Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Visagio Vilivyofanya Chakula Kipatikane

Visagio Vilivyofanya Chakula Kipatikane

Visagio Vilivyofanya Chakula Kipatikane

MKATE umetajwa kuwa ‘chakula chenye kutegemeza uhai,’ “chakula kikuu kati ya vyakula vyote,” “chakula ambacho kimemtegemeza mwanadamu tangu zamani za kale.” Naam, tangu zamani mkate umekuwa chakula kikuu. Hata mojawapo ya mahitaji muhimu zaidi ya mwanadamu ni kupata mkate wake wa kila siku.

Unga ambao hupatikana kwa kusaga nafaka, ndio kichanganyiko kikuu cha kutengeneza mkate. Kwa hiyo, kusaga ni ufundi wa zamani. Kwa kweli, ilikuwa kazi ngumu sana kusaga nafaka iwe unga bila mashini. Nyakati za Biblia, sauti ya kisagio cha mkononi ilihusianishwa na hali za kawaida zenye amani, lakini ukosefu wa sauti hiyo ulionyesha hali ya ukiwa.—Yeremia 25:10, 11.

Kusaga kumehusisha nini katika enzi ambazo zimepita? Ni njia na vifaa vipi ambavyo vimetumiwa kusagia? Na ni visagio vya aina gani vinavyokuwezesha kupata chakula leo?

Kwa Nini Visagio Vilihitajiwa?

Yehova aliwaambia hivi wanadamu wawili wa kwanza, Adamu na Hawa: “Tazama nimewapa mimea yote inayozaa mbegu iliyo juu ya uso wa dunia yote na kila mti ambao una matunda ya mti unaozaa mbegu. Na iwe chakula kwenu.” (Mwanzo 1:29) Nafaka ilikuwa mojawapo ya vyakula ambavyo Yehova Mungu aliwapa wanadamu. Chakula hicho kilikuwa muhimu ili mwanadamu aendelee kuishi, kwakuwa nafaka zote—kutia ndani ngano, shayiri, rai, mchele, mtama, na mahindi—zina wanga ambao mwili unaweza kuugeuza kuwa namna ya sukari ambayo ndiyo chanzo kikuu cha nguvu mwilini.

Hata hivyo, mwanadamu hana uwezo wa kumeng’enya nafaka nzima-nzima ambazo hazijapikwa. Ni rahisi zaidi kuzila zikiwa zimesagwa na kupikwa. Njia zilizo rahisi zaidi za kusaga kiasi kikubwa cha nafaka kuwa unga ni kuzitwanga ndani ya kinu, kuziponda katikati ya mawe mawili, au kutumia njia zote mbili.

Visagio Vilivyoendeshwa na Mwanadamu

Sanamu ndogo katika makaburi ya Misri ya kale inaonyesha aina moja ya kisagio cha nafaka cha zamani kinachofanana na tandiko la farasi. Kisagio hicho kilitia ndani mawe mawili—chini kulikuwa na jiwe moja lenye mbonyeo kidogo ambalo liliinama upande mmoja, na juu kulikuwa na jiwe lingine dogo. Mwenye kusaga, ambaye kwa kawaida alikuwa mwanamke, alipiga magoti nyuma ya kifaa hicho na kulishika jiwe la juu kwa mikono yote miwili. Kisha uzito wote wa sehemu ya juu ya mwili wake ukiwa juu ya jiwe hilo, alilisukuma mbele na nyuma juu ya lile jiwe kubwa la chini, akiponda nafaka katikati ya mawe hayo mawili. Hicho kilikuwa kifaa rahisi lakini chenye matokeo kama nini!

Lakini kupiga magoti kwa muda mrefu kulikuwa na madhara yake. Kulisukuma jiwe la juu hadi mwisho kisha kulivuta nyuma tena kulitia mkazo mkubwa mno kwenye mgongo, mikono, mapaja, magoti, na vidole vya miguu vya mwenye kusaga. Uchunguzi kuhusu mifupa yenye kasoro kutoka Siria ya kale umefanya wataalamu wa visukuku wakate kauli kwamba kutumia vifaa hivyo kulifanya wanawake vijana wapatwe na majeraha yanayosababishwa na kufanya tena na tena kitu kinachotia mkazo sehemu fulani ya mwili. Majeraha hayo ni kubonyea kwa pia za magoti, madhara katika sehemu ya chini ya uti wa mgongo, na kuharibika vibaya kwa mifupa ya kidole kikubwa cha mguu. Katika Misri ya kale, wajakazi ndio waliofanya kazi ya kusaga. (Kutoka 11:5) * Wasomi fulani wanaamini kwamba Waisraeli walipoondoka Misri, walibeba kisagio hicho kinachofanana na tandiko la farasi.

