Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Zingatia Kazi za Mungu za Ajabu

Zingatia Kazi za Mungu za Ajabu

Zingatia Kazi za Mungu za Ajabu

“Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi miujiza yako [“kazi zako za ajabu,” “NW”] na mawazo yako kwetu; hakuna awezaye kufananishwa nawe.”—ZABURI 40:5.

1, 2. Tuna uthibitisho gani wa kazi za Mungu za ajabu, na hilo lapasa kutuchochea tufanye nini?

USOMAPO Biblia unaweza kuona kwa urahisi kwamba Mungu alifanya mambo ya ajabu kwa ajili ya watu wake Waisraeli walioishi zamani. (Yoshua 3:5; Zaburi 106:7, 21, 22) Hata ingawa sasa Yehova haingilii shughuli za wanadamu kwa njia hiyo, tunaona uthibitisho mwingi wa kazi zake za ajabu. Kwa hiyo tuna sababu ya kujiunga na mtunga-zaburi kusema: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”—Zaburi 104:24; 148:1-5.

2 Watu wengi leo hupuuza au hukataa uthibitisho huo ulio wazi wa matendo ya Muumba. (Waroma 1:20) Hata hivyo, ingefaa tuyatafakari na kufanya maamuzi yanayopatana na msimamo wetu na wajibu wetu mbele za Muumba. Ayubu sura ya 38 hadi 41 yaweza kutusaidia sana katika jambo hilo, kwa kuwa kwenye sura hizo Yehova alimjulisha Ayubu baadhi ya kazi Zake za ajabu. Fikiria masuala fulani yafaayo ambayo Mungu alizusha.

Kazi za Ajabu na Zenye Nguvu

3. Mungu aliuliza juu ya mambo gani kwenye Ayubu 38:22-23, 25-29?

3 Wakati mmoja, Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe, nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, kwa siku ya mapigano na vita?” Theluji na mvua ya mawe hutokea katika sehemu nyingi za dunia yetu. Mungu aliendelea kumwuliza: “Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, au njia kwa umeme wa radi; kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, na kuyameza majani yaliyo mororo? Je! mvua ina baba au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? Barafu ilitoka katika tumbo la nani na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?”—Ayubu 38:22, 23, 25-29.

4-6. Ni katika maana gani mwanadamu amekosa ujuzi kamili kuhusu theluji?

4 Huenda watu fulani wanaoishi katika jamii zenye hekaheka nyingi, ambao ni lazima wasafiri, wakaiona theluji kuwa kizuizi. Hata hivyo, watu wengine huvutiwa sana na theluji wakati wa majira ya baridi kali kwa kuwa hiyo huwapa fursa ya kufanya mambo ya pekee. Unapofikiria swali ambalo Mungu aliuliza, je, wewe unaijua theluji vizuri, na je, umewahi kuiona? Tunajua jinsi rundo kubwa la theluji lilivyo, aidha kwa kuwa tumeliona kwa macho yetu wenyewe au tumeona picha zake. Lakini namna gani chembe za theluji? Je, wajua chembe za theluji zinafananaje, labda kwa kuchunguza jinsi zinavyotokea?

5 Watu fulani wamechunguza na kupiga picha chembe za theluji kwa makumi ya miaka. Chembe moja ya theluji inaweza kuwa na chembe ndogondogo mia moja za barafu zenye maumbo mbalimbali yenye kupendeza. Kitabu kiitwacho Atmosphere chasema: ‘Namna nyingi za chembe za theluji zajulikana sana, na ingawa wanasayansi wanasisitiza kwamba hakuna sheria ya asili ambayo huzuia chembe hizo zisifanane, hawajawahi kupata chembe mbili zinazofanana. Wilson A. Bentley alifanya uchunguzi mkubwa uliochukua muda wa miaka 40 kwa kutumia darubini kupiga picha chembe za theluji, lakini hakupata chembe mbili zinazofanana.’ Na hata kama angalipata chembe mbili zinazofanana, jambo ambalo ni nadra, je, hilo lingebadili kwa njia yoyote maajabu tunayoona katika namna nyingi za chembe za barafu?

