Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Heri Mtu Yule Aonaye Hekima”

“Heri Mtu Yule Aonaye Hekima”

“Heri Mtu Yule Aonaye Hekima”

ALIKUWA mshairi, msanifu wa majengo, mfalme. Akiwa na pato la dola za Marekani zaidi ya milioni 200 kwa mwaka, ndiye aliyekuwa mfalme tajiri kuliko wafalme wote duniani. Mtu huyo pia alikuwa maarufu kwa hekima yake. Malkia mmoja aliyemtembelea alivutiwa sana na kusema hivi kwa mshangao: “Tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.” (1 Wafalme 10:4-9) Hiyo ndiyo iliyokuwa hadhi ya Mfalme Solomoni wa Israeli la kale.

Solomoni alikuwa na utajiri na hekima pia. Hali hiyo isiyo ya kawaida ya kuwa na utajiri na hekima ilimfanya Solomoni aweze kuchanganua na kuamua ni nini kilichokuwa muhimu zaidi. Aliandika hivi: “Heri mtu yule aonaye hekima, na mtu yule apataye ufahamu. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi. Yeye ana thamani kuliko marijani, wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.”—Mithali 3:13-15.

Ingawa hivyo, hekima yaweza kupatikana wapi? Kwa nini ni yenye thamani zaidi kuliko mali? Ni mambo gani yenye kuvutia kuhusu hekima? Sura ya 8 ya kitabu cha Biblia cha Mithali, iliyoandikwa na Solomoni, yajibu maswali hayo kwa njia yenye kuvutia. Katika sura hiyo hekima yafananishwa na mtu, kana kwamba inaweza kuzungumza na kutenda. Na hekima yaonyesha jinsi inavyovutia na vilevile thamani yake.

“Anapiga Kelele”

Sura ya 8 ya Mithali yaanza kwa swali lisilohitaji jibu: “Je! hekima halii? ufahamu hatoi sauti yake?” * Naam, hekima na ufahamu waendelea kulia, lakini kwa njia iliyo tofauti kabisa na mwanamke asiye na maadili anayeotea mahali penye giza na kumnong’onezea maneno ya utongozi kijana asiye na ujuzi. (Mithali 7:12) “Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo. Karibu na malango, mahali pa kuingia mjini, mahali pa kuyaingilia malango anapiga kelele.” (Mithali 8:1-3) Sauti kubwa na ya ujasiri ya hekima yasikika kwa nguvu na waziwazi mahali pa umma—malangoni, penye njia panda, mahali pa kuingia mjini. Watu wanaweza kusikia sauti hiyo kwa urahisi na kuitikia.

Ni nani awezaye kukana kwamba karibu kila mtu duniani anaweza kupata hekima ya Mungu iliyo katika Neno lake lililopuliziwa, Biblia? “Biblia ni kitabu ambacho kimesomwa na watu wengi zaidi katika historia,” chasema kichapo The World Book Encyclopedia. Chaongezea hivi: “Biblia ndiyo imegawanywa kwa wingi zaidi kuliko kitabu kingine chochote. Biblia imetafsiriwa pia mara nyingi zaidi, na katika lugha nyingi zaidi, kuliko kitabu kingine chochote.” Kwa kuwa Biblia nzima au visehemu vyake vyapatikana katika lugha na lahaja zaidi ya 2,100, zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaweza kusoma angalau sehemu fulani ya Neno la Mungu katika lugha yao wenyewe.

Mashahidi wa Yehova wanatangaza hadharani ujumbe wa Biblia kotekote. Katika nchi 235, wanahubiri kwa bidii habari njema za Ufalme wa Mungu na kufundisha watu kweli inayopatikana katika Neno la Mungu. Nakala zaidi ya milioni 20 hugawanywa za majarida yao yanayotegemea Biblia ambayo ni Mnara wa Mlinzi, jarida linalochapishwa katika lugha zaidi ya 140, na Amkeni! jarida linalochapishwa katika lugha 83. Bila shaka, hekima inaendelea kupiga kelele katika mahali pa umma!

“Sauti Yangu Ni kwa Wanadamu”

Hekima inayofananishwa na mtu yaanza kwa kusema hivi: “Enyi watu, nawaita ninyi; na sauti yangu ni kwa wanadamu. Enyi wajinga, fahamuni werevu, nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu.”Mithali 8:4, 5.

Mwito wa hekima unawafikia wanadamu kila mahali. Unaalika wanadamu wote. Hata wale wasio na uzoefu wanaalikwa kujipatia werevu, au busara, na wapumbavu wapate uelewevu. Kwa kweli, Mashahidi wa Yehova wanaamini kwamba Biblia ni kitabu kwa ajili ya watu wote nao hujitahidi pasipo ubaguzi wowote kutia moyo kila mtu wanayezungumza naye kuichunguza na kupata maneno ya hekima yaliyomo.

