Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mkataba wa Amani wa Westphalia Waleta Mabadiliko Makubwa Ulaya

Mkataba wa Amani wa Westphalia Waleta Mabadiliko Makubwa Ulaya

Mkataba wa Amani wa Westphalia Waleta Mabadiliko Makubwa Ulaya

“BILA shaka, si jambo la kawaida kwa wakuu wengi hivi wa Serikali za Ulaya kukutana pamoja kama ambavyo wamefanya leo.” Maneno hayo yalisemwa mnamo Oktoba 1998 na Roman Herzog, aliyekuwa rais wa Serikali ya Shirikisho ya Ujerumani. Alisema maneno hayo mbele ya wafalme wanne, malkia wanne, wana wawili wa wafalme, mkuu mmoja, na marais kadhaa. Mkutano huo uliogharimiwa na Baraza la Ulaya, ulikuwa muhimu sana katika historia ya miaka 50 ya taifa la kisasa la Ujerumani. Walikutana kwa kusudi gani?

Mnamo Oktoba, 1998, miaka 350 ilikuwa imepita tangu Mkataba wa Amani wa Westphalia utiwe sahihi. Mara nyingi mikataba ya amani inapofanywa maamuzi muhimu hufanywa ambayo yataathiri sana historia, na kwa sababu hiyo, Mkataba wa Amani wa Westphalia ulikuwa wa kipekee. Kutiwa sahihi kwa mkataba huo mwaka wa 1648 kulikomesha Vita vya Miaka Thelathini na kuanzisha nchi huru zinazofanyiza bara la Ulaya la kisasa.

Mfumo wa Zamani Wabadilishwa

Katika Enzi za Kati, Kanisa Katoliki na Milki Takatifu ya Roma ndizo zilizokuwa zenye nguvu zaidi barani Ulaya. Milki hiyo ilikuwa na mamia ya majimbo yenye ukubwa mbalimbali, na eneo la majimbo hayo sasa linafanyiza Austria, Jamhuri ya Cheki, Ufaransa mashariki, Ujerumani, Uswisi, Nchi za Nyanda za Chini za Ulaya Magharibi, na maeneo fulani ya Italia. Kwa kuwa Ujerumani ndiyo iliyokuwa na majimbo mengi zaidi katika milki hiyo, baadaye milki hiyo iliitwa Milki Takatifu ya Roma ya Taifa la Ujerumani. Kila jimbo lilikuwa na uhuru wa kadiri fulani wa kujitawala chini ya mkuu. Maliki alikuwa Mkatoliki wa familia ya Habsburg ya Austria. Hivyo, Ulaya ilidhibitiwa kabisa na Kanisa Katoliki kwa kuwa mamlaka yalikuwa mikononi mwa papa na milki hiyo.

Hata hivyo, katika karne ya 16 na ya 17, mfumo uliokuwako ulibadilishwa. Barani Ulaya, watu wengi walichukizwa na maovu ya Kanisa Katoliki. Waleta-mageuzi wa kidini kama vile Martin Luther na John Calvin walizungumza kuhusu kurudia viwango vya Biblia. Luther na Calvin waliungwa mkono na watu wengi, na katika harakati zao za kuleta mabadiliko, Mageuzi Makubwa ya Kidini yakatokea na vilevile dini za Kiprotestanti. Mageuzi hayo yalifanya kuwe na vikundi vitatu vya kidini—Katoliki, Walutheri, na wafuasi wa Calvin.

Wakatoliki hawakuwaamini Waprotestanti, nao Waprotestanti waliwadharau wapinzani wao Wakatoliki. Hali hiyo ilisababisha kuanzishwa kwa Muungano wa Waprotestanti na Ushirika wa Wakatoliki mapema katika karne ya 17. Wakuu fulani wa milki hiyo walijiunga na Muungano wa Waprotestanti, huku wengine wakijiunga na Ushirika wa Wakatoliki. Huko Ulaya, na hasa katika milki hiyo, watu hawakuaminiana, na vita vingetokea kama wangechokozwa kidogo tu. Mwishowe, uchokozi huo ulipotokea, vita vilianza navyo vilidumu kwa miaka 30 iliyofuata.