6 Kumbuka swali la Mungu: “Je! umeziingia ghala za theluji?” Wengi hufikiria mawingu kuwa ghala za theluji. Je, waweza kuwazia ukiingia katika ghala hizo kuhesabu chembe za theluji za namna nyingi sana na kuchunguza jinsi zilivyotokea? Ensaiklopidia moja ya sayansi yasema hivi: ‘Asili ya kiini cha barafu, ambacho husababisha matone ya maji kwenye mawingu yagande wakati wa baridi kali, haijulikani bado.’—Zaburi 147:16, 17; Isaya 55:9, 10.

7. Mwanadamu ana ujuzi mwingi kadiri gani kuhusu mvua?

7 Namna gani mvua? Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?” Ensaiklopidia hiyohiyo yasema hivi: ‘Ni vigumu kwa wanasayansi kueleza jinsi ambavyo mawingu na matone ya mvua hutokea kwa sababu kuna utendaji mwingi tata katika angahewa na kiwango cha mvuke na chembe zilizo hewani hubadilika-badilika.’ Kwa maneno sahili, wanasayansi wametoa dhana zenye maelezo mengi, lakini hawawezi kueleza kikamili jinsi ambavyo mvua hutokea. Hata hivyo, unajua kwamba mvua ambayo ni muhimu hunyesha na kuitia dunia maji. Husitawisha mimea na hutuwezesha kuishi na kufurahia maisha.

8. Kwa nini maneno ya Paulo kwenye Matendo 14:17 yafaa?

8 Je, hukubaliani na kauli aliyokata mtume Paulo? Aliwahimiza wengine waone kazi za Mungu za ajabu kuwa zatoa ushuhuda juu ya Yule aliyezifanya. Paulo alisema hivi kumhusu Yehova Mungu: “Hakujiacha mwenyewe bila ushahidi kwa kuwa alitenda mema, akiwapa nyinyi mvua kutoka mbinguni na majira yenye kuzaa matunda, akijaza mioyo yenu kikamili kwa chakula na uchangamfu.”—Matendo 14:17; Zaburi 147:8.

9. Kazi za Mungu za ajabu hudhihirishaje nguvu zake kuu?

9 Bila shaka Mtekelezaji wa mambo hayo ya ajabu na yenye kunufaisha ana hekima na nguvu nyingi sana. Fikiria jambo hili kuhusu nguvu zake: Yasemekana kwamba kuna mvua za umeme na ngurumo zipatazo 45,000 zinazotokea kila siku, zaidi ya milioni 16 kwa mwaka. Hilo lamaanisha kwamba kuna mvua za aina hiyo zipatazo 2,000 zinazonyesha sasa hivi. Mawingu tata ya mvua moja ya umeme na ngurumo hutokeza nguvu zinazotoshana na nguvu za mabomu kumi au zaidi ya nyuklia yaliyoangushwa katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Baadhi ya nguvu hizo huonekana zikiwa umeme. Licha ya kuwa yenye kuogofya, mimweko ya umeme husaidia hasa kutokeza nitrojeni za namna mbalimbali zinazoufikia udongo na kufyonzwa na mimea zikiwa mbolea ya asili. Kwa hiyo umeme ni nguvu ionekanayo, yenye manufaa halisi.—Zaburi 104:14, 15.

Unafikia Mkataa Gani?

10. Ungejibuje maswali yanayoulizwa kwenye Ayubu 38:33-38?

10 Hebu wazia kuwa wewe ni Ayubu na unaulizwa maswali na Mungu Mweza Yote. Yaelekea utakubali kwamba watu wengi hawazingatii sana kazi za Mungu za ajabu. Yehova anatuuliza maswali tusomayo kwenye Ayubu 38:33-38. “Je! unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, ukakuambia, Sisi tupo hapa? Je! ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? Wakati mavumbi yagandamanapo, na madongoa kushikamana pamoja?”

11, 12. Ni baadhi ya mambo gani yanayothibitisha kwamba Mungu ni Mtekelezaji wa kazi za ajabu?

