Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutangaza Ufalme wa Mungu Katika Visiwa vya Fiji

Kutangaza Ufalme wa Mungu Katika Visiwa vya Fiji

Sisi Ni Namna ya Watu Walio na Imani

Kutangaza Ufalme wa Mungu Katika Visiwa vya Fiji

WAKATI mmoja Yesu Kristo alisema juu ya barabara mbili. Moja ni pana nayo huongoza kwenye kifo. Ile nyingine ni nyembamba lakini huongoza kwenye uhai. (Mathayo 7:13, 14) Ili kuwezesha watu kuchagua barabara inayofaa, Yehova Mungu alikusudia habari njema za Ufalme zihubiriwe ulimwenguni pote. (Mathayo 24:14) Kwa hiyo, watu kila mahali wanasikiliza ujumbe wa Ufalme, na baadhi yao wanachagua uhai kwa kuamua kuwa watu wa “namna iliyo na imani kuelekea kuhifadhi hai nafsi.” (Waebrania 10:39) Twakualika usome jinsi ambavyo baadhi ya watu wa Fiji na visiwa vinginevyo vya Pasifiki Kusini wamechagua uhai.

Walimtumaini Yehova

Mere alikuwa bado shuleni aliposikia ujumbe wa Ufalme kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1964. Kwa sababu ya kukaa katika kisiwa cha mbali, hakuweza kuwasiliana na Mashahidi wa Yehova. Hata hivyo, hatimaye, aliweza kupata ujuzi sahihi wa Biblia. Wakati huo alikuwa ameolewa na mwanamume aliyekuwa chifu katika kijiji chake. Kwa sababu Mere alichagua kuishi kwa kupatana na kanuni za Biblia, mume wake na watu wa jamaa yake walimtesa, nao watu wa kijiji wakamdharau. Hata hivyo, alibatizwa mwaka wa 1991.

Punde baadaye, mtazamo wa mume wa Mere, aitwaye Josua, ulibadilika na hata akaanza kushiriki katika mazungumzo ya Biblia pamoja na Mere na watoto wao. Josua aliacha kwenda Kanisa la Methodisti. Hata hivyo, kwa maana alikuwa chifu, bado aliongoza mikutano ya kila juma ya kijiji. Machoni pa watu wa kijiji, Josua hakuwa mwaminifu, kwa kuwa kushiriki Kanisa la Methodisti kulikuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu wa vijiji vya Fiji. Kwa hiyo, kasisi wa hapo akamhimiza Josua arudi katika dini yake ya awali.

Kwa ujasiri Josua alikiri kwamba yeye na jamaa yake walikuwa wamefanya uchaguzi wao na wameazimia kumwabudu Yehova Mungu “kwa roho na kweli.” (Yohana 4:24) Katika mkutano mmoja wa kijiji uliofuata, chifu mkuu aliagiza kwamba Josua na jamaa yake watengwe na kijiji na kuondoka. Walipewa siku saba za kuondoka kisiwani, na kuacha nyumba,shambanamazao—naam, riziki yao yote.

Ndugu wa kiroho katika kisiwa kingine walimsaidia Josua na jamaa yake, wakawaandalia mahali pa kukaa na shamba la kulima. Kwa sasa, Josua na mwanake mkubwa wamebatizwa, na mwana mwingine ni mhubiri asiyebatizwa wa habari njema. Hivi majuzi, Mere alianza kutumikia akiwa painia wa kawaida (mhubiri wa Ufalme wa wakati wote). Kwa sababu walichagua kumtumikia Yehova walipoteza cheo na mali, lakini kama vile mtume Paulo, wanaviona vitu hivyo kuwa visivyo na thamani vikilinganishwa na manufaa ambayo wamepata.—Wafilipi 3:8.

