Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nini Ufunguo wa Kupata Mafanikio?

Ni Nini Ufunguo wa Kupata Mafanikio?

Ni Nini Ufunguo wa Kupata Mafanikio?

VIJANA wanaume wawili jasiri walikuwa wakitengeneza kwa utaratibu chombo fulani cha ajabu-ajabu ili kufanya jaribio muhimu. Kwa ghafula, upepo mkali ukakirusha chombo hicho dhaifu angani na kukiangusha chini kwa kishindo kikubwa. Wakiwa wamevunjika moyo, wanaume hao walisimama kimya. Kazi yao ngumu, iliyofanywa kwa makini sana, ilikuwa mbele yao ikiwa rundo tu la mbao na vyuma vilivyovunjika-vunjika na kujikunja.

Kwa Orville na Wilbur Wright, jambo lililotukia siku hiyo ya Oktoba mwaka wa 1900 halikuwa ndilo kipingamizi cha kwanza chenye kuvunja moyo katika jaribio lao la kutengeneza chombo chenye kuruka angani ambacho ni kizito kuliko hewa. Walikuwa tayari wametumia muda wa miaka kadhaa na kiasi kikubwa cha fedha katika majaribio yao.

Hata hivyo, udumifu wao ulikuwa na matokeo mazuri baadaye. Mnamo Desemba 17, 1903, wakiwa Kitty Hawk, North Carolina, Marekani, akina Wright walifanikiwa kurusha chombo kingine sampuli ya kile cha kwanza ambacho kilibaki hewani kwa sekunde 12—muda mfupi ukilinganishwa na mwendo wa ndege siku hizi, lakini mrefu vya kutosha kubadili ulimwengu milele!

Mafanikio katika mambo mengi hutegemea sanasana udumifu wenye subira. Iwe ni kujifunza lugha mpya, kujifunza kazi fulani, au hata kusitawisha uhusiano, mambo mengi yenye thamani hufanikiwa kupitia jitihada yenye kudumu. “Mara tisa kwa kumi,” asema mwandishi Charles Templeton, “mafanikio huwa ni matokeo ya moja kwa moja ya kitu kimoja: jitihada.” Mwandishi wa habari za magazeti, Leonard Pitts, Jr., asema: “Sisi huzungumza juu ya kipawa, hukubali kuna bahati, lakini mara nyingi, sisi hupuuza mambo muhimu zaidi. Jitihada zilizofanywa na kule kushindwa mara nyingi kupata mafanikio. Sisi hupuuza pia muda wa saa nyingi zinazotumiwa ili kufanikiwa.”

Jambo hilo lathibitisha kile Biblia ilichosema muda mrefu uliopita: “Mkono wa mwenye bidii utatawala.” (Mithali 12:24) Bidii humaanisha kwamba tudumu katika jitihada zetu. Jambo hilo ni muhimu tukitaka kufanikiwa katika yale tunayokusudia kufanya. Udumifu ni nini? Tunaweza kudumuje katika jitihada za kutimiza miradi yetu, nasi tudumu katika mambo gani? Maswali hayo yatajibiwa katika makala inayofuata.

[Picha katika ukurasa wa 3]

U.S. National Archives photo