11 Tumezungumzia mambo machache tu ambayo Elihu alimwuliza Ayubu, kisha tumeona baadhi ya maswali ambayo Yehova alimwuliza Ayubu ajibu “kama mwanamume.” (Ayubu 38:3) Twasema “baadhi” kwa sababu katika Ayubu sura ya 38 na 39, Mungu alikazia fikira uumbaji mwingine mbalimbali wenye kutokeza. Kwa mfano, alitaja makundi ya nyota yaliyo katika mbingu. Ni nani ajuaye amri au sheria zake zote? (Ayubu 38:31-33) Yehova alimtajia Ayubu wanyama fulani—simba na kunguru, mbuzi-mwitu na punda-milia, nyati na mbuni, kisha farasi na tai. Ni kana kwamba Mungu alimwuliza Ayubu iwapo alikuwa amewapa wanyama hao mbalimbali tabia zao na kuwawezesha kuishi na kusitawi. Huenda ukafurahia kusoma sura hizo, hasa ikiwa wewe unapendezwa na farasi au wanyama wengineo.—Zaburi 50:10, 11.

12 Waweza pia kuchunguza Ayubu sura ya 40 na 41, ambapo Yehova amwomba tena Ayubu ajibu maswali yake juu ya viumbe wawili hususa. Twawajua viumbe hao, nao ni kiboko (Behemothi), mwenye mwili mkubwa na mwenye nguvu, na mamba wa Naili (Leviathani) mwenye kuogofya. Kila mmoja wao ni kiumbe wa ajabu asiyepasa kupuuzwa. Acheni sasa tuone yatupasa kukata kauli gani.

13. Maswali ya Mungu yalikuwa na matokeo gani kwa Ayubu, nayo yapasa kuwa na matokeo gani kwetu?

13 Ayubu sura ya 42 yatuonyesha maswali ya Mungu yalikuwa na matokeo gani kwa Ayubu. Awali, Ayubu alikuwa akijifikiria mwenyewe na wanadamu wengine kupita kiasi. Lakini, kwa kuwa alikubali sahihisho lililodokezwa na maswali ya Mungu, Ayubu alibadili maoni yake. Alikiri hivi: “Najua ya kuwa [wewe Yehova] waweza kufanya mambo yote, na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa? Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu, mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.” (Ayubu 42:2, 3) Naam, baada ya kuzingatia kazi za Mungu, Ayubu alisema kwamba kazi hizo zilikuwa za ajabu sana. Baada ya kuzungumzia maajabu hayo ya uumbaji, sisi pia twapaswa kuvutiwa na hekima na nguvu za Mungu. Kwa madhumuni gani? Je, ni ili tu tuvutiwe na nguvu na uwezo mwingi wa Yehova? Au twapaswa kuchochewa kufanya mengi zaidi?

14. Daudi alizionaje kazi za Mungu za ajabu?

14 Katika Zaburi 86, tunapata maneno yanayofanana na hayo ambayo yalisemwa na Daudi katika Zaburi fulani iliyotangulia: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake. Mchana husemezana na mchana, usiku hutolea usiku maarifa.” (Zaburi 19:1, 2) Lakini Daudi alisema mengi zaidi. Kwenye Zaburi 86:10, 11 twasoma hivi: “[Wewe] ndiwe uliye mkuu, wewe ndiwe mfanya miujiza, ndiwe Mungu peke yako. Ee BWANA, unifundishe njia yako; nitakwenda katika kweli yako; moyo wangu na ufurahi kulicha jina lako.” Daudi alikuwa na hofu yenye staha kwa Muumba kwa sababu ya kazi Zake zote za ajabu. Waweza kuona ni kwa nini. Daudi hakutaka kumchukiza Yule awezaye kufanya kazi hizo za ajabu. Wala sisi hatupaswi kumchukiza.

15. Kwa nini hofu yenye staha ya Daudi kwa Mungu ilifaa?

15 Ni lazima Daudi awe alitambua kwamba kwa kuwa Mungu ana nguvu nyingi anazoweza kutumia vile atakavyo, aweza kuzitumia dhidi ya yeyote asiyestahili fadhili zake. Hilo ni onyo kwao. Mungu alimwuliza Ayubu hivi: “Je! umeziingia ghala za theluji, au umeziona ghala za mvua ya mawe, nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, kwa siku ya mapigano na vita?” Theluji, mvua ya mawe, dhoruba za mvua, upepo, na umeme, zote hizo ni silaha za Mungu. Nazo ni kani za asili zilizo nyingi kama nini!—Ayubu 38:22, 23.