Uchokozi Wasababisha Vita Hatari Huko Ulaya

Viongozi Waprotestanti walijaribu kuwashawishi Wakatoliki wa familia ya Habsburg watoe uhuru zaidi wa ibada. Lakini wakakubali shingo upande, na katika mwaka wa 1617-1618, makanisa mawili ya Kilutheri huko Bohemia (Jamhuri ya Cheki) yakafungwa kwa nguvu. Jambo hilo liliwaudhi wakuu Waprotestanti, ambao waliingia kwa fujo katika jumba la mfalme huko Prague, wakawakamata maofisa watatu Wakatoliki na kuwatupa chini kupitia dirisha lililokuwa kwenye orofa. Tendo hilo ndilo uchokozi uliosababisha vita barani Ulaya.

Kulikuwa na mapigano kati ya dini zenye kupingana ingawa wafuasi wake walidai kuwa wafuasi wa Mkuu wa Amani, Yesu Kristo. (Isaya 9:6) Katika Vita vya Mlima Mweupe, Ushirika wa Wakatoliki ulishinda vibaya ule Muungano wa Waprotestanti ambao ulisambaratika. Wakuu Waprotestanti waliuawa sokoni huko Prague. Katika Bohemia yote, mali ya Waprotestanti waliokataa kukana imani yao ilitwaliwa na kugawanywa kati ya Wakatoliki. Kitabu 1648—Krieg und Frieden in Europa (1648—Vita na Amani Barani Ulaya) kinaeleza kutwaliwa huko kwa mali kuwa “mojawapo ya hali zilizoleta mabadiliko makubwa sana katika umilikaji wa mali huko Ulaya ya kati.”

Mgogoro wa kidini ulioanza huko Bohemia ulipanuka na kuwa mapambano ya kujipatia uwezo mkubwa wa kisiasa juu ya mataifa mengine. Katika miaka 30 iliyofuata, Denmark, Hispania, Sweden, Ufaransa, na Uholanzi zilijitia katika mapambano hayo. Mara nyingi, watawala Wakatoliki na Waprotestanti waliochochewa na pupa na tamaa ya kuwa na mamlaka, walipigana ili kuwa na uwezo mkubwa wa kisiasa na kujinufaisha kibiashara. Vile Vita vya Miaka Thelathini vimegawanywa katika sehemu tatu, na kila sehemu imepewa jina la wapinzani wakuu wa maliki. Vitabu kadhaa vya kitaalamu vinataja sehemu nne: Vita kati ya Bohemia na Palatine, Vita kati ya Denmark na Nyanda za Chini za Saxon, Vita vya Sweden, na Vita kati ya Sweden na Ufaransa. Vita vilivyo vingi vilipiganwa katika Milki Takatifu ya Roma.

Silaha zilizotumiwa wakati huo zilitia ndani bastola, bunduki zinazobebwa mabegani, makombora, na mizinga na nyingi za silaha hizo zilitoka Sweden. Wakatoliki na Waprotestanti walihusika katika vita hivyo. Askari walienda vitani huku wakipaaza sauti “Mtakatifu Maria” au “Mungu yuko pamoja nasi.” Wanajeshi walipita katika majimbo ya Ujerumani huku wakipora mali na kuwatendea kinyama maadui na raia. Vita hivyo vilizidi kuwa vikatili. Hali hiyo ilikuwa kinyume sana na unabii huu wa Biblia: “Hawatainua upanga, taifa juu ya taifa, wala hawatajifunza vita tena”!—Mika 4:3.

Kizazi fulani cha Wajerumani kililelewa katika mazingira ya vita, nao wakaaji waliochoshwa na vita walitamani amani. Yaelekea amani ingepatikana, kama watawala hawangekuwa na mapendezi ya kisiasa yenye kupingana. Vita hivyo viliacha kuwa vya kidini na kuegemea zaidi upande wa kisiasa. Jambo la kushangaza ni kwamba ofisa mkuu wa Kanisa Katoliki ndiye aliyechochea badiliko hilo.