Uchaguzi Unaohusisha Dhamiri

Kuchagua kufuata dhamiri iliyozoezwa na Biblia kwataka imani na ujasiri. Kwa hakika, Suraang alihitaji imani na ujasiri. Alikuwa amebatizwa karibuni, naye aliishi Tarawa, mojawapo ya visiwa vya Kiribati. Suraang aliomba aruhusiwe asifanye sehemu moja ya kazi yake ya uuguzi hospitalini. Maombi yake hayakukubaliwa na alipelekwa kufanya kazi katika kituo kidogo cha kitiba katika kisiwa kidogo cha mbali, mahali ambapo hapakuwapo watu wengine wa dini yake.

Katika kisiwa hicho ni desturi kwamba wapya wanaowasili watolee “roho” ya hapo sadaka. Watu wanaamini kwamba kutokufanya hivyo kutasababisha kifo. Kwa sababu Suraang alikataza tendo hilo la ibada ya sanamu lisifanywe kwa niaba yake na wenzake, watu wa kijiji walitarajia anyongwe na roho huyo aliyeudhika. Watu walipoona kwamba Suraang na wenzake hawakupatwa na madhara yoyote, Suraang alipata fursa nyingi za kutoa ushuhuda.

Lakini majaribu ya Suraang hayakuwa yameisha. Baadhi ya vijana wa kisiwa hicho hupenda kutongoza wanawake wachanga wanaotembelea kisiwa hicho. Hata hivyo, Suraang alikataa kabisa utongozaji wao, akashika uaminifu wake kwa Mungu. Ijapokuwa angeweza kuitwa kazini wakati wowote, iwe mchana au usiku, aliweza kutumikia kama painia wa kawaida.

Kabla ya karamu iliyofanywa kwa heshima ya Suraang alipokuwa anajitayarisha kuhama kisiwa hicho, wazee wa kijiji walisema kwamba Suraang alikuwa mishonari wa kwanza wa kweli kuwatembelea. Kwa sababu ya msimamo wake imara kwa kanuni za Biblia, baadhi ya watu katika kisiwa hicho wamevutiwa na ujumbe wa Ufalme.

Magumu ya Kimwili

Kwa sababu vijiji kadhaa viko mbali na mikutano ya Kikristo, ni lazima watu wa Yehova wajitahidi kabisa ili kuihudhuria na kushiriki katika utumishi. Ebu fikiria Mashahidi wanne waliobatizwa, mwanamume mmoja na wanawake watatu, wanaosafiri kwa muda wa saa kadhaa ili kufika mikutanoni na kurudi. Safari yao ya miguu yatia ndani kuvuka mito mitatu, wanapokwenda na vilevile wanaporudi. Wakati mito imefurika, ndugu huvuka kwanza kwa kuogelea, huku akivuta nyungu kubwa yenye mikoba, vitabu, na mavazi yao ya mikutano. Halafu hurudi kwa kuogelea ili kuwasaidia dada hao watatu.

Kikundi kingine kidogo cha watu wanaohudhuria mikutano katika kisiwa cha mbali cha Kiribati kiitwacho Nonouti, wana magumu tofauti. Nyumba ambamo wanakutania ina nafasi ya watu saba au wanane tu. Wengine wanaohudhuria huketi nje na kuchungulia ndani kupitia kuta za wavu wa chuma wa nyumba hiyo. Watu wa kijiji wanaweza kuona yote yanayoendelea wanapopita wakienda na kurudi kutoka katika makanisa yao yenye fahari. Bila shaka, watumishi wa Yehova wanatambua kwamba watu, wala si majengo, ndio wanaotamaniwa machoni pa Mungu. (Hagai 2:7) Shahidi pekee aliyebatizwa kisiwani humo ni dada mzee na hawezi kutembea mbali kwa miguu. Hata hivyo, anasaidiwa katika huduma na mwanamke mchanga, mhubiri asiyebatizwa, ambaye humsukuma katika mkokoteni. Wanaithamini kweli kama nini!

Wahubiri zaidi ya 2,100 wanaotumikia katika Fiji na Kiribati wameazimia kuendelea kutangaza habari njema za Ufalme wa Mungu. Nao wana uhakika wa kwamba wengi zaidi watapata kuwa watu wa “namna iliyo na imani kuelekea kuhifadhi hai nafsi.”

[Ramani katika ukurasa wa 8]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Australia

Fiji