Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tetemeko la Haiti—Imani na Upendo Zadhihirika

Tetemeko la Haiti—Imani na Upendo Zadhihirika

Tetemeko la Haiti—Imani na Upendo Zadhihirika

Jumanne, (Siku ya 2), Januari 12, 2010, saa 10:53 jioni, Evelyn alisikia ngurumo kama ya ndege kubwa ya abiria ikianza kupaa, na ardhi ikaanza kutetemeka. Karibu na eneo alilokuwa, nguzo za saruji zilianza kupasuka kwa sauti, nayo majengo yakaanguka. Tetemeko lilipokwisha, Evelyn alielekea mahali ambapo angeweza kuona eneo lote. Kila mahali aliwasikia watu wakipiga mayowe. Wingu kubwa la vumbi liliinuka kutoka kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.

BAADA ya sekunde chache tu, nyumba, majengo ya serikali, benki, hospitali, na shule ziliporomoka. Watu wa matabaka yote walikufa—zaidi ya watu 220,000. Watu 300,000 wakajeruhiwa.

Watu wengi waliookoka waliketi chini wakiwa wamepigwa na butwaa kando ya nyumba zao zilizoporomoka. Wengine walichimba maporomoko hayo kwa wasiwasi kwa kutumia mikono yao ili kuwaokoa watu wa ukoo na majirani. Umeme ulipotea na giza likatanda na hivyo kuwalazimu waokoaji kufanya kazi kwa kutumia tochi na mishumaa.

Katika jiji la Jacmel, Ralphendy mwenye umri wa miaka 11 alikuwa amenaswa katika jengo ambalo sehemu yake ilikuwa imeanguka. Kwa saa kadhaa, kikundi cha waokoaji kilifanya kazi kwa bidii ili kumwokoa. Matetemeko mengine yaliyofuatia yaliwalazimisha kuacha kwa sababu waliogopa kuangukiwa na sehemu ile nyingine ya nyumba. Philippe, ambaye ni mmishonari na Shahidi wa Yehova, alikataa kuacha na anaeleza, “Singeweza kumwacha Ralphendy hapo ndani afe.”

Philippe na watu wengine watatu walijipenyeza kupitia nafasi ndogo chini ya jengo hilo liliporomoka na kukaribia polepole hadi mahali ambapo Ralphendy alikuwa, miguu yake ikiwa imenaswa. Polepole kuanzia saa sita usiku, walitoa vitu vilivyokuwa vimemwangukia. Kila mara tetemeko lingine lilipotokea, walisikia saruji iliyokuwa juu yao ikisonga na kuvunjika. Saa 11 asubuhi, zaidi ya saa 12 baada ya tetemeko hilo la nchi, walifaulu kumtoa Ralphendy chini ya nyumba hiyo iliyoporomoka.

Kwa kusikitisha, si jitihada zote kama hizo zilizofaulu. Katika jiji la Léogâne lililoathiriwa sana, Roger na mwana wake mkubwa, Clid, walikimbia kutoka ndani ya nyumba yao ilipokuwa ikiporomoka. Mwana wake mdogo, Clarence alikufa. Mke wa Roger, Clana, alikuwa hai na angeweza kuzungumza, lakini kichwa chake kilikuwa kimenaswa na dari iliyomwangukia. Roger na rafiki yake walijitahidi kumwokoa. “Fanyeni haraka!” aliwasihi kutoka chini ya rundo hilo. “Nguvu zangu zinakwisha! Hewa inaniishia!” Saa tatu hivi baadaye, kikundi cha waokoaji kilifika. Lakini walipomtoa, alikuwa amekufa.

Jumatano (Siku ya 3), Januari 13, Siku ya 2 Baada ya Tetemeko

Kulipoanza kukucha siku iliyofuata mtu angeweza kuona uharibifu huo ulikuwa mkubwa kadiri gani. Sehemu kubwa ya Port-au-Prince ilikuwa magofu. Habari kuhusu uharibifu huo ilipoenea katika sehemu nyingine za ulimwengu, mashirika ya kutoa msaada pamoja na watu wengine wenye kujitoa kutoka sehemu zote ulimwenguni walifika kusaidia. Wajitoleaji katika ofisi ya Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Dominika, iliyo umbali wa kilomita 300 hivi walikuwa pia wamesikia tetemeko hilo. Walipojua kwamba kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa karibu na eneo lenye watu wengi sana la Port-au-Prince, eneo ambalo ni makao ya karibu asilimia 33 ya watu wote milioni tisa nchini Haiti, Mashahidi nchini Dominika walianza mara moja kupanga njia za kutoa misaada.