‘Kinywa Changu Husema Kweli’

Ikipanua mwaliko wake, hekima yaendelea kusema: “Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili. Maana kinywa changu kitasema kweli, na uovu ni chukizo kwa midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi.” Naam, mafundisho ya hekima ni bora kabisa na ya unyofu, ni ya kweli na ya uadilifu. Hayana udanganyifu au upotovu wowote. “Yote humwelea yule afahamuye, yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.”—Mithali 8:6-9.

Kwa kufaa, hekima yahimiza hivi: “Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, na maarifa kuliko dhahabu safi.” Ombi hilo ni la busara, “maana hekima ni bora kuliko marijani; wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.” (Mithali 8:10, 11) Lakini ni kwa nini? Ni nini hufanya hekima iwe yenye thamani kuliko mali?

“Matunda Yangu Hupita Dhahabu”

Zawadi wanazopata wale wanaoisikiliza hekima ni zenye thamani zaidi ya dhahabu, fedha, au marijani. Ikifafanua zawadi hizo, hekima yasema hivi: “Mimi, hekima, nimefanya werevu kuwa kao langu; natafuta maarifa na busara. Kumcha BWANA ni kuchukia uovu; kiburi na majivuno, na njia mbovu, na kinywa cha ukaidi pia nakichukia.”Mithali 8:12, 13.

Hekima humpa yule aliye nayo werevu na maarifa. Mtu mwenye hekima ya kimungu ana staha na kicho pia kuelekea Mungu, kwa kuwa “kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima.” (Mithali 9:10) Kwa hiyo, anachukia kile Yehova anachochukia. Hana kiburi, wala majivuno, wala njia mbovu, wala kinywa cha ukaidi. Kuchukia lililo ovu humzuia asitumie mamlaka kwa njia ya kibinafsi. Ni jambo la maana kama nini kwamba wale wenye madaraka katika kutaniko la Kikristo, pamoja na vichwa vya familia, watafute hekima!

“Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi,” hekima yaendelea kusema. “Mimi ni ufahamu, mimi nina nguvu. Kwa msaada wangu wafalme humiliki, na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia.” (Mithali 8:14-16) Matunda ya hekima yatia ndani ufahamu wenye kina, uelewevu, na nguvu—sifa zinazohitajiwa sana na watawala, maofisa wa cheo cha juu, na wakuu. Hekima ni muhimu kwa wale walio na mamlaka na wale wanaowashauri wengine.

Hekima ya kweli hupatikana kwa wote kwa urahisi lakini si wote wanaoipata. Wengine huikataa au kuikwepa, hata wakati wanapoweza kuipata kwa urahisi. “Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” yasema hekima. (Mithali 8:17) Hekima hupatikana tu kwa wale wanaoitafuta kwa bidii.

Njia za hekima ni za unyofu na uadilifu. Huwanufaisha wale wanaoitafuta. Hekima husema: “Utajiri na heshima ziko kwangu, naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, na faida yangu hupita fedha iliyo teule. Natembea katika njia ya haki, katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, tena nipate kuzijaza hazina zao.”Mithali 8:18-21.

Zawadi za hekima zatia ndani sifa bora kabisa kama vile busara, uwezo wa kufikiri, unyenyekevu, ufahamu wenye kina, hekima itumikayo, na uelewevu, na vilevile mali na heshima. Mtu mwenye hekima anaweza kupata mali kwa njia ya uadilifu, na atasitawi kiroho. (3 Yohana 2) Hekima humfanya mtu aheshimike pia. Isitoshe, anaridhika na kile anachopata, na ana amani ya akili na dhamiri safi mbele za Mungu. Naam, heri mtu yule aonaye hekima. Kwa kweli matunda ya hekima ni bora kuliko dhahabu safi na fedha iliyo teule.

Shauri hilo ni la wakati unaofaa kama nini kwetu, kwa kuwa tunaishi katika ulimwengu unaofuatia vitu vya kimwili na ambao hukazia kupata mali kwa njia yoyote ile! Na tusisahau kamwe thamani ya hekima wala tusitumie njia zisizo za haki kujipatia mali. Na tusipuuze kamwe maandalizi hasa yanayotoa hekima—mikutano yetu ya Kikristo na funzo la kibinafsi la Biblia na vichapo vinavyoandaliwa na “mtumwa mwaminifu na mwenye busara”—kwa ajili tu ya kujipatia mali.—Mathayo 24:45-47.

