Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unahitaji Dhamiri Iliyozoezwa

Unahitaji Dhamiri Iliyozoezwa

Unahitaji Dhamiri Iliyozoezwa

Ingalikuwa siku ya kukumbuka kwa abiria na wafanyakazi waliokuwa kwenye ndege, ndege namba 901 ya shirika la ndege la New Zealand, iliyokuwa ikisafiri Antaktika. Abiria hao walikuwa wenye furaha nyingi huku wakiwa tayari kupiga picha wakati ndege hiyo iliporuka chini kwa chini ili waweze kuona mandhari ya Antaktika vizuri.

RUBANI wa ndege hiyo alikuwa ameendesha ndege kwa jumla ya saa 11,000 katika kipindi cha miaka 15. Kabla ya kuanza kuruka alikuwa ameingiza kwa uangalifu ratiba ya safari katika kompyuta yake kwenye ndege, bila kujua kwamba tarakimu alizopewa hazikuwa sahihi. Ndege hiyo ilikuwa ikiruka urefu wa meta zisizozidi 600 wakati ilipogonga sehemu ya chini ya Mlima Erebus, na kuua abiria wote 257.

Wanadamu wamepewa dhamiri iwaongoze maishani kama vile ambavyo ndege leo huongozwa na kompyuta zinapokuwa angani. Msiba mbaya uliopata ndege hiyo unaweza kutufunza mambo muhimu sana kuhusu dhamiri yetu. Kwa mfano, kama vile usalama wa ndege unavyotegemea mfumo wa kuongozea ndege ulio sahihi na unaofanya kazi vizuri, vivyo hivyo hali nzuri ya kiroho, kiadili, na hata kimwili hutegemea dhamiri yenye kutenda, inayoongozwa vizuri kiadili.

Inasikitisha kwamba katika ulimwengu wa leo, mwongozo huo unatoweka haraka au unapuuzwa. “Tunasikia mengi leo kuhusu jinsi mvulana wa kawaida wa shule huko Marekani asivyoweza kusoma, kuandika, na jinsi anavyotatizika katika somo la Jiografia,” akasema mwalimu mmoja wa Marekani. “Pia, ni kweli kwamba mvulana huyo hawezi kupambanua mema na mabaya. Mbali na matatizo ya kutojua kusoma na kuandika, na vilevile matatizo ya kutoelewa hesabu na sayansi, mvulana huyo amechanganyikiwa kabisa kiadili.” Alisema pia kwamba “vijana wa siku hizi hawaelewi maadili vizuri. Mwulize mmoja wao kama kuna mambo kama ‘ubaya na wema,’ na mara moja utaona kijana mwenye wasiwasi, aliyechanganyikiwa, asiyejua la kusema. . . . Hali hiyo huwa mbaya hata zaidi wanapojiunga na vyuo.”

Jambo moja linalosababisha kuchanganyikiwa huko ni yale maoni yaliyoenea kwamba maadili hutegemea mapendezi ya mtu binafsi au utamaduni. Hebu wazia kungetokea nini kama marubani wangeendesha ndege kwa kufuata ishara za kuongozea ndege zisizotegemeka ambazo wakati mwingine hata hutoweka kabisa, badala ya kufuata mwongozo ulio thabiti! Maafa kama yale yaliyotokea kwenye Mlima Erebus yangekuwa mambo ya kawaida. Vivyo hivyo, kwa sababu ya kuacha kufuata viwango thabiti vya maadili, watu wanazidi kuteseka na kufa huku familia zikivunjika kutokana na ukosefu wa uaminifu, na mamilioni wakiteseka kutokana na UKIMWI au magonjwa mengine yanayoambukizwa kingono.

Huenda maoni yaliyoenea kwamba maadili hutegemea mapendezi ya mtu binafsi au utamaduni yakasikika kuwa ya kisasa, lakini ukweli ni kwamba wanaofuata maoni hayo wanafanana na Waninawi wa kale ambao hawakupambanua ‘kati ya mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto.’ Wale wanaofuata maoni hayo wanafanana pia na Waisraeli waasi-imani waliosema kwamba “uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu.”—Yona 4:11; Isaya 5:20.

Kwa hiyo ni wapi tunapoweza kupata sheria na kanuni zilizo wazi na zenye kueleweka za kuzoeza dhamiri yetu ili ituongoze kwa njia iliyo salama? Watu wengi wameona kwamba Biblia hutimiza kikamili uhitaji huo. Biblia ina habari zote muhimu kuhusu maadili kwa jumla, maadili ya kazi, kuzoeza watoto, na kumwabudu Mungu. (2 Timotheo 3:16) Biblia imekuwa yenye kutegemeka kabisa kwa karne nyingi. Viwango vya maadili vya Biblia vinawafaa watu wote kwa kuwa viliwekwa na Muumba wetu aliye na mamlaka ya juu zaidi. Hivyo, hatuhitaji kuishi bila kujua yaliyo mema na yaliyo mabaya.

Hata hivyo, siku hizi dhamiri yako inashambuliwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Inawezekanaje? Nawe unaweza kuilinda dhamiri yako jinsi gani? Jambo la hekima kufanya ni kujua yule anayeshambulia dhamiri yetu na mbinu zake. Mambo hayo yatazungumziwa katika makala inayofuata.