Miaka 150 imepita tangu Haiti ilipokumbwa na tetemeko kubwa la nchi. Kwa sababu hiyo, watu nchini Haiti walikuwa wameacha kujenga nyumba zinazoweza kudhibiti matetemeko ya nchi na badala yake kujenga zile zinazoweza kuwalinda kutokana na vimbunga na mafuriko. Hivyo, kuta nyingi zilizotengenezwa kwa mawe na paa nzito zilizotengenezwa kwa saruji hazingeweza kustahimili tetemeko hilo lenye kipimo cha 7.0 kwenye kipimo cha Richter. Hata hivyo, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Haiti iliyokamilishwa katika mwaka wa 1987, ilikuwa imejengwa kupatana na viwango vya ujenzi vya maeneo yaliyo na uwezekano wa kupatwa na matetemeko ya nchi. Ingawa ofisi hiyo imejengwa karibu na upande wa mashariki wa Port-au-Prince, haikuharibika.

Katika usiku huo mmoja, ofisi hiyo nchini Haiti iligeuka kuwa kituo kilicho na kazi nyingi ya kutoa msaada. Kwa kuwa haikuwezekana kuwasiliana kwa simu au kwa kutumia barua-pepe, washiriki wa ofisi hiyo walisafiri mara mbili hadi kwenye mpaka wa Jamhuri ya Dominika ili watume ripoti. Wakati huohuo, mamia ya watu waliokuwa wamejeruhiwa, wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya sana, walimiminika kwenye ofisi ya tawi ya Haiti. Wengine wengi walipelekwa kwenye hospitali za eneo hilo, na upesi zilijaa kupita kiasi.

Katika eneo la hospitali, watu walilala ardhini—wakitokwa na damu na kupiga mayowe. Mmoja wao alikuwa Marla, ambaye alikuwa amefunikwa kwa saa nane chini ya nyumba iliyoanguka. Miguu yake ilikuwa imekufa ganzi na hangeweza kuisogeza. Majirani walimwokoa na kumpeleka hospitalini, lakini hospitali gani? Evan, Shahidi ambaye ni daktari, aliyekuwa amefika mapema kutoka Jamhuri ya Dominika, alienda kumtafuta lakini alijua tu jina lake.

Kufikia wakati huo, zaidi ya saa 24 zilikuwa zimepita baada ya tetemeko hilo kutukia na usiku ulikuwa umeingia. Akipita juu ya maiti zilizokuwa nje ya hospitali moja, Evan alisali kimyakimya huku akimwita Marla kwa sauti. Mwishowe, alisikia mtu akijibu, “Naam!” Marla alikuwa akimtazama huku akitabasamu kwa uchangamfu. Evan akamwuliza hivi akiwa ameshangaa, “Mbona unatabasamu?” Akamjibu, “Ni kwa sababu sasa niko na ndugu yangu wa kiroho.” Evan alitokwa na machozi.

Alhamisi (Siku ya 4), Januari 14, Siku ya 3 Baada ya Tetemeko

Makao makuu ya Mashahidi wa Yehova, huko Marekani—kutia ndani ofisi nyingine za tawi huko Guadeloupe, Jamhuri ya Dominika, Kanada, Martinique, Ufaransa, Ujerumani, na kwingine—yalisimamia kazi ya kutoa msaada ili chakula, maji, dawa na vitu vingine, kutia ndani usafiri, mawasiliano, pesa, na wafanyakazi waongozwe kwa njia inayofaa zaidi. Kwa ujumla, madaktari 78 ambao ni Mashahidi wa Yehova walifika ili kusaidia, pamoja na wajitoleaji wengine wengi. Kufikia saa 8:30 usiku, lori la kwanza liliondoka kwenye ofisi ya tawi ya Dominika likielekea Haiti likiwa na kilogramu 6,804 hivi za chakula, maji, dawa, na vitu vingine.