“Nalitukuka Tokea Milele”

Katika sura ya 8 ya Mithali hekima haifananishwi na mtu ili kufafanua sifa fulani ya kuwazia tu. Kwa njia ya ufananisho, hekima yarejezea pia uumbaji wa Yehova ulio wa maana zaidi. Hekima yaendelea kusema: “BWANA alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, kabla ya matendo yake ya kale. Nalitukuka tokea milele, tangu awali, kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde wala chanzo cha mavumbi ya dunia.”Mithali 8:22-26.

Ufafanuzi uliotangulia wa hekima inayofananishwa na mtu walingana kama nini na yale yanayosemwa na Maandiko kuhusu “Neno”! “Hapo mwanzoni Neno alikuwako, na Neno alikuwa pamoja na Mungu, na Neno alikuwa mungu,” akaandika mtume Yohana. (Yohana 1:1) Hekima inayofananishwa na mtu yawakilisha kwa njia ya mfano Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, kabla ya kuwa mwanadamu. *

Yesu Kristo ni “mzaliwa wa kwanza wa uumbaji wote; kwa sababu kwa njia yake vitu vingine vyote viliumbwa katika mbingu na juu ya dunia, vitu vinavyoonekana na vitu visivyoonekana.” (Wakolosai 1:15, 16) Hekima inayofananishwa na mtu yaendelea kusema: [Yehova] alipozithibitisha mbingu nalikuwako; alipopiga duara katika uso wa bahari; alipofanya imara mawingu yaliyo juu; chemchemi za bahari zilipopata nguvu; alipoipa bahari mpaka wake, kwamba maji yake yasiasi amri yake; alipoiagiza misingi ya nchi; ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; nikawa furaha yake kila siku; nikifurahi daima mbele zake; nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.” (Mithali 8:27-31) Mwana mzaliwa wa kwanza wa Yehova alikuwa kando ya Baba yake, akifanya kazi kwa bidii pamoja naye—Muumba asiye na kifani wa mbingu na dunia. Yehova Mungu alipoumba mwanadamu wa kwanza, Mwana Wake alishiriki kazi hiyo akiwa Stadi wa Kazi. (Mwanzo 1:26) Si ajabu kwamba Mwana wa Mungu anawapenda sana wanadamu!

“Ana Heri Mtu Yule Anisikilizaye”

Akiwa kama hekima inayofananishwa na mtu, Mwana wa Mungu asema: “Basi, wanangu, nisikilizeni sasa; maana heri hao wazishikao amri zangu. Sikieni mafundisho, mpate hekima, wala msiikatae. Ana heri mtu yule anisikilizaye, akisubiri sikuzote malangoni pangu, akingoja penye vizingiti vya milango yangu. Maana yeye anionaye mimi aona uzima, naye atapata kibali kwa BWANA. Bali anikosaye hujidhuru nafsi yake mwenyewe, na wao wanichukiao hupenda mauti.”Mithali 8:32-36.

Yesu Kristo ndiye mfano halisi wa hekima ya Mungu. “Zenye kusitiriwa kwa uangalifu ndani yake ni hazina zote za hekima na za ujuzi.” (Wakolosai 2:3) Acheni basi, tumsikilize kwa makini na kufuata hatua zake kwa ukaribu. (1 Petro 2:21) Kumkataa ni kuangamiza nafsi yetu wenyewe na kupenda kifo, kwa kuwa “hakuna wokovu katika mwingine yeyote.” (Matendo 4:12) Kwa kweli, acheni tumkubali Yesu kuwa mtu ambaye Mungu ametoa kwa ajili ya wokovu wetu. (Mathayo 20:28; Yohana 3:16) Kwa kufanya hivyo tutapata furaha inayotokana na ‘kuona uzima na kupata kibali kwa Yehova.’

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Neno la Kiebrania lililotafsiriwa “hekima” liko katika ngeli ya kike. Kwa hiyo, watafsiri fulani hutumia viwakilishi vya ngeli ya kike wanaporejezea hekima.

^ fu. 25 Uhakika wa kwamba neno la Kiebrania “hekima” sikuzote huwa katika ngeli ya kike haupingani na matumizi ya hekima kuwakilisha Mwana wa Mungu. Neno la Kigiriki “upendo” katika usemi “Mungu ni upendo” liko katika ngeli ya kike pia. (1 Yohana 4:8) Hata hivyo, linatumiwa kurejezea Mungu.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Hekima ni muhimu sana kwa wale walio na madaraka

[Picha katika ukurasa wa 27]

Usipuuze maandalizi yanayotoa hekima