Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

‘Kimbieni kwa Njia Hiyo’

‘Kimbieni kwa Njia Hiyo’

‘Kimbieni kwa Njia Hiyo’

HEBU wazia ukiwa katika uwanja wa michezo ambao umejaa watu wenye msisimuko. Wanariadha wanaingia uwanjani. Umati unapiga kelele mashujaa wao wanapoingia. Waamuzi wako karibu na tayari kutekeleza sheria. Kuna mchanganyiko wa vigelegele vya ushindi na sauti za kuvunjika moyo, mashindano yanapoendelea. Washindi wanashangiliwa kwa vifijo!

Unahudhuria, si mashindano ya kisasa ya riadha bali mashindano yaliyofanywa miaka 2,000 iliyopita katika shingo ya nchi iitwayo Isthmus ya Korintho. Kwenye eneo hilo, Michezo ya Isthmus iliyokuwa maarufu sana ilifanywa kila baada ya miaka miwili kuanzia karne ya sita K.W.K. hadi karne ya nne W.K. Kwa muda mrefu mashindano hayo yalivutia Ugiriki yote. Michezo hiyo haikuwa mashindano tu ya riadha. Wanariadha walikuwa wonyesho wa utayari wa kijeshi. Washindi—mashujaa waliochukuliwa kama miungu—walipokea taji zilizotengenezwa kwa majani ya miti. Walipewa zawadi nyingi, nalo jiji liliwapa pensheni kubwa kwa maisha yao yote.

Mtume Paulo aliifahamu Michezo hiyo ya Isthmus iliyofanywa karibu na Korintho na hivyo kulinganisha maisha ya Mkristo na mashindano ya riadha. Kwa kurejezea wakimbiaji, wapiganaji mieleka na wanandondi, Paulo alitoa mfano ufaao wa kuonyesha manufaa ya mazoezi mazuri, nguvu zilizotumiwa vizuri, na uvumilivu. Bila shaka, Wakristo alioandikia pia waliifahamu michezo hiyo. Yaelekea baadhi yao walikuwa miongoni mwa umati uliopiga kelele kwenye uwanja wa michezo. Kwa hiyo wangeelewa mifano ya Paulo kwa urahisi. Namna gani sisi leo? Sisi pia tumo katika shindano la mbio—la kupata uhai udumuo milele. Tunaweza kunufaikaje kutokana na kurejezea kwa Paulo mashindano hayo?

Kushindana Kulingana na Kanuni’

Matakwa ya kujiunga na michezo hiyo ya kale yalikuwa makali sana. Mpiga-mbiu fulani alitokeza kila mwanariadha mbele ya watazamaji kisha akapaaza sauti: ‘Je, kuna yeyote anayeweza kumshtaki mtu huyu kwa uhalifu wowote? Je, yeye ni mpokonyaji au ni mtu mwovu, mwenye maisha na tabia zilizopotoka?’ Kulingana na Archaeologia Graeca, “hakuna mtu ambaye alikuwa mhalifu sugu, au mtu wa ukoo [wa karibu] wa mtu kama huyo ambaye angeruhusiwa kushiriki katika mashindano.” Na waliovunja kanuni za michezo hiyo waliadhibiwa vikali kwa kuzuiwa kushiriki katika mashindano.

Jambo hilo latusaidia kuelewa maneno haya ya Paulo: “Ikiwa yeyote ashindana hata katika michezo, havikwi taji isipokuwa awe ameshindana kulingana na kanuni.” (2 Timotheo 2:5) Vivyo hivyo, ili kushiriki katika shindano la mbio la kupata uhai, yatupasa kutimiza matakwa ya Yehova na kushika viwango vyake vya juu kama vionyeshwavyo katika Biblia. Hata hivyo, Biblia yatuonya: “Mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake.” (Mwanzo 8:21) Hivyo, hata baada ya kujiunga na shindano la mbio, yatupasa kuwa waangalifu ili kuendelea kushindana kulingana na kanuni kusudi tuendelee kukubalika kwa Yehova na kupata uhai udumuo milele.

Kumpenda Mungu hutusaidia sana kufanya hivyo. (Marko 12:29-31) Upendo huo utatufanya tutake kumpendeza Yehova na kutenda kulingana na mapenzi yake.—1 Yohana 5:3.

