Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ustadi wa Kusafiri wa Mbawakawa

Ustadi wa Kusafiri wa Mbawakawa

MBAWAKAWA hutumia kinyesi kwa makusudi mbalimbali. Mdudu huyo hutumia kinyesi kama chakula na mahali pa kutagia mayai. Wadudu fulani wa kiume huwapa wadudu wa kike kipande kikubwa ili kuwavutia. Wadudu hao hupigania kinyesi ambacho hakijakauka. Watafiti walishuhudia mbawakawa 16,000 wakivamia rundo kubwa la kinyesi cha ndovu na kukimaliza kwa muda wa saa mbili tu.

Aina fulani ya mbawakawa huviringisha kipande cha kinyesi kama mpira, halafu wanaondoka nacho na kukizika kwenye udongo laini. Mbawakawa huviringisha mpira huo kwa kufuata mstari ulionyooka, ili waondoke haraka na kuepuka kunyang’anywa na mbawakawa wengine.

Hata hivyo, mbawakawa huepukaje kuzunguka mahali palepale, hasa usiku?

Fikiria hili: Mwanzoni utafiti ulionyesha kwamba mbawakawa wanasafiri kwa kutegemea mwangaza wa jua au mwezi, hata hivyo, wanaweza kusafiri kwenye mstari ulionyooka usiku usio na mwangaza wa mwezi. Watafiti nchini Afrika Kusini waligundua kwamba mbawakawa husafiri si kwa kutazama nyota, bali kwa kutumia mwangaza unaotoka kwenye kikundi cha nyota cha Kilimia. Kulingana na gazeti Current Biology, huo ndio “uchunguzi wa kwanza unaoonyesha viumbe wanaotegemea kundi la nyota la Kilimia katika kusafiri.”

Mtafiti Marcus Byrne , anasema kwamba mbawakawa wana “mfumo bora unaowawezesha kuona usiku usio na mwangaza wa nyota, bila kutumia akili nyingi.” Anaendelea kusema: “Hivyo basi, wanaweza kuwafundisha wanadamu kutazama na kuchanganua habari ngumu kueleweka.” Kwa mfano, roboti inaweza kuwekewa programu ili ipekue vifusi vya jengo lililoporomoka kwa kuiga mfumo wa kusafiri wa mbawakawa.

Una maoni gani? Je, uwezo wa kusafiri wa mbawakawa ulijitokeza wenyewe? Au je, ni kazi ya ubuni?

Je, wajua?

Mbawakawa hulegeza na kuongeza rutuba kwenye udongo, husambaza mbegu za mimea, na kudhibiti idadi ya nzi.