Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 NCHI NA WATU

Kutembelea Azerbaijan

Kutembelea Azerbaijan

AZERBAIJAN ndiyo nchi kubwa zaidi kati ya nchi tatu zilizo kusini mwa safu ya milima ya Caucasus. Miaka elfu moja hivi iliyopita, makabila mengi yanayozungumza Kituruki yalianza kuishi katika eneo hilo. Wahamiaji hao walifuata baadhi ya desturi za wenyeji, nao wenyeji wakafuata baadhi ya tamaduni za wahamiaji hao. Kwa hiyo, si ajabu kwamba Kiazerbaijani kinafanana sana na Kituruki na lugha ya Turkmen.

Waazerbaijani wanajulikana kuwa watu wachangamfu na wenye shauku. Familia zina uhusiano wa karibu sana, na watu wa ukoo hutegemezana wakati wa matatizo.

Waazerbaijani wanapenda muziki na mashairi. Katika aina moja ya muziki inayoitwa mugam, mwimbaji anakariri mashairi ya Kiazerbaijani akiambatana na muziki uliopigwa kwa ala za kitamaduni. Mwimbaji wa mugam anapaswa kufahamu vizuri mashairi yote ya Kiazerbaijani na anapaswa kuwa na uwezo wa kutunga wimbo akiwa papo hapo jukwaani.

Chai ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Waazerbaijani

 Chai ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Waazerbaijani. Chai iliyotiwa kipande cha sukari hunywewa kwenye gilasi zenye umbo la pea, labda ikiambatana na njugu aina ya pistachio, lozi, na zabibu kavu. Mikahawa inayouza chai inaweza kupatikana hata katika miji midogo sana.

Samaki mkubwa anayeitwa sturgeon hupatikana katika Bahari ya Kaspiani iliyo upande wa mashariki wa nchi. Beluga sturgeon anaweza kuishi zaidi ya miaka 100. Mmoja kati ya sturgeon wakubwa zaidi ambao wamewahi kuvuliwa alikuwa na urefu wa mita 8.5 na uzito wa kilogramu 1,297! Samaki hao wanapendwa sana kwa sababu ya mayai yao meusi ambayo ni chakula maarufu na ghali sana.

Waazerbaijani ni watu wa kidini ambao hupenda kuzungumza kumhusu Mungu. Wengi wao ni Waislamu. Kuna dini nyingine pia, kutia ndani Mashahidi wa Yehova zaidi ya elfu moja—wengi wao ni Waazerbaijani wa asili.

Wanamuziki wa kitamaduni wa Azerbaijan

JE, WAJUA?

Mashahidi wa Yehova wanajifunza Biblia na mamilioni ya watu duniani kote, wakitumia kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? Kinapatikana katika lugha zaidi ya 250, kutia ndani Kiazerbaijani.