Kadinali Richelieu Atumia Mamlaka

Jina rasmi la Armand-Jean du Plessis lilikuwa Kadinali wa Richelieu. Alikuwa pia waziri mkuu wa Ufaransa kutoka mwaka wa 1624 hadi 1642. Richelieu alitaka kuifanya Ufaransa kuwa serikali kuu barani Ulaya. Ili kutimiza lengo hilo, alijaribu kupunguza mamlaka ya Wakatoliki wenzake, wale wa familia ya Habsburg. Alifanyaje hivyo? Aliyapa pesa majeshi ya Waprotestanti katika majimbo ya Ujerumani, Denmark, Uholanzi, na Sweden ambayo yalikuwa yanapigana na familia ya kifalme ya Habsburg.

Mnamo mwaka wa 1635, Richelieu alipeleka majeshi ya Ufaransa vitani kwa mara ya kwanza. Kitabu vivat pax—Es lebe der Friede! (Amani na Idumu!) kinaeleza kwamba katika kipindi cha mwisho-mwisho cha “vile Vita vya Miaka Thelathini, vita hivyo havikuwa vita vya kidini tena. . . . Vita hivyo viligeuka vikawa vya kupigania uwezo mkubwa wa kisiasa huko Ulaya.” Mapigano ya kidini yaliyoanza kati ya Wakatoliki na Waprotestanti yaliishia kuwa vita ambavyo Wakatoliki waliungana na Waprotestanti kupigana na Wakatoliki wengine. Ushirika wa Wakatoliki, ambao ulikuwa tayari umedhoofika mwanzoni mwa miaka ya 1630, ulivunjiliwa mbali mwaka wa 1635.

Mkutano wa Amani Huko Westphalia

Bara la Ulaya lilikumbwa na uporaji, mauaji, magonjwa, na wanawake kulalwa kinguvu. Hatua kwa hatua tamaa ya kupata amani iliongezeka watu walipotambua kwamba vita hivyo havingekuwa na mshindi. Kitabu vivat pax—Es lebe der Friede! kinasema kwamba “kuelekea mwisho wa miaka ya 1630, wakuu waliokuwa wakitawala walitambua kwamba uwezo wa kijeshi haungewasaidia kutimiza lengo lao.” Lakini ikiwa kila mtu alitamani amani, ingepatikanaje?

Maliki Ferdinand wa Tatu wa Milki Takatifu ya Roma, Mfalme Louis wa Kumi na Tatu wa Ufaransa, na Malkia Christina wa Sweden walikubali kwamba mkutano ufanywe mahali ambapo wale waliopigana vita hivyo wangekusanyika ili kujadiliana kuhusu amani. Maeneo mawili yalichaguliwa kwa ajili ya mazungumzo hayo—mji wa Osnabrück na wa Münster katika mkoa wa Ujerumani wa Westphalia. Miji hiyo ilichaguliwa kwa sababu ilikuwa katikati ya jiji kuu la Sweden na la Ufaransa. Kuanzia mwaka wa 1643, wajumbe 150 hivi, baadhi yao wakiwa na washauri wengi sana, walimiminika katika majiji hayo mawili. Wajumbe Wakatoliki walikutania Münster, nao Waprotestanti wakakutania Osnabrück.

Kwanza, utaratibu fulani uliwekwa ili kuthibitisha vyeo vya wajumbe, kujua watakapoketi, na mambo mengine kuhusu mkutano huo. Kisha, mazungumzo ya amani yakaanza, huku mapendekezo yakipitishwa na wapatanishi kutoka kwa mjumbe mmoja hadi mwingine. Baada ya miaka mitano hivi, vita vikiwa vingali vinaendelea, makubaliano ya amani yalifikiwa. Mkataba wa Amani wa Westphalia uliandikwa katika hati zaidi ya moja. Hati moja ilitiwa sahihi kati ya Maliki Ferdinand wa Tatu na Sweden, nayo nyingine ikatiwa sahihi kati ya maliki na Ufaransa.

Habari za mkataba huo ziliposambaa, watu walianza kusherehekea. Waliangaza anga kwa fataki katika majiji mbalimbali. Kengele za kanisa zikalia, mizinga ikapigwa kuunga mkono mkataba huo, nao watu wakaimba barabarani. Je, kungekuwa na amani ya kudumu huko Ulaya?

Je, Amani ya Kudumu Inaweza Kupatikana?