‘Ondoeni Kila Uzito’

Katika michezo hiyo ya zamani, wakimbiaji hawakulemewa na mavazi au vifaa. “Katika mashindano ya mbio za miguu, . . . wakimbiaji walikuwa wakitokea wakiwa uchi kabisa,” chasema kitabu The Life of the Greeks and Romans. Kutokuwa na mavazi yoyote kulifanya wanariadha wawe wepesi na waweze kukimbia kwa urahisi. Hakuna nishati zilizopotea bure kutokana na uzito usio wa lazima. Yaelekea Paulo alikumbuka jambo hilo alipowaandikia Wakristo Waebrania hivi: “Acheni sisi pia tuondoe kila uzito . . . , na acheni tukimbie kwa uvumilivu shindano la mbio lililowekwa mbele yetu.”—Waebrania 12:1.

Tunaweza kuzuiwa na aina gani ya uzito katika shindano letu la mbio la kupata uhai? Mojawapo ingekuwa tamaa ya kurundika vitu vya kimwili visivyohitajika au kuishi maisha ambayo ni ghali sana. Huenda wengine wakategemea mali ili kupata usalama au kuiona kuwa chanzo cha furaha. “Uzito” huo wa ziada waweza kufanya mkimbiaji apunguze mwendo kiasi kwamba, huenda hatimaye akamchukua Mungu kivivi hivi. (Luka 12:16-21) Huenda uhai udumuo milele ukaja kuonekana kama tumaini lililo mbali. ‘Ulimwengu mpya utakuja wakati fulani,’ huenda mtu akasababu, ‘lakini kwa sasa acheni tujinufaishe na mambo ya ulimwengu huu.’ (1 Timotheo 6:17-19) Mtazamo huo wa kufuatia vitu vya kimwili waweza kukengeusha mtu kwa urahisi sana atoke katika shindano la mbio la kupata uhai au kumzuia hata asianze shindano hilo.

Katika Mahubiri ya Mlimani, Yesu alisema: “Hakuna awezaye kutumikia kama mtumwa mabwana-wakubwa wawili; kwa maana ama atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, ama atashikamana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kutumikia kama watumwa Mungu na Utajiri.” Kisha baada ya kutaja jinsi ambavyo Yehova hushughulikia mahitaji ya wanyama na mimea na kusema kwamba wanadamu ni wenye thamani kuliko wanyama na mimea, alishauri hivi: “Kwa hiyo msihangaike kamwe na kusema, ‘Tule nini?’ au, ‘Tunywe nini?’ au, ‘Tuvae nini?’ Kwa maana vyote hivi ndivyo vitu ambavyo mataifa yanafuatia kwa hamu. Kwa maana Baba yenu wa kimbingu ajua mwahitaji vitu hivi vyote. Basi, fulizeni kutafuta kwanza ufalme na uadilifu wake, na vitu vingine vyote hivi mtaongezewa.”—Mathayo 6:24-33.

“Tukimbie kwa Uvumilivu”

Si mashindano yote ya kale ya mbio za miguu yaliyokuwa mafupi. Shindano moja lililoitwa doʹli·khos, lilikuwa na urefu upatao kilometa nne. Shindano hilo lilijaribu uvumilivu na nguvu za mtu sana. Kulingana na desturi, baada ya kushinda shindano hilo mwaka wa 328 K.W.K. mwanariadha aitwaye Ageas alikimbia kwenda Argos, jiji la kwao nyumbani, ili kutangaza ushindi wake. Siku hiyo alikimbia umbali upatao kilometa 110!

Shindano la mbio la Kikristo pia ni la masafa marefu ambalo hujaribu uvumilivu wetu. Tunahitaji kuvumilia hadi mwisho katika shindano hilo ili kupata kibali cha Yehova na tuzo la uhai udumuo milele. Paulo alikimbia shindano hilo la mbio kwa njia kama hiyo. Alipokaribia kufa, aliweza kusema hivi: “Nimepigana pigano bora, nimekimbia mwendo hadi mwisho, nimeshika imani. Tangu wakati huu na kuendelea kumewekwa akiba kwa ajili yangu taji la uadilifu.” (2 Timotheo 4:7, 8) Kama Paulo, ni lazima tukimbie “hadi mwisho.” Ikiwa uvumilivu wetu utapungua kwa sababu tu shindano ni refu kidogo kuliko vile tulivyotazamia mwanzoni, tutakosa tuzo letu. (Waebrania 11:6) Huo ungekuwa msiba ulioje, kwa kuwa tuko karibu sana na mwisho!