Kuboreshwa kwa visagio kulitia ndani kuchonga mistari kwenye mawe yote mawili ili yasage vizuri zaidi. Kutoboa tundu katikati ya jiwe la juu kulimwezesha mwenye kusaga kulijaza nafaka, ambayo ilitiririka yenyewe katikati ya mawe hayo mawili. Katika karne ya nne na ya tano K.W.K., Wagiriki walibuni mashini rahisi ya kusagia. Mpini wa mlalo, au wenzo, ambao upande mmoja ulizunguka katika kiegemeo, uliunganishwa na jiwe la juu. Kwa kusukuma upande ule mwingine wa mpini mbele na nyuma, kulifanya jiwe la juu lenye tundu la kuwekea nafaka lisugue lile la chini.

Visagio vyote ambavyo vimetangulia kutajwa vilikuwa na shida moja kubwa. Vilihitaji kusukumwa mbele na nyuma na hakuna mnyama ambaye angeweza kuzoezwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, mwanadamu tu ndiye angeweza kuendesha visagio hivyo. Ndipo kukabuniwa kifaa kipya cha kusagia, yaani, kisagio cha kuzungushwa. Sasa wanyama wangeweza kutumiwa kukiendesha.

Visagio vya Kuzungushwa Vyarahisisha Kazi

Ingawa vyanzo vya habari vinatofautiana, yaelekea kwamba kisagio cha kuzungushwa kilibuniwa katika bonde la Mediterania yapata karne ya pili K.W.K. Kufikia karne ya kwanza W.K., Wayahudi huko Palestina walijua visagio hivyo, kwa kuwa Yesu alitaja “jiwe la kusagia kama lile ambalo huzungushwa na punda.”—Marko 9:42.

Kisagio kilichozungushwa na mnyama kilitumiwa huko Roma na katika sehemu nyingi za Milki ya Roma. Visagio vingi kama hivyo bado vinapatikana huko Pompeii. Visagio hivyo vimefanyizwa kwa jiwe kubwa la juu linalofanana na chupa ya mchanga ya kuhesabia wakati, nalo lilitumiwa kuwekea nafaka. Jiwe la chini lilifanana na pia. Jiwe la juu lilipozunguka juu ya jiwe la chini, nafaka ziliingizwa katikati ya mawe hayo mawili na kupondwa-pondwa. Mawe ya juu ya aina hiyo yanayopatikana leo yana ukubwa unaotofautiana—yana kipenyo kati ya sentimeta 45 hadi 90. Visagio hivyo hata vilifikia urefu wa sentimeta 180.

Haijulikani kabisa kama kisagio chepesi kilichozungushwa kwa mkono kilitokana na kile kilichozungushwa na wanyama, au vinginevyo. Vyovyote vile, kisagio kilichozungushwa kwa mkono kilikuwa na manufaa kwa kuwa kingeweza kubebwa na kilikuwa rahisi kutumiwa. Kisagio hicho kilitengenezwa kwa mawe mawili ya mviringo yenye kipenyo kati ya sentimeta 30 hadi 40. Sehemu ya juu ya jiwe la chini ilikuwa imebenuka kidogo, nayo sehemu ya chini ya jiwe la juu ilikuwa imebonyea kidogo ili mawe hayo mawili yaingiane vizuri. Jiwe la juu lilikuwa na kiegemeo kilichokuwa katikati, nalo lilizungushwa kwa kutumia mpini wa mbao. Kwa kawaida, wanawake wawili waliketi wakiangaliana, na kila mmoja alishika upande mmoja wa mpini huo ili kulizungusha jiwe la juu. (Luka 17:35) Kwa mkono ule mwingine, mwanamke mmoja aliweka nafaka kidogo-kidogo kwenye tundu lililokuwa katika jiwe la juu, huku mwenzake akikusanya unga uliotiririka kando-kando ya mawe hayo na kuuweka kwenye sinia au kipande cha nguo kilichotandazwa chini ya kisagio. Kisagio kama hicho kilitimiza mahitaji ya askari, mabaharia, na jamaa ndogo-ndogo zilizoishi mbali na sehemu za kusagia.

