Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Kwa kuzingatia amri za Biblia juu ya matumizi yafaayo ya damu, Mashahidi wa Yehova huonaje mbinu za tiba ambazo damu ya mtu mwenyewe hutumiwa?

Badala ya kufanya uamuzi kwa kutumia upendezi wa mtu binafsi tu au pendekezo fulani la kitiba, yampasa kila Mkristo afikirie kwa uzito vile Biblia isemavyo. Jambo hilo ni kati yake na Yehova.

Yehova, ambaye ndiye chanzo cha uhai wetu, alikataza ulaji wa damu. (Mwanzo 9:3, 4) Katika Sheria aliyowapa Waisraeli wa kale, Mungu alikataza matumizi ya damu kwa kuwa inawakilisha uhai. Aliamuru hivi: “Uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu.” Namna gani ikiwa mtu aliua mnyama kwa ajili ya chakula? Mungu alisema: “Atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga.” * (Mambo ya Walawi 17:11, 13) Yehova alirudia amri hiyo tena na tena. (Kumbukumbu la Torati 12:16, 24; 15:23) Kichapo cha Kiyahudi, Soncino Chumash, chasema: “Damu haipasi kuwekwa akiba lakini yapasa kumwagwa chini ili isifae kuliwa.” Hakuna Mwisraeli aliyepaswa kutwaa, kuweka akiba, na kutumia damu ya kiumbe mwingine, ambaye uhai wake ulitoka kwa Mungu.

Takwa la kushika Sheria ya Kimusa liliisha Mesiya alipokufa. Hata hivyo, maoni ya Mungu kuhusu utakatifu wa damu hayakubadilika. Mitume walichochewa na roho takatifu ya Mungu kuwaagiza Wakristo ‘wajiepushe na damu.’ Amri hiyo haikupasa kuchukuliwa vivi hivi. Kiadili, amri hiyo ilikuwa muhimu kama vile amri ya kujiepusha na ukosefu wa adili katika ngono au kuabudu sanamu. (Matendo 15:28, 29; 21:25) Wakati utoaji na utiaji damu mishipani ulipopata kuwa jambo la kawaida mnamo karne ya 20, Mashahidi wa Yehova walielewa kwamba kufanya hivyo kunapingana na Neno la Mungu. *

Mara kwa mara, daktari atamhimiza mgonjwa kuweka akiba ya damu yake mwenyewe majuma kadhaa kabla ya upasuaji ili ikihitajika, aweze kumtia mgonjwa huyo damu yake mwenyewe iliyowekwa akiba. Lakini kutoa damu hiyo, kuiweka akiba, na kuitia mishipani hupingana moja kwa moja na yale yasemwayo katika kitabu cha Mambo ya Walawi na Kumbukumbu la Torati. Damu haipasi kuwekwa akiba; yapasa kumwagwa—kana kwamba kuirudisha kwa Mungu. Ni kweli kwamba Sheria ya Kimusa haitumiki sasa. Hata hivyo, Mashahidi wa Yehova wanaheshimu kanuni za Mungu zilizo katika sheria hiyo, nao wameazimia ‘kujiepusha na damu.’ Kwa hiyo, hatutoi damu, wala hatuweki akiba damu yetu kwa ajili ya kutiwa mishipani kwa sababu yapasa ‘kumwagwa.’ Kutoa damu au kuiweka akiba hupingana na sheria ya Mungu.

Mbinu nyingine za tiba au upimaji zinazohusisha damu ya mtu mwenyewe hazipingani moja kwa moja na kanuni za Mungu. Kwa mfano, Wakristo wengi wameruhusu damu yao itolewe ili ipimwe au ichunguzwe, na baadaye damu hiyo inamwagwa. Mbinu nyingine tata zaidi zinazohusisha damu ya mtu mwenyewe zaweza pia kupendekezwa na daktari.