Tuzo

Washindi katika mashindano ya riadha katika Ugiriki ya zamani walikuwa wakipewa shada la maua ambalo kwa kawaida lilitengenezwa kwa majani ya miti na kupambwa kwa maua. Katika Michezo ya Pythia, washindi walipokea taji lililotengenezwa kwa laurusi. Katika Michezo ya Olimpiki walipata mataji ya majani ya mizeituni-mwitu, ilhali katika Michezo ya Isthmus walipewa mataji ya msonobari. “Ili kuwahamasisha washindanaji,” asema msomi mmoja wa Biblia, “mataji, thawabu za ushindi, na matawi ya mchikichi, yaliwekwa wazi mbele yao, juu ya kigoda au meza iliyokuwa ndani ya uwanja.” Ilikuwa ishara ya heshima kubwa kwa mshindi kuvaa taji. Aliporudi nyumbani, aliingia jijini kwa shangwe ya ushindi huku akiwa amepanda gari la vita.

Akikumbuka jambo hilo, Paulo aliwauliza hivi wasomaji wake Wakorintho: “Je, hamjui kwamba wakimbiaji katika mbio wote hukimbia, lakini ni mmoja tu apokeaye tuzo? Kimbieni kwa njia ambayo mwaweza kuipata tuzo. . . . Sasa wao, bila shaka hufanya hilo ili waweze kupata taji lenye kuharibika, lakini sisi lisiloharibika.” (1 Wakorintho 9:24, 25; 1 Petro 1:3, 4) Kuna tofauti iliyoje! Tofauti na mataji yenye kunyauka ya michezo ya kale, tuzo watakalopata wale wanaokimbia hadi mwisho katika shindano la mbio la kupata uhai halitaharibika kamwe.

Kwa habari ya taji hili bora, mtume Petro aliandika: “Mchungaji mkuu akiisha kuwa amefanywa dhahiri, mtapokea taji la utukufu lisiloweza kufifia.” (1 Petro 5:4) Je, kuna tuzo lolote ambalo ulimwengu huu hutoa ambalo laweza kulinganishwa na hali ya kutoweza kufa, tuzo la uhai usioweza kuharibika katika utukufu wa kimbingu pamoja na Kristo?

Leo, wakimbiaji wengi Wakristo hawakutiwa mafuta na Mungu kuwa wana wake wa kiroho na hawana tumaini la kimbingu. Hivyo, hawakimbii ili kupewa tuzo la uhai usioweza kufa. Hata hivyo, Mungu anawaahidi pia tuzo ambalo halina kifani. Tuzo hilo ni uhai udumuo milele wakiwa wakamilifu kwenye dunia paradiso chini ya Ufalme wa mbinguni. Hata mkimbiaji Mkristo awe anatarajia tuzo la aina gani, apaswa kukimbia kwa kuazimia na kwa nguvu kuliko mkimbiaji mwingine yeyote katika mashindano ya riadha. Kwa nini? Kwa sababu tuzo hilo halitanyauka kamwe: “Hili ndilo jambo lililoahidiwa ambalo yeye mwenyewe alituahidi, uhai udumuo milele.”—1 Yohana 2:25.

Kwa kuwa mkimbiaji Mkristo ameahidiwa tuzo hilo lisilo na kifani, anapaswa kuwa na maoni gani kuhusu vishawishi vya ulimwengu huu? Anapaswa kuwa na maoni kama yale ya Paulo, aliyesema hivi: “Kwa kweli naona vitu vyote kuwa hasara kwa sababu ya thamani iliyo bora zaidi ya ujuzi wa Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa sababu yake nimekubali hasara ya vitu vyote nami naviona kuwa takataka nyingi.” Kupatana na hilo, Paulo alikimbia kwa bidii kama nini! “Akina ndugu, bado mimi sijifikirii mwenyewe kuwa nimekwisha kulishika hilo; bali kuna jambo moja juu ya hilo: Nikisahau mambo ya nyuma na kujinyoosha mbele kwenye mambo ya mbele, ninafuatilia sana kuuelekea mradi kwa ajili ya tuzo.” (Wafilipi 3:8, 13, 14) Paulo alikimbia huku macho yake yakiwa yamekazwa kabisa kwenye tuzo. Nasi twapaswa kufanya hivyo.

