Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wataalamu wa Umekanika wa Enzi za Kati

Wataalamu wa Umekanika wa Enzi za Kati

MASHINE zinafanya utendaji wote katika viwanda​—hasa utendaji unaofanywa kwa ukawaida na kwa kurudia-rudia. Lakini mashine zilizo na maagizo ya kujiendesha zenyewe zilivumbuliwa lini? Je, zilivumbuliwa karne chache zilizopita wakati wa mvuvumko wa kiviwanda huko Ulaya? Huenda ukashangaa kujua kwamba mashine zinazojiendesha zenyewe zilivumbuliwa mapema zaidi ya wakati huo.

Mwanzoni mwa kipindi ambacho elimu ya kisayansi katika milki ya Kiislamu ilikuwa imefikia kilele chake, kuanzia karne ya 8 hadi ya 13 W.K. hivi, wasomi huko Mashariki ya Kati walitafsiri katika Kiarabu vitabu vya kisayansi na kifalsafa vya Wagiriki mashuhuri kama vile Archimedes, Aristoto, Ctesibius, Hero wa Aleksandria, and Philo wa Bizantiamu. * Wakiwa na vitabu hivyo na vingine, wataalamu katika Milki ya Kiislamu​—ambayo ilianzia Hispania, kupitia Afrika Kaskazini, Mashariki ya kati, hadi Afghanistan—​walikuwa na ujuzi ambao uliwawezesha kutengeneza mashine zinazojiendesha zenyewe.

Mwanahistoria wa teknolojia, Donald Hill, anasema kwamba mashine hizo “zingeendelea kufanya kazi kwa vipindi virefu—saa, siku, au hata kipindi kirefu zaidi—bila kusimamishwa na mwanadamu.” Hilo liliwezekanaje? Mainjinia walikuwa wamebuni mifumo ya kudhibiti mashine hizo iliyoziwezesha kujiendesha zenyewe. Mashine hizo zilitumia maji yaliyokuwa kwenye matangi yaliyowekwa mahali palipoinuka ili kutokeza nishati kwa ukawaida. Zilikuwa na swichi iliyowezesha valvu kujifungua na kujifunga au kubadili mkondo wa maji. Mashine hizo zilikuwa pia na valvu iliyofunga maji yalipofurika na kufunguka yalipopungua, na pia kile ambacho Hill alikiita “kifaa cha zamani cha kukinga mashine isiharibike ikiwa kungekuwa na hitilafu.” Ona mifano michache.

Banu Musa Wabunifu

Banu Musa watatu waliishi katika karne ya tisa huko Baghdad. Banu Musa ni neno la Kiarabu linalomaanisha “wana wa Musa.” Wana hao walitumia vitabu vya Wagiriki waliowatangulia kama vile Philo na Hero, na pia vya mainjinia Wachina, Wahindi, na Waajemi kubuni vifaa zaidi ya 100. Mwandishi wa mambo ya kisayansi, Ehsan Masood, anasema kwamba vifaa hivyo vilitia ndani mabubujiko ya maji ambayo yalibadili mwelekeo wake baada ya muda hususa, saa ambazo zilikuwa na madoido yenye kuvutia, na mashine zilizowamiminia watu vinywaji na kujaza vinywaji kwenye kopo kwa kutumia boya, valvu, na mirija. Kulingana na mwanahistoria wa sayansi Jim Al-Khalili, wana wa Musa pia walitengeneza mashine sahili—mashine iliyokuwa kama “msichana wa chai,” ambayo iliwamiminia watu chai, na mashine iliyocheza filimbi, “ambayo huenda ndiyo iliyokuwa mashini ya zamani zaidi yenye maagizo ya kujiendesha yenyewe.”

Mashine hizo zilifanana sana na mashine za kisasa. Hata hivyo, “ziliendeshwa kwa maji yenye nguvu badala ya umeme, lakini zilitumia kanuni zilezile za utendaji,” anaandika Ehsan Masood, mwandishi wa mambo ya kisayansi.

Al-Jazari​—“Mvumbuzi wa Roboti”

Katika mwaka wa 1206, Ibn al-Razzaz al-Jazari alimaliza kuandika kitabu chake ambacho nyakati nyingine kinatafsiriwa Muhtasari wa Nadharia na utumizi wa Stadi za Umekanika (Compendium on the Theory and Practice of the Mechanical Arts). Kitabu hicho kimetajwa kuwa “ujuzi wa hatua kwa hatua wa ubuni wa mashine.” Baadhi ya teknolojia aliyotumia al-Jazari iliendelea kutumiwa muda mrefu baada ya kuchapishwa kwa vitabu vilivyoandikwa na Banu Musa, na ufafanuzi na michoro yake ilikuwa na habari nyingi sana hivi kwamba mainjinia wa kisasa wanaweza kutumia ujuzi huo kutengeneza vifaa hivyo.

Kitabu cha al-Jazari kina michoro ya vifaa vya kuinua maji, saa zinazoendeshwa na maji, saa za mishumaa, mashine za kutoa maji, mashine za muziki, na pampu inayoweza kugeuza mzunguko wa gurudumu la kupigia maji lisonge mbele na nyuma kama pistoni inayopiga maji kwa nguvu. Wanahistoria wanasema kwamba al-Jazari ndiye aliyekuwa wa kwanza kubuni pampu inayoendeshwa kwa maji karne tatu kabla ya muundo huohuo kubuniwa huko Ulaya.

Al-Jazari pia alibuni saa zenye muundo wenye kuchekesha lakini zilizofanya kazi. Saa iliyoonyeshwa hapa iliundwa upya katika eneo la maduka la Dubai. Mashine inayoendesha saa hiyo ni bakuli lililotobolewa mashimo ambalo limewekwa kwenye kidimbwi cha maji ndani ya tumbo la ndovu. Bakuli hilo hujaa maji baada ya dakika 30 kisha huzama na kutokeza utendaji mwingi unaohusisha kamba na mipira inayotoka katika “kasri” lililo mgongoni mwa ndovu. Mzunguko huo wa nusu saa unapokamilika, bakuli la maji hulea tena, na mzunguko unaanza tena. Saa hiyo na mashine nyingine zinazojiendesha zenyewe ambazo zilibuniwa na al-Jazari zimefanya aiitwe “mvumbuzi wa roboti.”

Ubunifu wa mwanadamu tangu zama za kale unastaajabisha sana! Lakini ubunifu huo hautustaajabishi tu. Unatusaidia tuone mambo kwa njia pana. Wakati watu wengi wanapojivunia teknolojia ya kisasa, tunakumbushwa kwamba teknolojia hiyo ilivumbuliwa na watu werevu na wabunifu walioishi kabla yetu.

^ fu. 3 Kuhusu kazi ya kutafsiri iliyofanywa na Wasomi Waarabu, ona makala “Jinsi Kiarabu Kilivyokuja Kuwa Lugha ya Wasomi,” katika toleo la Amkeni! la Februari?2012.

Pump: © Gianni Dagli Orti/The Art Archive at Art Resource, NY; clock: © The Metropolitan Museum of Art/Art Resource, NY