Kwa mfano, wakati wa upasuaji fulani, huenda kiasi fulani cha damu kikatolewa mwilini kwa kutumia mbinu iitwayo hemodilution. Damu ya mgonjwa inayobaki inatiwa umajimaji. Baadaye, damu yake iliyo katika mzunguko wa damu wa nje inarudishwa katika mwili wake, hivyo kufanya kiasi cha damu yake kiwe karibu sawa na kile cha kawaida. Vivyo hivyo, damu inayotiririka kwenye kidonda inaweza kuchukuliwa na kuchujwa ili chembe nyekundu ziweze kurudishwa katika mwili wa mgonjwa; mbinu hii inaitwa uokoaji wa chembe za damu. Katika mbinu nyingine, damu inaweza kuelekezwa katika mashine ambayo kwa muda inafanya kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na viungo vya mwili (kwa mfano, moyo, maini, au mafigo). Kisha damu hiyo iliyo katika mashine irudishwe katika mwili wa mgonjwa. Katika mbinu nyingine, damu inaelekezwa katika chombo cha kuitenganisha (mashinepewa) ili sehemu zake zilizoharibika au zenye kasoro ziondolewe. Au lengo laweza kuwa kutenga sehemu fulani ya damu na kuitumia katika sehemu nyingine ya mwili. Pia kuna upimaji mwingine ambao kiasi fulani cha damu hutolewa ili kujua aina yake au kuichanganya na dawa, halafu inarudishwa katika mwili wa mgonjwa.

Mbinu hizo zaweza kuwa tofauti, na bila shaka mbinu, matibabu, na upimaji mpya wa damu zitatokezwa. Si jukumu letu kuchanganua kila mbinu tofauti na kutoa uamuzi. Mkristo apaswa kuamua mwenyewe kuhusu jinsi damu yake mwenyewe itakavyotumiwa wakati wa upasuaji, upimaji damu, au tiba inayotumika wakati huo. Anapaswa kujua mapema kutoka kwa daktari au mtaalamu wa kitiba mambo ambayo huenda yakafanyiwa damu yake wanapotumia mbinu hiyo. Kisha lazima aamue kulingana na dhamiri yake. (Ona sanduku.)

Inawapasa Wakristo wakumbuke wakfu wao kwa Mungu na wajibu ‘wa kumpenda kwa moyo wao wote na kwa nafsi yao yote na kwa nguvu zao zote na kwa akili yao yote.’ (Luka 10:27) Mashahidi wa Yehova huthamini sana uhusiano wao na Mungu tofauti na watu walio wengi duniani. Mpaji-Uhai anawahimiza wote watumaini damu ya Yesu iliyomwagwa. Twasoma hivi: “Kwa njia yake [Yesu Kristo] tuna kuachiliwa kwa njia ya fidia kupitia damu ya huyo, ndiyo, msamaha wa makosa yetu.”—Waefeso 1:7.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Profesa Frank H. Gorman aandika: “Kumwaga damu kunaeleweka vizuri kuwa kitendo cha staha kinachodhihirisha heshima kwa uhai wa mnyama, na hivyo heshima kwa Mungu, aliyeumba na anayeendelea kuutunza uhai huo.”

^ fu. 5 Gazeti la Mnara wa Mlinzi la Julai 1, 1951 (la Kiingereza), lilijibu maswali muhimu kuhusu habari hii, likionyesha ni kwa nini haifai kutia mishipani damu iliyotolewa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 31]

MASWALI UNAYOPASWA KUJIULIZA

Ikiwa sehemu ya damu yangu itaelekezwa sehemu nyingine nje ya mwili wangu na mtiririko wake ukatishwe kwa muda, je, dhamiri yangu itaniruhusu kuona damu hiyo kuwa sehemu ya mwili wangu bado, hivyo nisihitaji ‘kuimwaga chini’?

Je, dhamiri yangu iliyozoezwa kwa Biblia itanisumbua ikiwa wakati wa kupima ugonjwa au wa matibabu sehemu ya damu yangu itatolewa, iongezwe vitu vingine, na kurudishwa mwilini mwangu?