Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutafuta Viongozi Wazuri

Kutafuta Viongozi Wazuri

Kutafuta Viongozi Wazuri

“Nasema ondoka, hatukutaki tena. Kwa jina la Mungu, ondoka!”—Maneno ya Oliver Cromwell; yaliyonukuliwa na Leopold Amery, Mbunge wa Bunge la Uingereza.

Vita vya Pili vya Ulimwengu vilikuwa vimeendelea kwa miezi minane, vilikuwa vikisababisha uharibifu mwingi na ilionekana kwamba Uingereza na washirika wake wangeshindwa katika vita hivyo. Leopold Amery na wengine serikalini, waliona kwamba kulikuwa na uhitaji wa kiongozi mwingine. Hivyo, Mei 7, 1940, katika Bunge la Wawakilishi la Uingereza, Bw. Amery alinukuu maneno yaliyotajwa juu kwa Waziri Mkuu Neville Chamberlain. Siku tatu baadaye, Bw. Chamberlain aliacha kazi na mahali pake pakachukuliwa na Winston Churchill.

WANADAMU wana uhitaji wa msingi wa kuwa na kiongozi, lakini si kiongozi yeyote tu. Hata katika familia, baba anapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza, ili mke na watoto wake wawe wenye furaha. Basi wazia jinsi mengi zaidi yanavyotakiwa kwa kiongozi wa nchi au wa ulimwengu! Haishangazi kwamba imekuwa vigumu sana kupata viongozi wazuri.

Hivyo, kwa miaka mingi, kumekuwa na maasi, mapinduzi, uteuzi, uchaguzi, mauaji ya kisiasa, wengi wametawazwa, na pia mabadiliko ya serikali. Wafalme, mawaziri wakuu, wakuu, marais, makatibu wakuu, na madikteta wamechaguliwa na kuondolewa. Hata viongozi wenye nguvu wameondolewa mamlakani baada ya mabadiliko yasiyotarajiwa kutokea. (Ona sanduku “Kuondolewa Mamlakani kwa Ghafula,” kwenye ukurasa wa 5.) Hata hivyo, imekuwa vigumu kupata viongozi hodari na wenye kudumu.

‘Hatuna la Kufanya’ —Lazima Tuvumilie Tu

Kwa hiyo, haishangazi kwamba wengi wamepoteza kabisa tumaini la kupata viongozi wazuri. Katika nchi fulani, hisia za watu za kuwa wenye ubaridi na kukata tamaa huonekana hasa wakati wa uchaguzi. Geoff Hill, mwandishi-habari barani Afrika alisema hivi: “Kunakuwa na hali ya ubaridi au ya kususia [kupiga kura] watu wanapohisi kuwa hawana nguvu za kubadili hali yao mbaya maishani . . . Barani Afrika, watu wanapokosa kupiga kura, haimaanishi kwamba wameridhika. Mara nyingi, hicho ni kilio cha watu wanaohisi kwamba hakuna anayejali shida zao.” Vivyo hivyo, mwandishi mmoja wa gazeti huko Marekani aliandika hivi kuhusu uchaguzi uliokuwa ukikaribia: “Laiti tungekuwa na mgombezi bora kabisa wa kiti hiki.” Aliongeza kusema: “Hakuna mgombezi kama huyo. Hayuko kabisa. Lazima tuvumilie tu.”

Je, ni kweli kwamba mwanadamu hana la kufanya, ila kuvumilia tu viongozi wasio wakamilifu? Kwa kuwa viongozi wa kibinadamu wameshindwa kutosheleza mahitaji ya raia zao, je, hilo linathibitisha kwamba hatutapata kuwa na viongozi wazuri? La. Kuna kiongozi bora kabisa. Makala inayofuata itazungumza juu ya kiongozi huyo wa wanadamu aliye bora na jinsi uongozi wake unavyoweza kunufaisha mamilioni ya watu wa malezi yote—kutia ndani wewe.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Juu kushoto: Neville Chamberlain

Juu kulia: Leopold Amery

Chini: Winston Churchill

[Hisani]

Chamberlain: Photo by Jimmy Sime/Central Press/Getty Images; Amery: Photo by Kurt Hutton/Picture Post/Getty Images; Churchill: The Trustees of the Imperial War Museum (MH 26392)