Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tumaini Licha ya Shida Kusanyiko Katika Kambi ya Wakimbizi

Tumaini Licha ya Shida Kusanyiko Katika Kambi ya Wakimbizi

Tumaini Licha ya Shida Kusanyiko Katika Kambi ya Wakimbizi

KAMBI ya wakimbizi ya Kakuma iko kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka wa Sudani. Zaidi ya watu 86,000 huishi huko. Hilo ni eneo kavu, na wakati wa mchana halijoto hufikia nyuzi 50 Selsiasi. Jamii mbalimbali za wakimbizi huzozana mara nyingi. Wakimbizi wengi hupata shida nyingi kambini. Hata hivyo, wengine wao wana tumaini.

Baadhi ya wakimbizi ni Mashahidi wa Yehova, na wanahubiri habari njema za Ufalme kwa bidii. Wanashirikiana na kutaniko dogo huko Lodwar, kilometa 120 kusini mwa kambi hiyo. Ili ufike kwenye kutaniko lililo karibu na lile la Lodwar, itakubidi usafiri kwa gari kwa muda wa saa nane.

Kwa kuwa wakimbizi hao hawawezi kutoka nje ya kambi kwa urahisi, wengi wao hawawezi kuhudhuria makusanyiko ya Mashahidi wa Yehova. Kwa hiyo, mipango ilifanywa kuwe na kusanyiko la pekee ndani ya kambi.

Kusafiri Kwenda Kaskazini

Ili kufanikisha kusanyiko hilo, Mashahidi 15 kutoka mji wa Eldoret, ambao uko kilometa 480 kusini mwa kambi hiyo, walijitolea kufunga safari ngumu ya kwenda kaskazini. Waliambatana na mwanafunzi mmoja wa Biblia aliyekubali gari lake litumiwe na kuendeshwa na dereva wake. Mashahidi hao walitaka kuwatia moyo na kuwaimarisha ndugu zao.

Safari ilianza mapema asubuhi katika maeneo ya milimani yaliyo magharibi mwa Kenya, huku kukiwa na baridi. Walipitia barabara mbovu iliyopita katikati ya mashamba na misitu kabla ya kuteremka kwenye jangwa lenye joto na lenye vichaka. Mbuzi na ngamia walikuwa wakilisha kwenye eneo hilo kame. Wenyeji walivalia nguo zao za kitamaduni, na wengi wao walibeba marungu, nyuta, na mishale. Baada ya kusafiri kwa saa 11, Mashahidi hao walifika Lodwar, eneo lenye joto na vumbi ambalo lina wakaaji 20,000 hivi. Walipokewa kwa uchangamfu na Mashahidi wa huko, kisha wakapumzika ili wawe tayari kwa ajili ya shughuli za mwisho wa juma.

Asubuhi iliyofuata, wageni hao walitembelea sehemu za pekee za eneo hilo. Bila shaka, hawangekosa kutembelea Ziwa Turkana, ambalo ndilo ziwa kubwa zaidi nchini Kenya. Limezingirwa na jangwa lenye vichaka vingi nalo ndilo lenye mamba wengi zaidi ulimwenguni. Maji yake ya chumvi huwasaidia watu wachache wanaoishi karibu nalo kupata riziki. Jioni hiyo wageni walifurahia kuhudhuria Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na Mkutano wa Utumishi katika kutaniko la huko. Kutaniko hilo lina Jumba la Ufalme lenye kupendeza ambalo lilijengwa mwaka wa 2003 kupitia mpango wa ujenzi wa kusaidia nchi zenye matatizo ya kiuchumi.

Kusanyiko la Pekee

Kusanyiko la pekee lilifanywa Jumapili. Kutaniko la Lodwar, na ndugu waliowatembelea, waliruhusiwa kuingia kambini kufikia saa mbili asubuhi kwa hiyo Mashahidi hao waliamua kuanza safari mapema. Walisafiri kwenye barabara yenye kujipinda-pinda iliyopita jangwani ikielekea mpaka wa Sudani. Kando ya barabara hiyo kulikuwa na milima iliyochongoka. Walipofika kijiji cha Kakuma, mandhari yakawa wazi zaidi. Mvua ilikuwa imenyesha na sehemu fulani za barabara ya vumbi inayoelekea kambini zilijaa maji. Nyumba nyingi zilikuwa za udongo na ziliezekwa paa la mabati au turubai. Waethiopia, Wasomali, Wasudani, na watu wengineo huishi katika maeneo yao. Wakimbizi waliwasalimu kwa uchangamfu wasafiri hao.

Kusanyiko lilifanywa kwenye kituo cha elimu. Michoro kwenye ukuta inaonyesha shida ambazo wakimbizi hukabili, lakini watu waliokuwa ndani ya jumba hilo siku hiyo walikuwa na nyuso zenye tumaini. Hotuba zote zilitolewa katika Kiingereza na Kiswahili. Hata wasemaji fulani ambao wanazungumza lugha hizo mbili vizuri walitafsiri hotuba zao. Ndugu mmoja kutoka Sudani ambaye ni mkimbizi alitoa hotuba ya kwanza yenye kichwa, “Kuuchunguza Moyo Wetu wa Mfano.” Hotuba nyingine zilitolewa na wazee waliotembelea eneo hilo.