Kielelezo Chetu Kilicho Bora Kabisa

Katika michezo ya zamani, mabingwa walivutia watu wengi. Washairi waliandika juu yao, nao wachongaji wakachonga sanamu zao. Mwanahistoria Věra Olivová asema kwamba “walitukuzwa na kupendwa na watu wengi sana.” Hata walikuwa violezo vya kuigwa na kizazi cha mabingwa wachanga.

Ni nani aliye “bingwa” ambaye anawawekea Wakristo kielelezo bora zaidi? Paulo anajibu: “Acheni tukimbie kwa uvumilivu shindano la mbio lililowekwa mbele yetu, tumkaziapo macho Wakili Mkuu na Mkamilishaji wa imani yetu, Yesu. Kwa ajili ya shangwe iliyowekwa mbele yake alivumilia mti wa mateso, akidharau aibu, na ameketi kwenye mkono wa kuume wa kiti cha ufalme cha Mungu.” (Waebrania 12:1, 2) Naam, ikiwa tutashinda katika shindano la mbio la kupata uhai udumuo milele, twahitaji kumkazia macho Yesu Kristo ambaye ni Kielelezo chetu. Tunaweza kufanya hivyo kwa kusoma masimulizi ya Gospeli kwa ukawaida na kutafakari njia ambazo tunaweza kumwiga. Funzo kama hilo litatusaidia kufahamu kwamba Yesu Kristo alimtii Mungu na kuthibitisha ubora wa imani yake kwa kuvumilia. Alipata kibali cha Yehova Mungu pamoja na mapendeleo mengi mazuri yakiwa tuzo kwa sababu ya uvumilivu wake.—Wafilipi 2:9-11.

Bila shaka, upendo wake ndio sifa iliyokuwa yenye kutokeza zaidi ya Yesu. “Hakuna aliye na upendo mkubwa zaidi kuliko huu, kwamba mtu fulani aisalimishe nafsi yake kwa niaba ya marafiki wake.” (Yohana 15:13) Alilipa neno “upendo” maana zaidi kwa kutuambia tuwapende hata adui zetu. (Mathayo 5:43-48) Kwa kuwa alimpenda Baba yake wa mbinguni, Yesu alipata shangwe kufanya mapenzi ya Baba yake. (Zaburi 40:9, 10; Mithali 27:11) Kwa kumtazama Yesu akiwa Kielelezo chetu na akiwa mwongozaji wetu wa mwendo katika shindano kali la mbio la kupata uhai kutatuchochea pia kumpenda Mungu na jirani yetu na kupata shangwe halisi katika utumishi wetu mtakatifu. (Mathayo 22:37-39; Yohana 13:34; 1 Petro 2:21) Kumbuka kwamba Yesu hatuambii tufanye yale tusiyoweza kufanya. Anatuhakikishia hivi: “Mimi ni mwenye tabia-pole na wa hali ya chini moyoni, nanyi mtapata burudisho kwa ajili ya nafsi zenu. Kwa maana nira yangu ni ya fadhili na mzigo wangu ni mwepesi.”—Mathayo 11:28-30.

Kama Yesu, twahitaji kukaza macho yetu kwenye tuzo ambalo limewekwa kwa ajili ya wote wanaovumilia hadi mwisho. (Mathayo 24:13) Tukishindana kulingana na kanuni, tukiondoa kila uzito na kukimbia kwa uvumilivu, tunaweza kuwa na uhakika wa kushinda. Mwisho wa mbio ambao umekaribia watuchochea kuendelea mbele! Hututia nguvu mpya kwa sababu ya shangwe ambayo mwisho huo hutupa, shangwe ambayo hufanya barabara iliyo mbele yetu ipitike kwa urahisi.

[Picha katika ukurasa wa 29]

Shindano la mbio la Kikristo ni la masafa marefu—lahitaji uvumilivu

[Picha katika ukurasa wa 30]

Tofauti na wanariadha waliovikwa taji, Wakristo wanaweza kutazamia kwa hamu tuzo lisiloweza kuharibika

[Picha katika ukurasa wa 31]

Wote wanaovumilia mpaka mwisho watapata tuzo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 28]

Copyright British Museum