16, 17. Nguvu kuu za Mungu hudhihirishwa na nini, naye ametumiaje nguvu hizo wakati uliopita?

16 Huenda wakumbuka msiba fulani uliosababishwa na mojawapo ya mambo hayo—iwe kimbunga, dhoruba ya mvua ya mawe, au furiko la ghafula. Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka wa 1999, dhoruba kubwa ilikumba kusini-magharibi mwa Ulaya. Iliwashangaza hata wataalamu wa hali ya anga. Pepo zenye nguvu zilifikia mwendo wa kilometa 200 kwa saa, ziking’oa maelfu ya paa, zikiangusha nguzo za chuma za kuegemeza nyaya za nguvu za umeme, na kuangusha magari. Hebu wazia hili: Dhoruba hiyo iling’oa au kuvunja miti ipatayo milioni 270. Miti 10,000 kati ya hiyo ilikuwa katika bustani ya Versailles, nje ya Paris. Mamilioni ya nyumba yaliachwa bila umeme. Karibu watu 100 walikufa. Uharibifu wote huo ulichukua muda mfupi sana. Ni nguvu zilizoje!

17 Mtu anaweza kuita dhoruba tukio lisilo la kawaida, lisilo na mwelekezo na lisilodhibitiwa. Hata hivyo, hali ingekuwaje iwapo Yule mwenye nguvu zote, angefanya kazi za ajabu kwa kutumia kani hizo kwa njia inayodhibitiwa, chini ya mwelekezo wake? Alifanya jambo kama hilo zama za Abrahamu, ambaye alijifunza kwamba Hakimu wa dunia yote alikuwa amezingatia uovu wa majiji mawili, Sodoma na Gomora. Majiji hayo yalikuwa na ufisadi mwingi sana hivi kwamba malalamiko mengi dhidi yake yalimfikia Mungu, ambaye aliwasaidia waadilifu wote kukimbia majiji hayo yaliyohukumiwa adhabu. Historia yasema hivi: ‘Ndipo BWANA akanyesha kiberiti na moto toka mbinguni,’ juu ya miji hiyo ya kale. Ilikuwa kazi ya ajabu kuwahifadhi waadilifu na kuwaharibu watu hao waliokuwa waovu kupita kiasi.—Mwanzo 19:24.

18. Isaya sura ya 25 inazungumzia mambo gani ya ajabu?

18 Baadaye, Mungu alikata kauli kuhukumu Babiloni, mji wa kale ambao waweza kuwa ndio mji unaorejezewa kwenye Isaya sura ya 25. Mungu alitabiri kwamba mji huo ungekuwa magofu: “Umefanya mji kuwa ni chungu; mji wenye boma kuwa ni magofu; jumba la wageni kuwa si mji; hautajengwa tena milele.” (Isaya 25:2) Watu wanaozuru leo mahali ulipokuwa Babiloni wa kale waweza kuthibitisha kwamba ndivyo ilivyo. Je, kuharibiwa kwa Babiloni kulitukia kiaksidenti tu? La. Badala yake twaweza kukubali maoni ya Isaya: “Ee BWANA, wewe u Mungu wangu; nitakutukuza na kulihimidi jina lako; kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu, mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.”—Isaya 25:1.

Kazi za Ajabu Wakati Ujao

19, 20. Tunaweza kutarajia utimizo gani wa Isaya 25:6-8?

19 Mungu alitimiza unabii ambao umetajwa hapo juu wakati uliopita, naye atafanya hivyo kwa njia ya ajabu wakati ujao. Katika muktadha huo, ambapo Isaya anataja “mambo ya ajabu” ya Mungu, tunapata unabii wenye kutegemeka ambao utatimizwa, kama vile tu hukumu dhidi ya Babiloni ilivyotimizwa. Ni ‘jambo gani la ajabu’ linaloahidiwa? Andiko la Isaya 25:6 lasema hivi: “Katika mlima huu BWANA wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.”

