Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kwa Nini Watu Huenda Kanisani?

Kwa Nini Watu Huenda Kanisani?

 Kwa Nini Watu Huenda Kanisani?

“JAMHURI ya Korea ina Wapresibiteri karibu mara nne ya wale walio Marekani.” Huenda taarifa hiyo katika gazeti la Newsweek iliwashangaza wasomaji wengi, kwa kuwa watu wengi hufikiri kwamba Korea ni jamii ya Wakonfyushasi au Wabudha. Leo, kuna makanisa mengi ya “Kikristo” huko na kwa kawaida hutambuliwa kwa misalaba ya mwangaza mwekundu. Jumapili, ni kawaida kuwaona watu wawili au watatu wakitembea pamoja, wakiwa na Biblia mkononi, wakienda kanisani. Kulingana na uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1998, asilimia 30 ya Wakorea ni wafuasi wa kanisa la Katoliki au Protestanti, wengi kuliko wale wanaodai kuwa Wabudha.

Leo hii sio ajabu kuwaona watu wengi kila mahali wakienda kanisani kwa kawaida. Hata hivyo, hilo halitendeki Korea peke yake bali pia katika nchi nyingine za Asia, hali kadhalika Afrika na Amerika Kusini. Kwa nini bado kuna watu wengi wanaodai kwamba wanamwamini Mungu huku kukiwa na ubaridi mwingi kuelekea dini duniani pote? Kwa nini wanaenda kanisani?

Kura ya maoni ilifunua kwamba zaidi ya nusu ya Wakorea waenda-kanisani wanatafuta amani ya akili; thuluthi moja wanatumaini kuishi milele baada ya kufa; na mtu mmoja kati ya kumi wanatafuta afya, mali, na mafanikio.

Watu wengi huko China humiminika makanisani wakitumaini kuziba pengo la kiroho ambalo limeachwa ubepari unapoendelea kuchukua mahali pa Ukomunisti. Kila mwaka, mamilioni ya Biblia yanachapwa na kugawanywa nchini China, na inaonekana kwamba watu wanaisoma kama walivyokuwa wakikisoma kile kitabu chekundu kidogo cha Mao.

Wakatoliki fulani huko Brazili, hasa walio wachanga kwa umri, hawaridhiki na ahadi ya maisha yajayo yenye furaha—wanataka  kuwa na maisha yenye kuridhisha sasa. Gazeti Tudo linasema: “Ikiwa watu walichochewa na harakati za kutafuta uhuru katika miaka ya 70, leo wanachochewa na harakati za kutafuta ufanisi.” Uchunguzi uliofanywa Uingereza uliwauliza waenda-kanisani nchini humo wataje jambo moja walilopenda kuhusu kanisa lao. Jambo kuu lilikuwa ushirika.

Yote hayo yanaonyesha kwamba ingawa watu wengi wanamwamini Mungu, wengi kati yao wanahangaikia hasa mambo wanayoweza kupata sasa badala ya mambo yatakayokuja—au hata juu ya Mungu mwenyewe. Unafikiri sababu nzuri ya kumwamini Mungu ni nini? Biblia inasema nini kuhusu jambo hilo? Utapata jibu katika makala inayofuata.