Wakaraite katika makala “Wakaraite na Utafutaji Wao wa Kweli,” kwenye Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 1995.

^ fu. 19 Sehemu nyingi za Kodeksi ya Sinai zilinunuliwa na Jumba la Makumbusho la Uingereza. Kuna vipande vichache tu katika Maktaba ya Kitaifa ya Urusi.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

JINA LA MUNGU LILIJULIKANA NA KUTUMIWA

Kwa hekima yake, Yehova amehakikisha kwamba Neno lake Biblia limehifadhiwa hadi wakati wetu. Waandishi wenye bidii wamefanya mengi ili kuihifadhi. Wamasora ndio waliokuwa waandishi makini zaidi. Wao walikuwa wanakili stadi Waebrania waliokuwa wakifanya kazi ya kunakili kati ya miaka ya 500 na 900 W.K. Maandishi ya kale ya Kiebrania hayakuwa na irabu. Kwa hiyo baada ya muda matamshi sahihi yangeweza kusahauliwa watu walipoanza kuongea Kiaramu badala ya Kiebrania. Wamasora walibuni mfumo wa alama za irabu na kuzitia katika maandishi ya Biblia ili kuonyesha matamshi sahihi ya maneno ya Kiebrania.

Ni jambo la kupendeza kwamba alama za irabu katika Kodeksi ya Leningrad zinaonyesha njia tatu za kutamka jina la Mungu katika Kiebrania, yaani, Yehwah’, Yehwih’, na Yeho·wah’. Sasa watu wengi sana wanalitamka “Yehova.” Waandishi wa Biblia na watu wengine wa enzi za kale walijua na kulitumia jina la Mungu. Leo, watu wanaolijua na kutumia jina la Mungu hutambua kwamba ‘Yehova, pekee ndiye Aliye Juu Zaidi, juu ya dunia yote.’—Zaburi 83:18.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Chumba cha hati za kale katika Maktaba ya Kitaifa

[Picha katika ukurasa wa 11]

Malkia Katerina wa Pili

[Picha katika ukurasa wa 11]

Konstantin von Tischendorf (katikati) na maliki wa Urusi, Aleksanda wa Pili

[Picha katika ukurasa wa 12]

Abraham Firkovich

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Both images: National Library of Russia, St. Petersburg

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 11]

Catherine II: National Library of Russia, St. Petersburg; Alexander II: From the book Spamers Illustrierte Weltgeschichte, Leipzig, 1898