Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Uwezo wa DNA wa Kuhifadhi Habari

Uwezo wa DNA wa Kuhifadhi Habari

WATUMIAJI wa kompyuta huwa na habari nyingi zinazohitaji kuhifadhiwa ili zitumiwe wakati wowote zitakapohitajiwa. Wanasayansi wanatumaini kwamba watafaulu kuboresha mbinu za sasa za kuhifadhi habari kwa kuiga mfumo bora zaidi wa kuhifadhi habari wa DNA.

Fikiria hili: DNA inayopatikana katika chembe, ina habari nyingi sana kuhusu urithi. “Tunaweza kupata [DNA] kutoka kwenye mifupa ya tembo wenye manyoya walioishi zamani . . . na tufaulu kuifanyia uchunguzi,” anasema Nick Goldman wa Taasisi ya Ulaya ya Bioinformatics. “Pia ni ndogo, ina uwezo wa kuhifadhi habari nyingi, na haihitaji umeme ili mtu afaulu kuhifadhi habari ndani yake, kwa hiyo ni rahisi kuisafirisha na kuiweka.” Je, DNA inaweza kuhifadhi habari zilizotayarishwa na wanadamu? Watafiti wanasema inaweza.

Wanasayansi wamebuni mbinu ya kuhifadhi maandishi, picha, na rekodi za sauti katika DNA, kwa njia ileile kama vifaa vingine vya kielektroniki vinavyofanya. Baadaye, watafiti hao walifaulu kupata tena habari yote hiyo waliyokuwa wamehifadhi. Wanasayansi wanaamini kwamba baada ya muda, gramu moja ya DNA iliyotengenezwa na wanadamu itaweza kuhifadhi habari zinazoweza kutoshea katika CD 3,000,000 na habari hizo zinaweza kuhifadhiwa kwa maelfu ya miaka. Inakadiriwa kwamba mfumo huo utafaulu kuhifadhi habari zote za kielektroniki ulimwenguni. Kwa sababu hiyo, DNA imesemekana kuwa “kifaa bora zaidi cha kuhifadhi habari.”

Una maoni gani? Je, uwezo wa DNA wa kuhifadhi habari ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?