Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ushindi Kwenye Mahakama ya Jimbo

Ushindi Kwenye Mahakama ya Jimbo

Ushindi Kwenye Mahakama ya Jimbo

MASHAHIDI WA YEHOVA nchini Ujerumani walipata ushindi mkubwa kwenye Mahakama ya Jimbo huko Karlsruhe. Hivyo walichukua hatua muhimu ili watambuliwe kisheria kuwa shirika la kidini.

Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakihubiri nchini Ujerumani kwa miaka zaidi ya 100. Walivumilia mnyanyaso mkali uliosababishwa na serikali mbili za kidikteta za karne ya 20—Serikali ya Wanazi na ya Wakomunisti. Tangu mwaka wa 1990, Mashahidi wamejaribu kutafuta kutambuliwa kisheria kuwa shirika la kidini. Baada ya maamuzi mawili ya mahakama yaliyowaunga mkono na pia uamuzi mwingine ambao haukuwaunga mkono, Mashahidi walikata rufani katika Mahakama ya Jimbo, ambayo ilitoa uamuzi wake Desemba 19, 2000.

Uamuzi wa Pamoja kwa Ajili ya Mashahidi wa Yehova

Mahakimu wote saba wa mahakama walitoa uamuzi uliowaunga mkono Mashahidi. Mahakimu hao walibatilisha uamuzi uliofanywa mwaka wa 1997 na Mahakama ya Utawala ya Jimbo na kuagiza mahakama hiyo ifikirie tena ombi la Mashahidi.

Mahakama ya Jimbo ilitumia pindi hiyo kueleza uhusiano muhimu uliopo kati ya Serikali na dini. Kwa kawaida, hali ya dini “huamuliwa, si kwa kutegemea imani ya washiriki wake, bali kwa mwenendo wao.”

Mahakama hiyo ilisema pia kwamba Mashahidi wanapodumisha “kutokuwamo kwa Kikristo,” “hawashambulii kanuni ya kidemokrasia” na “hawana haja ya kuleta serikali tofauti ili ichukue mahali pa demokrasia.” Kwa hiyo, kutojihusisha katika uchaguzi wa kisiasa hakupaswi kuchukuliwa kuwa sababu ya kukataa kuwatambua kisheria Mashahidi.—Yohana 18:36; Waroma 13:1.

Mahakama hiyo iliendelea kusema kwamba nyakati nyingine mwamini—awe ni Shahidi au mtu wa dini nyingine—anaweza kujikuta katika hali ambayo matakwa ya serikali yanahitilafiana na ya dini yake. Mtu huyo akitenda kupatana na dhamiri yake kwa “kutii zaidi imani ya kidini kuliko sheria,” huenda Serikali ikaona jambo hilo kuwa lafaa na lisilokiuka uhuru wa ibada.—Matendo 5:29.

Uamuzi huo wa mahakama ulipewa umuhimu mkubwa katika vichwa vya magazeti ya habari. Karibu magazeti yote nchini Ujerumani yaliripoti uamuzi huo. Vituo vyote vikuu vya redio na televisheni vilitangaza ripoti au mahojiano kuhusu uamuzi huo. Jina Yehova halijawahi kutangazwa sana hivyo nchini Ujerumani kama wakati huo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]

AP Photo/Daniel Maurer