Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Zheng He

Zheng He

“Tumesafiri zaidi ya li * elfu mia moja kupitia bahari kubwa sana na tumeona mawimbi makubwa ya bahari yakiinuka juu sana kama milima, na tumejionea maeneo ya mbali ya watu wasio na ustaarabu . . . huku matanga yetu yaliyo kama mawingu yakitusukuma usiku na mchana kama nyota inayofuata mkondo wake, tukipita juu ya mawimbi hayo makubwa kana kwamba tunakanyaga barabara kuu.”—Maandishi ya karne ya kumi na tano yanayosemekana yaliandikwa na Zheng He katika jiji la Changle, mkoa wa Fujian, nchini China.

CHINA ni nchi ya mambo makubwa. Ndiyo nchi yenye watu wengi zaidi na ni moja kati ya nchi zenye ardhi kubwa zaidi duniani. Wachina ndio waliojenga ule Ukuta Mkubwa, ambao ni mojawapo ya miradi mikubwa zaidi ya ujenzi katika historia. Meli zilizojengwa na Maliki Yongle na Xuande wa China wa milki ya Ming, zilikuwa nyingi kuliko zile ambazo nchi yoyote ingeweza kuunda kwa karne tano zilizofuata. Ofisa mkuu wa meli hizo alikuwa Mwislamu kutoka kusini-magharibi mwa China anayeitwa Zheng He.

MAMLAKA, BIASHARA, NA HESHIMA

Kulingana na maandishi yaliyoonyeshwa kwa sehemu mwanzoni mwa makala hii, utume wa Zheng He ulikuwa “kuonyesha mamlaka ya (maliki) ya kubadili mambo na kuwatendea watu wa maeneo ya mbali kwa fadhili.” Kutokana na safari hizo, maandishi hayo yanasema, “nchi zilizo mbali na watu kutoka miisho ya dunia wamekuwa wote raia [wa China] . . . watu wasio na ustaarabu upande ule mwingine wa bahari . . . wamekuja kwenye [ua wa maliki] wakiwa na vitu na zawadi zenye thamani.”

Baadhi ya bandari ambazo meli za Zheng He zilipitia

Kusudi la maliki wa milki ya Ming la kufunga safari hizo limejadiliwa kwa muda mrefu. Wengine humwona Zheng  He kuwa balozi wa utamaduni na amani kwa ajili ya taifa lenye nguvu na lenye amani. Wengine huona safari zake kuwa za kueneza ukoloni dhidi ya mataifa mengine. Kwa kweli, Zheng He aliwapa watawala waliomkaribisha zawadi nzuri na utegemezo wa kisiasa, lakini wale waliokataa kujitiisha kwa maliki wa China, aliwatiisha na kuwafanya kuwa wafungwa. Kwa sababu ya safari za Zheng He, watawala wengi sana katika maeneo ya Bahari ya Hindi walituma mabalozi nchini China ili kumpa maliki heshima ya pekee.

Vyovyote vile, meli za Zheng He zilibeba pia vyombo vya mbao vyenye mapambo na vilivyopakwa vanishi, vyombo vya kauri, na hariri. Vitu hivyo vilitengenezwa na mafundi Wachina ili vikauzwe katika bandari za mbali. Meli hizo zilirudi zikiwa na vito, pembe za tembo, vikolezo, mbao za maeneo yenye joto, na vitu vingine vyenye thamani vilivyopendwa na Wachina. Pia, zilibeba twiga, ambaye alitokeza msisimuko mkubwa sana nchini China. Kupitia kubadilishana huko kwa bidhaa na mawazo, ulimwengu ulipata kuona sehemu ndogo ya ustaarabu wa China wa karne ya 15.

Safari hizo kubwa hazikuendelea. Miaka kadhaa tu baada ya safari za Zheng He, China iliacha kabisa kujihusisha katika biashara na uhusiano wowote na nchi nyingine. Akihisi kwamba hakuna uhitaji wa kuwa na uhusiano wowote na nchi nyingine, maliki mpya pamoja na washauri wake Wakonfyushasi walijaribu kuzuia China isiathiriwe na uvutano kutoka nje. Waliamua meli hizo zilizobeba hazina zifutwe katika historia, na wakaharibu rekodi zozote kuhusiana na safari zake kubwa pamoja na meli zenyewe. Ni katika miaka ya karibuni tu ndipo watu, nchini China na pia nje, wamegundua kuhusu kipindi hicho muhimu ambapo meli nyingi sana za Zheng He zilifunga safari zake.

^ fu. 3 Neno li ni kipimo cha Kichina ambacho kwa karne mbalimbali kimerejelea urefu tofauti-tofauti. Inaaminiwa kwamba wakati wa Zheng He, li moja ilirejelea umbali wa nusu kilomita hivi.