Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Martin Luther na Mageuzi Aliyoleta

Martin Luther na Mageuzi Aliyoleta

Martin Luther na Mageuzi Aliyoleta

“INASEMEKANA kwamba vitabu vingi vimeandikwa kumhusu [Martin Luther] kuliko mtu mwingine yeyote katika historia, isipokuwa bwana wake, Yesu Kristo,” likasema gazeti la Time. Maneno na matendo ya Luther yalisaidia kuleta Mageuzi ya Kidini. Mageuzi hayo yametajwa kuwa “mapinduzi makubwa zaidi katika historia ya wanadamu.” Hivyo, Luther alisaidia kuleta mageuzi ya kidini huko Ulaya na kukomesha kipindi cha enzi za kati katika bara hilo. Luther pia alianzisha kanuni za msingi za lugha ya Kijerumani iliyoandikwa. Bila shaka, tafsiri yake ya Biblia ya Kijerumani bado inapendwa sana.

Martin Luther alikuwa mtu wa aina gani? Na ilikuwaje akawa na uvutano mkubwa hivyo barani Ulaya?

Luther Awa Msomi

Martin Luther alizaliwa huko Eisleben, Ujerumani, mnamo Novemba 1483. Ingawa baba yake alifanya kazi kwenye migodi ya shaba, alipata mshahara uliomwezesha kumwelimisha Martin vizuri. Mnamo mwaka wa 1501, Martin alijiunga na Chuo Kikuu cha Erfurt. Alisoma Biblia kwa mara ya kwanza katika maktaba ya chuo hicho. “Kitabu hicho kilinifurahisha sana,” akasema, “nami nilitumaini kwamba nitabarikiwa kuwa na kitabu kama hicho siku moja.”

Alipokuwa na umri wa miaka 22, Luther alijiunga na makao ya watawa ya Augustine huko Erfurt. Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Wittenberg, alikopata shahada ya juu ya theolojia. Luther alijiona kuwa hafai kupata kibali cha Mungu, na wakati mwingine alishuka moyo sana kwa sababu ya dhamiri yenye hatia. Lakini kujifunza Biblia, kusali, na kutafakari kulimsaidia aelewe vizuri zaidi jinsi Mungu anavyowaona watenda dhambi. Luther alitambua kwamba hatuwezi kupata kibali cha Mungu kwa jitihada zetu wenyewe. Badala yake, wale wanaoonyesha imani hupata kibali hicho kupitia fadhili zisizostahiliwa.—Waroma 1:16; 3:23, 24, 28.

Luther alifikiaje mkataa kwamba uelewevu wake mpya ulikuwa sahihi? Kurt Aland, profesa wa historia ya mapema ya kanisa na utafiti wa maandishi ya Agano Jipya, aliandika: “Alisoma na kuitafakari Biblia nzima ili aone kama ujuzi wake mpya ulipatana na habari nyingine katika Biblia, naye akaona kwamba ujuzi huo uliungwa mkono kabisa na Biblia.” Mojawapo ya mafundisho makuu ya Luther ni kwamba mtu anaweza tu kupata wokovu au kuhesabiwa kuwa mwenye haki kupitia imani wala si kupitia matendo au kuonyesha toba kwa kujitesa.

Akasirishwa Sana na Hati za Msamaha

Uelewevu wa Luther kuhusu jinsi Mungu anavyowaona watenda dhambi ulileta ugomvi kati yake na Kanisa Katoliki. Wakati huo watu wengi waliamini kwamba watenda dhambi walipaswa kuteswa kwa kipindi fulani baada ya kufa. Hata hivyo, ilisemekana kwamba kipindi hicho kingeweza kufupishwa kwa kununua hati za msamaha zilizotolewa kwa amri ya papa. Wauzaji wa hati za msamaha kama vile Johann Tetzel, aliyekuwa mwakilishi wa Askofu Mkuu Albert wa Mainz, walipata faida kubwa kwa kuwauzia watu wa kawaida hati hizo. Wengi waliziona kama aina fulani ya bima dhidi ya dhambi za wakati ujao.

Luther alikasirishwa sana na uuzaji wa hati za msamaha. Alijua kwamba wanadamu hawawezi kufanya mapatano na Mungu kupitia pesa. Katika mwaka wa 1517, aliandika zile hoja zake maarufu 95 naye alishutumu kanisa kwa kutumia vibaya pesa, mafundisho, na dini. Kwa kuwa alitaka kuchochea mageuzi wala si uasi, Luther alimtumia Askofu Mkuu Albert wa Mainz na wasomi kadhaa nakala za hoja zake. Wanahistoria wengi wanasema kuwa Mageuzi ya Kidini yalianza mwaka wa 1517 hivi.

Si Luther peke yake aliyehuzunishwa na matendo mabaya ya kanisa. Miaka 100 mapema, Jan Hus, mleta-mageuzi ya kidini wa nchi ya Cheki alishutumu uuzaji wa hati za msamaha. Hata kabla ya Hus kufanya hivyo, John Wycliffe wa Uingereza alikuwa amesema kwamba kanisa lilishika mapokeo fulani ambayo yalikuwa kinyume cha Maandiko. Erasmus wa Rotterdam na Tyndale wa Uingereza, ambao waliishi wakati mmoja na Luther, waliunga mkono mageuzi. Lakini kwa msaada wa mashine ya uchapaji iliyobuniwa na Johannes Gutenberg huko Ujerumani, ujumbe ulioandikwa na Luther ulikuwa na matokeo sana nao ulisambazwa zaidi kuliko wa waleta-mageuzi wengine.

Katika mwaka wa 1455 mashine hiyo ya Gutenberg ilikuwa ikitumiwa huko Mainz. Mwanzoni mwa mwaka wa 1500, kulikuwa na mashine za uchapaji katika miji 60 ya Ujerumani na nchi nyingine 12 za Ulaya. Kwa mara ya kwanza katika historia, watu wangeweza kujulishwa kwa haraka mambo yaliyowahusu. Huenda hoja 95 za Luther zilichapishwa na kusambazwa bila ruhusa yake. Suala la mageuzi ya kanisa halikuhusu eneo hilo tu bali lilitokeza ubishi ulioenea kila mahali naye Martin Luther akawa mtu mashuhuri sana nchini Ujerumani.

“Jua na Mwezi” Wachukua Hatua

Kwa karne nyingi, Ulaya ilitawaliwa na matengenezo mawili yenye nguvu: Miliki Takatifu ya Roma na Kanisa Katoliki. “Maliki na papa walishirikiana kwa ukaribu kama jua na mwezi,” akaeleza Hanns Lilje, aliyekuwa rais wa Muungano wa Kilutheri Ulimwenguni. Hata hivyo, haikuwa wazi ni nani aliyekuwa na uwezo mwingi kuliko mwingine. Mapema katika miaka ya 1500, matengenezo hayo yalikuwa yamepita upeo wa mamlaka yao. Mabadiliko yalikuwa karibu kutokea.

Alipopata zile hoja 95 za Luther, Papa Leo wa Kumi alitisha kumtenga na kanisa kama hangekana hoja hizo. Kwa ujasiri, Luther alikataa kufanya hivyo na kuteketeza hadharani barua ya papa iliyokuwa na tisho hilo naye akachapisha vitabu zaidi vilivyochochea maeneo yaliyotawaliwa na wakuu yafanye mageuzi katika kanisa hata bila kibali cha papa. Katika mwaka wa 1521, Papa Leo wa Kumi alimtenga Luther na kanisa. Luther alipolalamika kwamba alikuwa amehukumiwa bila kusikizwa vizuri, Maliki Charles wa Tano alimwita mleta mageuzi huyo aje mbele ya baraza au mkutano wa kifalme huko Worms. Safari ya Luther ya siku 15 kutoka Wittenberg kwenda Worms mnamo Aprili 1521 ilikuwa kama msafara wa ushindi. Watu waliunga mkono maoni yake, na kila mahali walitaka kumwona.

Huko Worms, Luther alisimama mbele ya maliki, wakuu, na mjumbe wa papa. Jan Hus alisikilizwa na baraza kama hilo huko Constance mwaka wa 1415 na kuteketezwa juu ya mti. Huku akitazamwa na wakuu wa kanisa na wa miliki, Luther alikataa kukana hoja zake isipokuwa wapinzani wake wathibitishe kupitia Biblia kwamba alikuwa mwenye makosa. Lakini uwezo wake wa kukumbuka Maandiko haukuwa na kifani. Hati iliyoitwa Amri ya Worms ilionyesha matokeo ya kesi hiyo. Ilimtangaza Luther kuwa mwasi sheria na kwamba maandishi yake yalipigwa marufuku. Sasa maisha yake yalikuwa hatarini kwa kuwa papa alimtenga na kanisa naye maliki akamtangaza kuwa mwasi sheria.

Kisha matukio yenye kutokeza na yasiyotazamiwa yakatokea. Alipokuwa safarini kurudi Wittenberg, mfadhili aliyeitwa Frederick wa Saxony alifanya mpango ili ionekane kana kwamba Luther ametekwa nyara. Hivyo ikawa vigumu kwa maadui wa Luther kumkamata. Luther aliingizwa kisiri katika ngome iliyojitenga ya Wartburg, ambako alikuza ndevu na kujiita Junker Jörg, jina la mtu fulani aliyekuwa mashuhuri.

Biblia ya Septemba Yahitajiwa Sana

Kwa miezi kumi, Luther aliishi akiwa mtoro katika ngome ya Wartburg ili kuepuka kukamatwa na maliki na papa. Kitabu Welterbe Wartburg kinaeleza kwamba “wakati alioishi Wartburg ndio uliokuwa wenye mafanikio zaidi maishani mwake.” Mojawapo ya mafanikio yake makubwa zaidi ni kumaliza kutafsiri maandishi ya Erasmus ya Maandiko ya Kigiriki katika lugha ya Kijerumani. Tafsiri hiyo ilichapishwa mnamo Septemba 1522, bila kumtaja Luther kuwa mtafsiri wake, nayo iliitwa Biblia ya Septemba. Thamani ya Biblia hiyo ilikuwa sawa na mshahara wa mwaka mmoja wa mfanyakazi wa nyumbani. Hata hivyo, watu wengi sana waliagiza Biblia hiyo. Katika kipindi cha miezi 12 nakala 6,000 zilichapwa katika matoleo 2, na katika miaka 12 iliyofuata, matoleo zaidi ya 69 yakachapwa.

Katika mwaka wa 1525, Martin Luther alimwoa Katharina von Bora, aliyekuwa mtawa. Katharina alikuwa na uwezo wa kushughulikia mambo, naye aliweza kutimiza kazi iliyotokana na ukarimu wa mume wake. Watu walioishi nyumbani kwa Luther walitia ndani mke wake na watoto sita na pia marafiki, wasomi, na wakimbizi. Baadaye maishani, Luther alikuwa mtu aliyeheshimiwa sana hivi kwamba wasomi waliomtembelea nyumbani kwake waliandika mambo aliyosema. Maandishi hayo yalikusanywa na kufanyizwa kitabu kilichoitwa Luthers Tischreden (Mazungumzo ya Luther Wakati wa Chakula). Kwa muda fulani, kitabu hicho kiliuzwa kwa wingi kuliko kitabu kingine chochote cha Kijerumani isipokuwa Biblia.

Mwandikaji na Mtafsiri Mwenye Kipawa Aliyeandika Vitabu Vingi

Kufikia mwaka wa 1534, Luther alikuwa amemaliza kutafsiri Maandiko ya Kiebrania. Alikuwa na uwezo wa kusawazisha mtindo wa kuandika, mtiririko, na maneno ya lugha. Hivyo alitafsiri Biblia iliyoeleweka vizuri na watu wa kawaida. Luther aliandika hivi kuhusu mtindo wake wa kutafsiri: “Tunapaswa kuzungumza na mama wa nyumbani, watoto barabarani na mtu wa kawaida sokoni, kisha tusikilize kwa makini jinsi wanavyozungumza halafu tutafsiri kulingana na hayo.” Biblia ya Luther iliweka kanuni za msingi za lugha iliyoandikwa ambayo baadaye ilikubaliwa kotekote Ujerumani.

Luther alikuwa mtafsiri mwenye kipawa na mwandikaji stadi. Inasemekana kwamba katika muda wote aliofanya kazi hiyo, aliandika makala moja kila baada ya majuma mawili. Baadhi ya makala hizo zilikuwa zenye kuleta ubishi kama vile mtungaji wazo. Mwanzoni, mtindo wa Luther wa kuandika ulikuwa mkali, naye hakubadili mtindo huo hata alipokuwa mzee. Maandishi yake ya baadaye yalikuwa makali hata zaidi. Kitabu Lexikon für Theologie und Kirche, kinasema kwamba vitabu vya Luther vinaonyesha “hasira yake iliyopita kiasi,” “ukosefu wa unyenyekevu na upendo,” na pia “hisia nyingi za kutimiza mwito wa pekee.”

Vita vya Wakulima vilipotokea na watu wengi kuuawa katika maeneo yaliyotawaliwa na wakuu, Luther aliombwa atoe maoni yake kuhusu maasi hayo. Je, wakulima hao walikuwa na sababu ya kulalamika dhidi ya mabwana wao? Luther hakujaribu kuwaunga mkono kwa kutoa jibu ambalo lingewapendeza wengi. Aliamini kwamba watumishi wa Mungu wanapaswa kuwatii wenye mamlaka. (Waroma 13:1) Luther alisema waziwazi kwamba nguvu zilipaswa kutumiwa ili kukomesha uasi huo. “Yule anayeweza kuchoma kwa kisu, kupiga, au kuua, na afanye hivyo,” akasema. Hanns Lilje alisema kwamba jibu hilo lilimfanya Luther apoteze “umaarufu wa pekee aliokuwa nao miongoni mwa watu.” Isitoshe, maandishi ya baadaye ya Luther kuhusu Wayahudi waliokataa kugeuka na kuwa Wakristo, hasa maandishi ya On the Jews and Their Lies, yamewafanya wengi kudai kwamba mwandikaji huyo aliwachukia Wayahudi.

Mageuzi Yaliyoletwa na Luther

Mageuzi hayo ya Kidini yaliyochochewa na watu kama vile Luther, Calvin, na Zwingli, yalisababisha kuundwa kwa dini mpya inayoitwa Uprotestanti. Kuhesabiwa kuwa mwenye haki kupitia imani ndilo fundisho kuu ambalo Luther aliacha katika Uprotestanti. Maeneo ya Ujerumani yaliyotawaliwa na wakuu yaliunga mkono imani ya Kiprotestanti au ya Kikatoliki. Uprotestanti ulienea na kuungwa mkono na watu wengi huko Skandinavia, Uswisi, Uingereza, na Uholanzi. Leo dini hiyo ina wafuasi wengi sana.

Watu wengi bado wanamheshimu sana Luther ingawa hawaamini mambo yote aliyofundisha. Katika mwaka wa 1983, ile iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani ambayo ilitia ndani Erfurt, Wittenberg, na Wartburg, ilisherehekea mwaka wa 500 wa kuzaliwa kwa Luther. Serikali hiyo ya Kisoshalisti ilimtambua Luther kuwa mtu mashuhuri katika historia na utamaduni wa Ujerumani. Isitoshe, mwanatheolojia Mkatoliki wa miaka ya 1980 alisema hivi kwa ufupi kuhusu uvutano wa Luther: “Hakuna mtu aliyeishi baada ya Luther anayeweza kulinganishwa naye.” Naye Profesa Aland aliandika: “Kila mwaka kuna angalau vichapo vipya 500 kuhusu Martin Luther na kuhusu Mageuzi ya Kidini. Vichapo hivyo vinachapishwa katika karibu lugha zote kuu ulimwenguni.”

Martin Luther alikuwa mwenye akili sana, uwezo wa ajabu wa kukumbuka mambo, stadi katika kutumia maneno, na mfanyakazi mwenye bidii. Pia alikuwa mtu asiye na subira na mwenye dharau, naye alipinga vikali unafiki. Alipokuwa anakaribia kufa huko Eisleben mnamo Februari 1546, marafiki wake walimwuliza kama bado aliamini kabisa mambo aliyokuwa amefundisha wengine. “Ndiyo,” akajibu. Luther alikufa, lakini wengi bado wanafuata mafundisho yake.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Luther alipinga uuzaji wa hati za msamaha

[Hisani]

Mit freundlicher Genehmigung: Wartburg-Stiftung

[Picha katika ukurasa wa 28]

Luther alikataa kukana hoja zake isipokuwa wapinzani wake wathibitishe kupitia Biblia kwamba alikuwa mwenye makosa

[Hisani]

From the book The Story of Liberty, 1878

[Picha katika ukurasa wa 29]

Chumba cha Luther katika ngome ya Wartburg ambapo alitafsiri Biblia

[Hisani]

Both images: Mit freundlicher Genehmigung: Wartburg-Stiftung

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

From the book Martin Luther The Reformer, 3rd Edition, published by Toronto Willard Tract Depository, Toronto, Ontario

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]

From the book The History of Protestantism (Vol. I)