20 Bila shaka unabii huo utatimizwa katika ulimwengu mpya ulio karibu, ambao Mungu ameahidi. Wakati huo, wanadamu wataondolewa matatizo yanayowalemea wengi leo. Kwa kweli unabii wa Isaya 25:7, 8 wahakikisha kwamba Mungu atatumia nguvu zake za uumbaji kufanya mojawapo ya kazi za ajabu zaidi zisizo na kifani: “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo.” Baadaye mtume Paulo alinukuu andiko hilo na kulitumia kuonyesha jinsi Mungu atakavyowafufua wafu. Hiyo itakuwa kazi ya ajabu kama nini!—1 Wakorintho 15:51-54.

21. Ni kazi gani za ajabu ambazo Mungu atawafanyia wafu?

21 Jambo jingine litakalofanya machozi ya huzuni yaishe ni kwamba magonjwa yataondolewa. Yesu alipokuwa duniani aliwaponya wengi, akawawezesha vipofu kuona, viziwi kusikia, na kuwapa nguvu walemavu. Andiko la Yohana 5:5-9 lasema kwamba alimponya mtu aliyekuwa kilema kwa miaka 38. Watazamaji waliona jambo hilo kuwa kazi ya ajabu sana. Nalo kwa kweli lilikuwa kazi ya ajabu! Lakini Yesu aliwaambia kwamba kufufuliwa kwa wafu ndilo litakalokuwa jambo la ajabu zaidi: “Msistaajabie hili, kwa sababu saa inakuja ambayo katika hiyo wote wale waliomo ndani ya makaburi ya ukumbusho watasikia sauti yake na kutoka, wale waliofanya mambo mema kwenye ufufuo wa uhai, wale waliozoea kufanya mambo maovu kwenye ufufuo wa hukumu.”—Yohana 5:28, 29.

22. Kwa nini maskini na wenye kuonewa watazamie wakati ujao kwa matumaini?

22 Bila shaka hilo litatukia kwa kuwa Yehova ndiye anayetoa ahadi hiyo. Waweza kuwa na hakika kwamba atumiapo na kuelekeza kwa uangalifu nguvu zake kuu za kuponya, matokeo yatakuwa ya ajabu. Andiko la Zaburi 72 hutaja atakayofanya kupitia Mwanaye Mfalme. Kisha waadilifu watasitawi na amani itakuwa tele. Mungu atawakomboa maskini na watu walioonewa. Anaahidi hivi: “Na uwepo wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima; matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni [ya kale], na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.”—Zaburi 72:16.

23. Kazi za Mungu za ajabu zapasa kutuchochea tufanye nini?

23 Ni wazi kwamba tuna sababu nyingi za kuzingatia kazi za Yehova za ajabu—mambo aliyofanya wakati uliopita, anayofanya leo na atakayofanya karibuni. “Na ahimidiwe BWANA, Mungu, Mungu wa Israeli, atendaye miujiza [“kazi za ajabu,” NW] Yeye peke yake; jina lake tukufu na lihimidiwe milele; dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.” (Zaburi 72:18, 19) Yatupasa kuzungumzia mambo hayo kwa ukawaida na kwa shauku pamoja na jamaa zetu na wengineo. Naam, acheni ‘tuwahubiri mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake.’—Zaburi 78:3, 4; 96:3, 4.

Ungejibuje?

• Maswali aliyoulizwa Ayubu yanakaziaje kwamba mwanadamu hana ujuzi kamili?

• Umevutiwa na mifano gani ya kazi za Mungu za ajabu zinazokaziwa kwenye Ayubu sura ya 37-41?

• Twapaswa kutendaje baada ya kuzingatia baadhi ya kazi za Mungu za ajabu?

[Maswali ya Funzo]

[Picha katika ukurasa wa 10]

Unafikia mkataa gani kuhusu namna nyingi za chembe za barafu na mimweko yenye kuogofya ya umeme?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

snowcrystals.net

[Picha katika ukurasa wa 13]

Zungumzia kwa ukawaida kazi za Mungu za ajabu