Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Aktiki

“Kiwango cha barafu wakati wa kiangazi ni robo tu ya kiwango kilichokuwapo miaka 30 iliyopita,” anasema Peter Wadhams, profesa wa fizikia ya bahari katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Katika mwaka wa 2012, meli zipatazo 50 zilipitia kwenye Njia ya Bahari ya Kaskazini ambayo imefunguka kwa sababu ya kuongezeka kwa joto duniani ambako kumesababisha kuyeyuka kwa barafu.

Dunia

Imegunduliwa kwamba maziwa ya mama yanayotokezwa siku kadhaa kuanzia siku ambayo mtoto anazaliwa yana aina zaidi ya 700 za bakteria—na hizo ni bakteria nyingi kuliko wataalamu walivyotazamia. Bado watafiti wanachunguza ili kujua bakteria hizo zina faida gani katika mfumo wa umeng’enyaji na wa kinga wa mtoto.

Uingereza

Utafiti uliofanywa na wanasayansi Waingereza kuhusiana na kuendesha gari, unaonyesha kwamba madereva walio na mafua hufanya maamuzi polepole zaidi kuliko madereva walevi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Afrika inakabiliwa na kile ambacho wengine wanakiita uchinjaji “mkubwa sana” wa makumi ya maelfu ya tembo kila mwaka kwa ajili ya pembe zao. Katika kisa kimoja, tembo kadhaa walipigwa risasi kichwani, na inaelekea kwamba wapigaji-risasi walikuwa kwenye helikopta.

Australia

Katika muda wa miaka 27 iliyopita, Tumbawe Kubwa la Australia limepoteza nusu ya marijani yake. Wanasayansi wanasema kwamba jambo hilo linasababishwa kwa kiasi kikubwa na tufani za kitropiki, kuvamiwa na kiti cha pweza anayeitwa crown-of-thorns, na kupoteza rangi kwa matumbawe kunakosababishwa na kuongezeka kwa joto baharini.