Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Ibilisi Yuko?

Je, Ibilisi Yuko?

Je, Ibilisi Yuko?

‘Ingawa leo ni watu wachache tu wanaomwona Mungu kuwa halisi na mwenye nguvu, kuna wakati ambapo Kanisa la Kikristo lilimwona ibilisi, Beelzebubi au Shetani kuwa mfalme halisi na mwovu. Ibilisi ambaye alionyeshwa kuwa nusu-mtu, nusu-mnyama, alibuniwa tu na Wayahudi na Wakristo wa mapema ili kueleza ni kwa nini kulikuwa na uovu. Baadaye Wakristo walikuja kutambua kwamba Ibilisi alikuwa kiumbe wa kuwaziwa tu na hatua kwa hatua wakaacha kuamini kuweko kwa Ibilisi.’—Kitabu “All in the Mind—A Farewell to God,” cha Ludovic Kennedy.

MWANDISHI na mtangazaji aitwaye Ludovic Kennedy asema kwamba, kwa karne nyingi hakuna hata mtu mmoja katika Jumuiya ya Wakristo aliyetilia shaka kuweko kwa Ibilisi. Badala yake, kama Profesa Norman Cohn asemavyo, nyakati nyingine Wakristo “walishikilia sana imani ya kuweko kwa nguvu za Shetani na roho wake waovu.” (Europe’s Inner Demons) Si watu wa kawaida tu wasio na elimu walioamini hivyo. Kwa mfano, imani kwamba Ibilisi alijivika umbo la mnyama ili kusimamia utekelezaji wa mambo maovu na matambiko machafu, ‘haikutokana na ngano za watu wasio na elimu ambao ndio waliokuwa wengi, bali ilitokana na wasomi,’ asema Profesa Cohn. ‘Wasomi hao’ waliotia ndani makasisi wenye elimu, ndio walioongoza msako wa wachawi kotekote Ulaya kuanzia karne ya 15 hadi ya 17. Inasemekana kwamba wakati huo, viongozi wa kidini na wa kiraia waliwaua watu wapatao 50,000 waliodaiwa kuwa wachawi.

Si ajabu kwamba wengi wamekataa kile ambacho wanakiona kuwa dhana zisizo na msingi na za kishirikina kuhusu Ibilisi. Hata katika mwaka wa 1726, Daniel Defoe alidhihaki imani ya watu kwamba Ibilisi ni jitu lenye umbo la kutisha “lenye mabawa ya popo, pembe, nyayo zilizopasuka sehemu mbili, mkia mrefu, ulimi uliogawanyika sehemu mbili, na kadhalika.” Alisema hizo zilikuwa ‘dhana za kipuuzi’ zilizobuniwa na ‘watu walioendeleza wazo la kuwako kwa ibilisi na ambao walidanganya watu wasio na ujuzi.’

Je, hayo ndiyo maoni yako? Je, unakubali kwamba “ibilisi ni ubuni tu wa mwanadamu ili kueleza hali yenye dhambi ya mwanadamu”? Maneno hayo yamo katika kichapo The Zondervan Pictorial Encyclopedia of the Bible, na wengi wanaodai kuwa Wakristo hufikiri hivyo. Jeffrey Burton Russell asema kwamba kwa jumla wanatheolojia wa Jumuiya ya Wakristo ‘walikataa kuwepo kwa Ibilisi na roho waovu wakisema huo ni ushirikina tu wa zamani.’

Hata hivyo, watu wengine humwona Ibilisi kuwa kiumbe halisi. Wao husababu kwamba lazima kuwe na nguvu fulani ya uovu inayozidi uwezo wa binadamu ambayo husababisha maovu yenye kutokea mara nyingi, maovu ambayo yameenea katika historia ya mwanadamu. “Mambo yenye kutisha ambayo yametokea katika karne ya ishirini,” asema Russell, ni sababu moja inayofanya “imani katika Ibilisi irudi, tena kwa haraka, baada ya kutoweka kwa muda mrefu.” Kulingana na mwandishi Don Lewis, watu kadhaa wa siku hizi walioelimika ambao ‘hudhihaki’ imani na hofu za kishirikina za ‘mababu wao wasiokuwa na elimu, wameanza kuvutiwa tena na kuweko kwa uovu unaotokana na viumbe wenye nguvu zisizo za kawaida.’—Religious Superstition Through the Ages.

Hivyo basi, ukweli ni nini kuhusu Ibilisi? Je, Ibilisi ni upuuzi mtupu tu wa kishirikina? Au je, yeye ni kiumbe asiyepasa kupuuzwa hata katika karne hii ya 21?

[Picha katika ukurasa wa 4]

Kama inavyoonyeshwa kwenye mchoro huu wa Gustave Doré, ushirikina wa kale ulimwonyesha Ibilisi kuwa nusu-mtu na nusu-mnyama

[Hisani]

The Judecca—Lucifer/The Doré Illustrations For Dante’s Divine Comedy/Dover Publications Inc.