Vyaendeshwa kwa Maji au Upepo

Yapata mwaka wa 27 K.W.K., injinia Mroma Vitruvius alifafanua kisagio kilichoendeshwa kwa maji katika siku zake. Maji yaliyotiririka yalisukuma makasia ya gurudumu lililokuwa wima, na ambalo lilikuwa na mpini wa mlalo katikati, na hivyo kulifanya lizunguke. Gia zilizokuwa kwenye gurudumu hilo zilizungusha mwimo uliokuwa wima, nao ukazungusha jiwe kubwa la juu la kusagia.

Kiasi cha unga ambacho kisagio hicho kilichoendeshwa kwa maji kingeweza kusaga kinalinganaje na cha visagio vingine? Inakadiriwa kwamba visagio vya mkononi vilisaga nafaka inayopungua kilogramu 10 kwa saa moja, navyo visagio bora zaidi vilivyoendeshwa na wanyama vikasaga kilogramu 50 za nafaka. Kwa upande mwingine, kisagio cha Vitruvius kilichoendeshwa kwa maji, kilikuwa na uwezo wa kusaga kilogramu 150 hadi 200 hivi kwa saa. Baada ya kurekebishwa na kuboreshwa mara nyingi, kanuni ya msingi ambayo ilifafanuliwa na Vitruvius iliendelea kutumiwa kwa karne nyingi baadaye na mafundi wenye ustadi wa vifaa vya kusagia.

Kulikuwa na vyanzo vingine vya nguvu za asili za kuendesha visagio mbali na maji yaliyotiririka. Hata kama magurudumu yaliyoendeshwa kwa maji yangeacha kutumiwa na badala yake kutumia visagio vilivyoendeshwa kwa upepo, bado matokeo yangekuwa ni yaleyale. Visagio vilivyoendeshwa kwa upepo vilianza kutumiwa Ulaya yapata karne ya 12 W.K., navyo vilitumiwa sana huko Ubelgiji, Ujerumani, Uholanzi, na kwingineko. Hatua kwa hatua, visagio hivyo viliacha kutumiwa wakati visagio vilivyoendeshwa kwa mvuke na nguvu nyingine vilipoanza kutumiwa.

“Mkate Wetu kwa Ajili ya Siku Hii”

Licha ya maendeleo ambayo yamefanywa, bado njia nyingi za kusaga za zamani zinatumiwa katika sehemu fulani duniani. Kinu na mchi bado zinatumiwa katika sehemu fulani barani Afrika na Visiwa vya Bahari ya Pasifiki. Huko Mexico na Amerika ya Kati, visagio vinavyofanana na tandiko la farasi hutumiwa kusagia mahindi ya kupikia keki. Navyo visagio vinavyoendeshwa kwa maji au upepo bado vinatumiwa katika sehemu mbalimbali.

Hata hivyo, leo katika nchi zilizoendelea unga mwingi unaotumiwa kuoka mikate husagwa kwa mashini za kusaga ambazo hujiendesha zenyewe. Nafaka husagwa hatua kwa hatua na kuwa unga zinapopondwa tena na tena katikati ya silinda za chuma cha pua zilizochongwa mistari ambazo huzunguka kwa mwendo unaotofautiana. Mfumo huo hufanya iwezekane kusaga unga wa gredi mbalimbali kwa gharama ya chini.

Bila shaka, kupata unga wa kuokea hakuchoshi sana kama zamani. Hata hivyo, tunaweza kumshukuru Muumba wetu kwa kutupatia nafaka na maarifa ya kuzibadili ziwe “mkate wetu kwa ajili ya siku hii.”—Mathayo 6:11.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 10 Katika nyakati za Biblia, maadui waliotekwa, kama vile Samsoni na Waisraeli wengine, walipewa kazi ya kusaga. (Waamuzi 16:21; Maombolezo 5:13) Wanawake waliokuwa huru walisaga nafaka kwa ajili ya jamaa zao.—Ayubu 31:10.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kisagio cha Wamisri kilichofanana na tandiko la farasi

[Hisani]

Soprintendenza Archeologica per la Toscana, Firenze

[Picha katika ukurasa wa 23]

Visagio vilivyozungushwa na wanyama vilitumiwa kushinikiza zeituni ili kupata mafuta

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]

From the Self-Pronouncing Edition of the Holy Bible, containing the King James and the Revised versions