Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mifereji—Maajabu ya Uhandisi wa Waroma

Mifereji—Maajabu ya Uhandisi wa Waroma

MIFEREJI ya Waroma ni mojawapo ya kazi za kale za uhandisi zenye kustaajabisha sana. Sextus Julius Frontinus, aliyeishi kati ya mwaka wa 35 hadi karibu mwaka wa 103 W.K., ambaye alikuwa gavana na pia msimamizi mkuu wa miradi ya maji jijini Roma, aliandika hivi: “Mifereji hii iliyotengenezwa kwa ustadi mkubwa na inayosafirisha maji mengi, haiwezi kulinganishwa na Mapiramidi au miradi maarufu, lakini isiyo na maana yoyote iliyofanywa na Wagiriki!” *

Kwa Nini Walihitaji Mifereji?

Kwa kawaida majiji ya kale yalijengwa karibu na vyanzo vya maji mengi, na jiji la Roma pia lilijengwa karibu na vyanzo kadhaa vya maji. Mwanzoni, maji ya kutosha yalipatikana kwenye Mto Tiber na pia kwenye chemchemi za maji na visima vilivyokuwa karibu. Hata hivyo, kuanzia karne ya nne K.W.K. na kuendelea jiji la Roma lilikua haraka na hivyo kukawa na uhitaji mkubwa wa maji.

Kwa kuwa ni watu wachache tu waliokuwa na maji katika nyumba zao, Waroma walijenga mamia ya mabafu ya kibinafsi na ya umma. Bafu la kwanza la umma jijini Roma lilipata maji yake kutoka kwenye mfereji ulioitwa Aqua Virgo, ambao ulizinduliwa mwaka wa 19 K.W.K. Mjenzi wa mfereji huo, Marcus Agrippa, aliyekuwa rafiki wa Kaisari Augusto, alitoa mali zake nyingi ili kukarabati na kupanua mifumo ya maji ya Roma.

Mabafu pia yalitumika kama kumbi ambako watu walikutana, na mabafu makubwa yalikuwa na bustani na maktaba. Siku zote maji yalipotoka kwenye mabafu, yaliingia kwenye mfumo wa maji-taka ili kuondoa uchafu, kutia ndani uchafu uliokuwa kwenye vyoo vilivyounganishwa na mabafu hayo.

Ujenzi na Ukarabati

Unaposikia maneno “Mifereji ya Waroma,” je, unafikiria ukubwa na urefu wa mifereji hiyo? Isitoshe, sehemu zilizojipinda za mifereji hiyo zilizoonekana zilikuwa chini ya asilimia 20, sehemu kubwa ilikuwa chini ya ardhi. Jinsi ilivyojengwa ilisaidia isiathiriwe na mmomonyoko wa udongo, na pia ilisaidia kupunguza madhara kwenye mashamba na makazi ya watu. Kwa mfano, mfereji wa Aqua Marcia uliokamilika mwaka 140 K.W.K., ulikuwa  na urefu wa karibu kilomita 92 ilhali sehemu zilizojipinda zilikuwa na urefu wa kilomita 11 tu.

Kabla ya kujenga mfereji wowote ule, wahandisi walipima ubora wa chanzo cha maji kwa kuchunguza usafi, mtiririko, na ladha ya maji. Pia walichunguza afya za wakazi waliokunywa maji kutoka kwenye chanzo hicho. Baada ya kumaliza ukaguzi wao, wataalamu wa vipimo walipima njia na miinuko ambapo mfereji huo ungepitia kutia ndani ukubwa na urefu wa mfereji. Watumwa ndio waliotumiwa kujenga mifereji. Nyakati nyingine ujenzi huo ulichukua miaka mingi kukamilika, jambo lililosababisha gharama kubwa, hasa ikiwa mifereji hiyo ilitia ndani sehemu zilizojipinda.

Zaidi ya hayo, mifereji ilihitaji kukarabatiwa na kulindwa. Wakati fulani jiji la Roma liliajiri karibu watu 700 ili kuitunza. Mifereji ilitengenezwa kwa njia ambayo ingeweza kukarabatiwa kwa urahisi. Kwa mfano, mtu angeweza kupita kwenye mashimo fulani ili afikie sehemu za mifereji zilizokuwa chini ya ardhi. Ikiwa sehemu fulani ya mfereji ilihitaji marekebisho makubwa, wahandisi walitengeneza mkondo mwingine wa maji wa muda mfupi ili watengeneze sehemu iliyoharibika.

Mifereji Mjini Roma

Kufikia mwanzoni mwa karne ya tatu W.K., kulikuwa na mifereji mikubwa 11 iliyopeleka maji jijini Roma. Mfereji wa kwanza ulioitwa Aqua Appia, ulijengwa mwaka wa 312 K.W.K., na ulikuwa na urefu wa zaidi ya kilomita 16, huku sehemu yake kubwa ikipitia chini ya ardhi. Leo bado kuna sehemu fulani za mfereji ulioitwa Aqua Claudia. Mfereji huo ulikuwa na urefu wa karibu kilomita 69 na sehemu zilizojipinda zenye jumla ya urefu wa kilomita 10, huku baadhi ya sehemu zake zilizojipinda zikiwa na kimo cha mita 27!

Mifereji iliyopitia jijini ilibeba maji kiasi gani? Mengi sana! Mfereji wa Aqua Marcia uliotajwa katika makala hii ulileta karibu lita milioni 190 za maji jijini Roma kila siku. Kwa sababu ya nguvu za uvutano maji yalifika maeneo ya mjini yakasukumwa kwa nguvu kuelekea kwenye matangi makubwa na kisha kuingizwa kwenye matangi mengine ambayo yalisambaza maji kwa watumiaji. Wengine wanakadiria kwamba mfumo wa kusambaza maji wa Milki ya Roma uliboreshwa hivi kwamba ungeweza kusambaza zaidi ya lita 1,000 za maji kwa kila mkaaji kila siku.

Kitabu Roman Aqueducts & Water Supply kinasema kwamba kadiri milki ya Roma ilivyozidi kupanuka ndivyo “mifereji yake ilivyofika kotekote katika milki hiyo.” Wageni wanaotembelea Asia Ndogo, Ufaransa, Hispania, na Afrika Kaskazini hustaajabishwa na maajabu hayo ya kale ya uhandisi.

^ fu. 2 Waroma hawakuwa wa kwanza kujenga mifereji ya maji. Walitanguliwa na mataifa mengine kama vile, Ashuru, Misri, India, na Uajemi.