Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ubongo wa Kindi wa Aktiki Unaoweza Kustahimili Baridi Kali

Ubongo wa Kindi wa Aktiki Unaoweza Kustahimili Baridi Kali

MNYAMA anapoanza kulala wakati wa majira ya baridi kali, joto mwilini mwake huanza kupungua. Linaweza kupungua kwa kiasi gani? Kiwango joto cha chini zaidi ambacho kimewahi kufikiwa na kindi wa aktiki ni nyuzi 2.9 Selsiasi chini ya sufuri! Tungetazamia kwamba kiwango hicho cha joto cha chini sana kingefanya ubongo wake ugande. Basi, ni nini kinachomwezesha kindi wa aktiki kuendelea kuishi?

Fikiria hili: Kila baada ya majuma mawili au matatu anapolala, kindi huyo wa aktiki hutikisa mwili wake hadi kiwango cha joto mwilini kinaporudia hali ya kawaida ya nyuzi 36.4 Selsiasi na joto hilo hudumu kwa muda wa saa 12 hadi 15 hivi. Watafiti wanasema kwamba ingawa kipindi hicho cha kujipasha joto ni kifupi, kinasaidia sana ubongo wake uendelee kufanya kazi. Isitoshe, kindi huyo anapolala inaonekana kwamba kichwa chake huendelea kuwa na joto kuliko sehemu nyingine zote za mwili wake. Wakati wa utafiti uliofanywa kwenye maabara, kiwango cha joto kwenye shingo yake hakikupungua chini ya nyuzi 0.7 Selsiasi.

Kindi huyo anapoamka kutoka kwenye usingizi huo wa muda mrefu, ubongo wake hurudia utendaji wa kawaida katika muda wa saa mbili hivi. Kwa kweli, uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba ubongo wa kindi huyo hufanya kazi vizuri zaidi baada ya kipindi hicho cha kulala! Watafiti walistaajabishwa sana na ugunduzi huo wenye kushangaza. Wanaulinganisha na jinsi mimea huchanua upya kutoka ardhini baada ya moto wa msitu.

Watafiti wanatumaini kwamba uchunguzi wao kumhusu kindi huyo wa aktiki utawasaidia kuelewa vizuri zaidi uwezo wa ubongo wa mwanadamu. Lengo lao ni kujifunza mengi zaidi kuhusu jinsi wanavyoweza kuzuia au hata kurekebisha chembe zilizoharibika kwa sababu ya magonjwa ya ubongo, kutia ndani ugonjwa wa Alzheimer.

Una maoni gani? Je, ubongo wa kindi wa aktiki unaoweza kustahimili baridi kali ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?