Mkataba wa Amani wa Westphalia ulitambua kanuni ya kujitawala. Hiyo ilimaanisha kwamba wote waliotia sahihi mkataba huo walikubali kuheshimu mipaka ya nchi nyingine zote na kutoingilia masuala yao ya ndani. Hivyo, kukawa na nchi huru zinazofanyiza bara la Ulaya la kisasa. Baadhi ya nchi hizo zilinufaika zaidi na mkataba huo kuliko nchi nyingine.

Ufaransa ilifanywa kuwa serikali kuu, nayo Uholanzi na Uswisi zikawa nchi huru. Mkataba huo ulikuwa hasara kwa majimbo ya Ujerumani, ambayo mengi yake yalikuwa yameharibiwa na vita. Kwa kiasi fulani mataifa mengine ndiyo yaliyoamua hali ya baadaye ya Ujerumani. Kichapo The New Encyclopædia Britannica kinaripoti: “Faida na hasara ambazo wakuu wa Ujerumani walipata zilitegemea mambo ambayo yangenufaisha zile serikali kuu: Ufaransa, Sweden, na Austria.” Badala ya majimbo ya Ujerumani kuungana na kuwa taifa moja, yaligawanyika kama hapo awali. Isitoshe, watawala wa mataifa mengine walipewa maeneo fulani ya Ujerumani, pamoja na sehemu fulani za mito yake mikuu, ambayo ni Rhine, Elbe, na Oder.

Dini ya Katoliki, Walutheri, na ya wafuasi wa Calvin zilitambuliwa kuwa na haki sawa. Hilo halikuwapendeza wote. Papa Innocent wa Kumi alipinga vikali mkataba huo na kusema kwamba haukuwa halali. Hata hivyo, mipaka ya kidini iliyowekwa haikubadilishwa sana katika miaka 300 iliyofuata. Ingawa watu mmoja-mmoja hawakupata uhuru wa kidini, uhuru huo ulikuwa unaelekea kupatikana.

Mkataba huo ulikomesha vile Vita vya Miaka Thelathini na pia ukakomesha karibu uadui wote uliokuwepo. Hivyo ndivyo vilivyokuwa vita vikuu vya mwisho vya kidini huko Ulaya. Vita havikukoma, lakini kisababishi kikuu kikawa siasa au biashara wala si dini. Hiyo haimaanishi kwamba dini hazikuchangia lolote katika uadui kati ya nchi za Ulaya. Katika Vita vya Kwanza na vya Pili vya Ulimwengu, askari Wajerumani walifunga mishipi yenye kishikizo kilichokuwa na maandishi haya yanayojulikana sana: “Mungu Yuko Pamoja Nasi.” Wakati wa mapigano hayo mabaya, Wakatoliki na Waprotestanti waliungana tena ili kupigana na Wakatoliki na Waprotestanti wenzao wa nchi nyingine.

Ni wazi kwamba Mkataba wa Amani wa Westphalia haukuleta amani ya kudumu. Hata hivyo, hivi karibuni wanadamu watiifu watapata amani hiyo. Yehova Mungu ataleta amani ya kudumu kupitia Ufalme wa Kimasihi wa Mwana wake, Yesu Kristo. Chini ya serikali hiyo, ile dini moja ya kweli itaunganisha watu, badala ya kuwagawanya. Hakuna mtu atakayekuwa na sababu yoyote ile ya kupigana, iwe ya kidini au nyingineyo. Watu watapata kitulizo kilichoje wakati Ufalme utakapotawala dunia yote na ‘kutakapokuwa na amani isiyo na mwisho’!—Isaya 9:6, 7.

[Blabu katika ukurasa wa 21]

Mapigano yaliyoanza kati ya Wakatoliki na Waprotestanti yaliishia kuwa vita ambavyo Wakatoliki waliungana na Waprotestanti kupigana na Wakatoliki wengine

[Blabu katika ukurasa wa 22]

Askari walienda vitani huku wakipaaza sauti “Mtakatifu Maria” au “Mungu yuko pamoja nasi”

[Picha katika ukurasa wa 21]

Kadinali Richelieu

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mchoro wa karne ya 16 unaoonyesha mapambano kati ya Luther, Calvin, na papa

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

From the book Spamers Illustrierte Weltgeschichte VI

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Religious leaders struggling: From the book Wider die Pfaffenherrschaft; map: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck