Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Maandishi ya Noa Yana Maana Kwetu?

Je, Maandishi ya Noa Yana Maana Kwetu?

Je, Maandishi ya Noa Yana Maana Kwetu?

YESU alisema hivi alipotoa unabii kuhusu ishara ya kuwapo kwake na ya umalizio wa mfumo wa mambo: “Kama vile siku za Noa zilivyokuwa, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa.” (Mathayo 24:3, 37) Yesu alitabiri waziwazi kwamba mambo yanayotukia wakati wetu yanafanana na ya wakati wa Noa. Masimulizi yanayotegemeka na yaliyo sahihi kuhusu matukio ya siku za Noa yanaweza kuwa na maana kubwa kwetu.

Je, maandishi ya Noa yana maana kwetu? Je, yamethibitishwa kihistoria kuwa ya kweli? Je, kweli tunaweza kujua Gharika hiyo ilitukia lini?

Gharika Ilitukia Lini?

Biblia inatoa habari za matukio kulingana na jinsi yalivyofuatana. Matukio hayo hutuwezesha kuhesabu miaka ambayo imepita tangu kuumbwa kwa mwanadamu. Katika andiko la Mwanzo 5:1-29, tunapata orodha ya vizazi vilivyoishi tangu kuumbwa kwa Adamu, mwanadamu wa kwanza, hadi kuzaliwa kwa Noa. Gharika ilianza “katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu.”—Mwanzo 7:11.

Ili kujua Gharika ilitukia wakati gani, tunahitaji kupiga hesabu kuanzia tarehe fulani ya msingi. Yaani, lazima tuanze na tarehe inayokubalika katika historia, ambayo jambo fulani hususa linalotajwa katika Biblia lilitukia. Kuanzia tarehe hiyo ya msingi, tunaweza kupiga hesabu na kujua tarehe hususa ambayo Gharika ilitukia kwa kutegemea kalenda ya Gregory inayotumiwa sasa.

Tarehe moja ya msingi ni 539 K.W.K., mwaka ambao Mfalme Koreshi wa Uajemi alishinda Babiloni. Habari kuhusu utawala wake zinapatikana katika mabamba na pia katika maandishi ya Diodorus, Africanus, Eusebius, na Ptolemy. Kwa amri ya Koreshi, mabaki ya Wayahudi waliondoka Babiloni na kuwasili nchini kwao mwaka wa 537 K.W.K. Kulingana na Biblia, kuondoka kwa Wayahudi kulionyesha kwamba miaka 70 ya ukiwa iliyoanza mwaka wa 607 K.W.K. ilikuwa imekwisha. Kwa kuhesabu muda ambao waamuzi na wafalme walitawala Israeli, tunaweza kubainisha kwamba ile safari ya Waisraeli kutoka Misri ilianza mwaka wa 1513 K.W.K. Tukihesabu miaka 430 kwenda nyuma kuanzia mwaka wa 1513 K.W.K., tunafikia mwaka wa 1943 K.W.K. ambapo Mungu alifanya agano na Abrahamu. Halafu, tunapaswa kufikiria wakati ambapo Tera, Nahori, Serugi, Reu, Pelegi, Eberi, na Shela walizaliwa na muda wa maisha yao, na vilevile Arfaksadi, aliyezaliwa “miaka miwili baada ya gharika.” (Mwanzo 11:10-32) Hivyo, tunaweza kusema kwamba Gharika ilianza mwaka wa 2370 K.W.K. *

Gharika Yaanza

Kabla ya kuchunguza matukio ya siku za Noa, huenda ukataka kusoma Mwanzo sura ya 7 mstari wa 11 hadi sura ya 8 mstari wa 4. Biblia inasema hivi kuhusu hiyo mvua kubwa: “Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu [2370 K.W.K.], mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka.”—Mwanzo 7:11.

Noa aliugawanya mwaka kwa miezi 12, kila mwezi ukiwa na siku 30. Zamani, mwezi wa kwanza ulianza karibu na katikati ya mwezi wa Septemba kulingana na kalenda ya sasa. Mvua ilianza kunyesha “mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi” na ikaendelea kwa siku 40 mchana na usiku hadi mwezi wa Novemba na Desemba, mwaka wa 2370 K.W.K.

Biblia inatuambia hivi pia kuhusu Gharika hiyo: “Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini. . . . Maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka. Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati.” (Mwanzo 7:24–8:4) Kwa hiyo, ilichukua muda wa siku 150 au miezi mitano tangu maji yafunike dunia kabisa hadi wakati yalipoanza kupungua. Hivyo, safina ilitua kwenye milima ya Ararati Aprili 2369 K.W.K.

Sasa huenda ukataka kusoma Mwanzo 8:5-17. Vilele vya milima vilianza kuonekana karibu miezi miwili na nusu (siku 73) baadaye, ‘mwezi wa kumi [Juni], siku ya kwanza ya mwezi.’ (Mwanzo 8:5) * Miezi mitatu [siku 90] baadaye—katika “mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza” ya maisha ya Noa, au katikati ya mwezi wa Septemba, 2369 K.W.K., Noa aliondoa kifuniko cha safina. Hivyo angeweza kuona kwamba “uso wa nchi umekauka.” (Mwanzo 8:13) Mwezi mmoja na siku 27 (siku 57) baadaye, “mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi [katikati ya mwezi wa Novemba, 2369 K.W.K.], nchi ilikuwa kavu.” Kwa hiyo Noa na familia yake wakatoka nje kwenye nchi kavu. Hivyo, Noa na wengine walikaa ndani ya safina kwa mwaka mmoja na siku kumi (siku 370).—Mwanzo 8:14.

Maandishi hayo sahihi yanayotaja matukio mbalimbali, yanayoeleza mambo kinaganaga, na kutaja wakati hususa yanathibitisha nini? Yanathibitisha jambo hili: Musa, nabii Mwebrania, ambaye yaonekana aliandika kitabu cha Mwanzo akitegemea habari alizopokea, aliandika mambo hakika, wala si hekaya tu. Kwa hiyo, Gharika ina maana kubwa sana kwetu leo.

Waandikaji Wengine wa Biblia Waliionaje Gharika?

Mbali na masimulizi ya kitabu cha Mwanzo, kuna vitabu vingi vya Biblia ambavyo hutaja Noa au Gharika. Kwa mfano:

(1) Mtafiti Ezra alimtaja Noa na watoto wake (Shemu, Hamu, na Yafethi) katika ukoo wa taifa la Israeli.—1 Mambo ya Nyakati 1: 4-17.

(2) Luka, tabibu na mwandishi wa Injili, anamtaja Noa anapoorodhesha watu wa ukoo wa Yesu Kristo.—Luka 3:36.

(3) Mtume Petro anataja Gharika mara nyingi anapowaandikia Wakristo wenzake.—2 Petro 2:5; 3:5, 6.

(4) Mtume Paulo anataja imani kubwa ambayo Noa alionyesha kwa kujenga safina ili kuokoa watu wa familia yake.—Waebrania 11:7.

Je, waandishi hao wa Biblia walioongozwa na roho ya Mungu walitilia shaka masimulizi ya Gharika? La, waliyaona kuwa ya kweli.

Yesu na Gharika

Yesu Kristo alikuwapo kabla ya kuwa mwanadamu. (Mithali 8:30, 31) Alikuwa kiumbe wa roho mbinguni wakati wa Gharika. Kwa hiyo, Yesu anatupatia uthibitisho mkubwa wa Kimaandiko kuhusu Noa na Gharika kwa sababu alishuhudia tukio hilo. Yesu alisema: “Kama vile siku za Noa zilivyokuwa, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa. Kwa maana kama walivyokuwa katika siku hizo kabla ya furiko, wakila na kunywa, wanaume wakioa na wanawake wakiozwa, hadi siku ambayo Noa aliingia ndani ya safina; nao hawakujali mpaka furiko likaja na kuwafagilia mbali wote, ndivyo kuwapo kwa Mwana wa binadamu kutakavyokuwa.”—Mathayo 24:37-39.

Je, Yesu angetumia hekaya kutuonya kuhusu kuja kwa mwisho wa mfumo huu wa mambo? La! Tuna hakika kwamba alitumia mfano halisi kueleza jinsi Mungu atakavyotekeleza hukumu yake juu ya waovu. Naam, watu wengi walikufa, lakini tunafarijika kujua kwamba Noa na familia yake waliokoka Gharika.

“Siku za Noa” zina maana kubwa kwa wote wanaoishi leo, wakati wa “kuwapo kwa Mwana wa binadamu,” Yesu Kristo. Tunaposoma maandishi yaliyohifadhiwa na Noa kuhusu Gharika ambayo yanataja mambo kinaganaga, tunaweza kuwa na hakika kwamba habari hiyo imethibitishwa kihistoria. Nayo masimulizi kuhusu Gharika katika kitabu cha Mwanzo ambayo yaliandikwa kwa mwongozo wa roho ya Mungu, yana maana kubwa kwetu. Kama vile Noa na watoto wake, na wake zao walivyodhihirisha imani katika njia ya Mungu ya kuokoa, sisi leo tunaweza kupata ulinzi wa Yehova kwa kuwa na imani katika dhabihu ya fidia ya Yesu. (Mathayo 20:28) Isitoshe, kama vile maandishi ya Noa yanavyoonyesha kwamba yeye na familia yake waliokoka Gharika iliyouharibu ulimwengu huo usiomwogopa Mungu, tunaweza kuwa na tumaini la kuwa miongoni mwa wale watakaookoka mwisho wa mfumo huu mwovu wa mambo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Ili upate habari zaidi kuhusu jinsi ya kupiga hesabu na kufikia mwaka ambao Gharika ilianza, ona kitabu Insight on the Scriptures, Buku la 1, ukurasa wa 458-460, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

^ fu. 12 Kichapo Commentary on the Old Testament cha Keil-Delitzsch, Buku la 1, ukurasa wa 148 kinasema: “Yaelekea baada ya siku 73 vilele vya milima ya Armenia iliyoizunguka safina vilionekana.”

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Je, Waliishi Muda Mrefu Hivyo?

BIBLIA inasema, “siku zote za Nuhu zilikuwa miaka mia kenda na hamsini, akafa.” (Mwanzo 9:29) Methusela, babu ya Noa aliishi miaka 969 na ndiye mwanadamu aliyeishi muda mrefu zaidi. Vizazi kumi kuanzia Adamu hadi Noa viliishi kwa wastani wa miaka 850. (Mwanzo 5:5-31) Je, watu wa enzi hizo waliishi muda mrefu hivyo?

Tangu mwanzoni, Mungu alikusudia mwanadamu aishi milele. Mwanadamu wa kwanza Adamu, aliumbwa akiwa na uwezo wa kuishi milele mradi tu angemtii Mungu. (Mwanzo 2:15-17) Lakini Adamu hakutii, hivyo hangeweza kuishi milele. Aliishi kwa miaka 930, ambapo hali yake ilidhoofika polepole hadi akafa na kurudi mavumbini ambako alitwaliwa. (Mwanzo 3:19; 5:5) Mwanadamu huyo wa kwanza alipitisha dhambi na kifo kwa wazao wake wote.—Waroma 5:12.

Hata hivyo, watu walioishi wakati huo walikuwa karibu na ukamilifu ambao Adamu alikuwa nao hapo awali na yaonekana ni kwa sababu hiyo waliishi muda mrefu kuliko wale waliozaliwa baadaye. Hivyo, watu waliishi kwa wastani wa miaka elfu moja kabla ya Gharika, lakini baada ya hapo muda wa kuishi wa wanadamu ulipungua sana. Kwa mfano, Abrahamu aliishi miaka 175 tu. (Mwanzo 25:7) Na miaka 400 baada ya kifo cha mzee huyo wa ukoo mwaminifu, nabii Musa aliandika hivi: “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; na kiburi chake ni taabu na ubatili, maana chapita upesi tukatokomea mara.” (Zaburi 90:10) Na ndivyo ilivyo leo.

[Chati/Picha katika ukurasa wa 6, 7]

Tangu Koreshi Atoe Amri ya Kuwaruhusu Wayahudi Warudi Kutoka Uhamishoni, Kuhesabu Kuelekea Nyuma Hadi Gharika ya Siku za Noa

537 Amri ya Koreshi *

539 Koreshi Mwajemi ashinda Babiloni

Miaka 68

607 Ukiwa wa Yuda wa miaka 70 waanza

Taifa la Israeli

laongozwa na viongozi,

waamuzi, na wafalme

kwa miaka 906

1513 Ile safari ya Waisraeli kutoka Misri

Miaka 430 Kile kipindi cha miaka 430 ambapo

wana wa Israeli waliishi katika nchi ya

Misri na Kanaani (Kutoka 12:40, 41)

1943 Uhalalishwa kwa agano la Kiabrahamu

Miaka 205

2148 Kuzaliwa kwa Tera

Miaka 222

2370 Kuanza kwa Gharika

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 35 Amri ya Koreshi ya kuachiliwa huru kwa Wayahudi kutoka uhamishoni ilitolewa “katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi,” yaelekea katika mwaka wa 538 K.W.K. au mapema mwaka wa 537 K.W.K.