Ubatizo huwa sehemu ya pekee ya kila kusanyiko. Baada ya hotuba ya ubatizo, mtu mmoja tu, anayeitwa Gilbert, ndiye aliyekuwa tayari kubatizwa, na wote walimkazia macho aliposimama. Gilbert alikimbia pamoja na baba yake kutoka nchi ya kwao wakati wa yale mauaji makubwa ya mwaka wa 1994. Mwanzoni, walifikiria wangekuwa salama Burundi, lakini wakatambua kwamba bado walikuwa hatarini. Gilbert alikimbilia Zaire, kisha Tanzania, na akiwa huko alijificha msituni nyakati nyingine. Mwishowe alifika Kenya. Wengi walitokwa na machozi wakati msemaji alipomkaribisha awe ndugu katika kutaniko. Gilbert alisimama mbele ya kusanyiko hilo la watu 95 na kujibu waziwazi na kwa uhakika “Ndiyo!,” alipoulizwa na msemaji maswali mawili. Gilbert na ndugu wengine walikuwa wamechimba shimo na kutandaza turubai ambalo hapo awali lilikuwa paa ya makao yake kambini. Asubuhi hiyohiyo, Gilbert alikuwa ameonyesha kwamba anatamani sana kubatizwa kwa kujaza maji ndani ya shimo hilo yeye mwenyewe!

Mojawapo ya mambo ya pekee katika kipindi cha alasiri ni masimulizi kuhusu hali ya pekee ambayo Mashahidi wakimbizi wanakabili. Ndugu mmoja alieleza jinsi alivyozungumza na mtu aliyekuwa akipumzika chini ya mti.

“Hebu niambie, je, ni salama kila wakati kuketi chini ya mti?”

“Ndiyo,” mtu huyo akajibu. Kisha akasema, “Lakini, si salama kufanya hivyo usiku.”

Ndugu huyo alimsomea Mika 4:3, 4: “Wataketi, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.” Kisha ndugu huyo akasema, “Unaona, katika ulimwengu mpya wa Mungu, itakuwa salama kila wakati kuketi chini ya mti.” Mtu huyo alikubali kupokea kichapo kinachoifafanua Biblia.

Dada mmoja aliyesafiri kwenda Kakuma alikuwa amefiwa na watu watatu wa karibu wa familia yake muda mfupi kabla ya wakati huo. Alisema hivi kuhusu ndugu hao wanaoishi kambini: “Huku kuna shida nyingi, lakini wana imani yenye nguvu. Ijapokuwa wanaishi katika mazingira yenye kuhuzunisha, wanamtumikia Yehova kwa furaha. Wana amani pamoja na Mungu. Nilitiwa moyo kuwa na amani na kumtumikia Yehova. Sipaswi kulalamika!”

Siku hiyo ya kusanyiko ilikwisha haraka sana. Katika hotuba ya mwisho, msemaji alitaja kwamba kusanyiko hilo lilihudhuriwa na watu kutoka nchi nane. Shahidi mmoja ambaye ni mkimbizi alisema kwamba kusanyiko hilo linaonyesha umoja na upendo uliopo miongoni mwa Mashahidi wa Yehova katika ulimwengu uliogawanyika. Kwa wazi, wana undugu wa kweli wa Kikristo.—Yohana 13:35.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

WAVULANA WALIOPOTEA WA SUDANI

Tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vianze nchini Sudani katika mwaka wa 1983, watu milioni tano wamelazimika kuhama makwao. Idadi hiyo inatia ndani wavulana 26,000 waliotenganishwa na familia zao. Maelfu ya wavulana hao walikimbilia kambi za wakimbizi nchini Ethiopia, ambako walikaa kwa miaka mitatu hivi. Walipolazimika kuhama tena, walitembea kwa mwaka mmoja kupitia Sudani kisha wakafika kaskazini mwa Kenya, na walishambuliwa na askari, wavamizi, wanyama wa pori, na magonjwa. Nusu yao tu ndio waliookoka safari hizo ngumu, na kuwa kati ya watu wa kwanza kwenye kambi ya Kakuma. Mashirika ya misaada huwaita, wavulana waliopotea wa Sudani.

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma imekuwa makao ya watu wa mataifa mbalimbali kama vile Sudani, Somalia, Ethiopia, na mengineyo. Mkimbizi anapofika kwenye kambi hiyo, yeye hupewa vifaa vya msingi vya kujengea mahali pa kukaa na turubai ya kuezekea paa. Mara mbili kwa mwezi, kila mkimbizi hupewa kilo sita hivi za unga, kilo moja ya maharagwe, na mafuta kidogo. Wakimbizi wengi huuza sehemu fulani ya posho yao ili wanunue vitu vingine vya msingi.

Baadhi ya wavulana hao wameunganishwa tena na familia zao au kupewa makao katika nchi nyingine. Lakini kulingana na Shirika la Kuwatafutia Wakimbizi Makao, “maelfu ya wavulana hao wamebaki katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma iliyo na vumbi na nzi wengi sana, ambako wamelazimika kutafuta chakula kwa shida na kujitahidi sana kupata elimu.”

[Hisani]

Courtesy Refugees International

[Ramani katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KENYA

Kambi ya Kakuma

Ziwa Turkana

Lodwar

Eldoret

Nairobi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Maisha ni magumu kambini

[Picha katika ukurasa wa 23]

Maji yapimwa katika kambi ya Kakuma

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mashahidi Wakenya wakifunga safari ngumu kuelekea kaskazini ili kuwatia moyo ndugu zao

[Picha katika ukurasa wa 24]

Mmishonari akitafsiri hotuba inayotolewa na painia wa pekee wa eneo hilo

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kidimbwi cha ubatizo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Rationing water and Kakuma Refugee Camp: Courtesy Refugees International