Lori hilo lilipofika asubuhi, wafanyakazi wa ofisi ya tawi nchini Haiti walianza kugawa vitu hivyo. Ili kuwapumbaza wezi wasiibe chakula na kwenda kukiuza, wafanyakazi hao wa kutoa msaada walificha mizigo yao kwa ujanja. Wajitoleaji walifanya kazi mchana na usiku wakipakia chakula na vifaa vingine katika mifuko midogo kwa ajili ya familia na watu mmojammoja. Katika miezi iliyofuata, Mashahidi wa Yehova walisambaza, bila malipo, zaidi ya kilogramu 450,000 za vitu vilivyochangwa, kutia ndani zaidi ya milo 400,000.

Ijumaa (Siku ya 5), Januari 15, Siku ya 4 Baada ya Tetemeko

Kufikia saa sita hivi mchana, jumla ya Mashahidi 19 ambao ni madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa kitiba kutoka Jamhuri ya Dominika na Guadeloupe walikuwa wamefika Haiti. Upesi walifungua kliniki ya kutoa huduma ya kwanza. Waliwatibu watu waliojeruhiwa kutia ndani watoto katika kituo cha watoto mayatima. Zaidi ya hilo, Mashahidi hao waliwapa wasimamizi wa kituo hicho chakula na turubai. “Ninawashukuru sana Mashahidi wa Yehova,” anasema Étienne, msimamizi wa kituo hicho. “Sijui tungefanya nini bila msaada wao.”

Alipotea Lakini Akapatikana

Tetemeko hilo lilipotokea, Islande mwenye umri wa miaka saba alitazama nje ya nyumba na kuona nyaya za stima zikikatika na cheche za moto zikiruka. Ndani ya nyumba, kuta zilianza kuyumbayumba na mawe yakamwangukia, yakavunja mguu wake, naye akajeruhiwa sana. Baada ya kuokolewa, baba yake, Johnny, alivuka mpaka na kumpeleka Islande kwenye hospitali katika Jamhuri ya Dominika. Akiwa huko, alipelekwa kwa ndege hadi kwenye hospitali iliyo katika mji mkuu, Santo Domingo. Lakini Johnny alipopiga simu baadaye kwenye hospitali hiyo, Islande hakuwapo.

Kwa siku mbili Johnny alimtafuta Islande kila mahali lakini hakumpata. Alikuwa amepelekwa kwenye hospitali tofauti ambako mjitoleaji mmoja alimsikia akisali kwa Yehova. (Zaburi 83:18) “Je, unampenda Yehova?” mjitoleaji huyo akauliza. “Ndiyo,” Islande akajibu huku akitokwa na machozi. “Basi usijali,” mjitoleaji huyo akamwambia. “Yehova atakusaidia.”

Johnny aliomba Ofisi ya Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Dominika imsaidie kumtafuta Islande. Shahidi anayeitwa Melanie alisema atamtafuta. Melanie alipouliza katika hospitali moja, yule mjitoleaji aliyekuwa amemsikia Islande akisali alisikia mazungumzo yao na akamwonyesha msichana huyo. Punde baada ya hapo, Islande alikutanishwa tena na familia yake.

Upasuaji na Mazoezi

Watu wengi waliojeruhiwa hawakutibiwa kabla ya kupelekwa kwenye kliniki iliyoanzishwa kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi nchini Haiti, na kwa sababu hiyo viungo vyao vingi vilikuwa na vidonda visivyoweza kupona. Katika visa vingi, viungo hivyo vilihitaji kukatwa ili kuokoa uhai wa mgonjwa. Siku chache za kwanza baada ya tetemeko hilo, kulikuwa na upungufu wa vifaa vya kufanyia upasuaji, dawa, na hata dawa za unusukaputi. Hali hiyo iliwaathiri madaktari vilevile. Mmoja wao alisema, “Mimi humwomba Mungu anisaidie nisahau mambo niliyoona na sauti nilizosikia.”

Juma moja baada ya tetemeko hilo, madaktari ambao ni Mashahidi kutoka Ulaya ambao walikuwa na uzoefu na vifaa vya kufanya upasuaji tata na uliohitajika haraka walianza kuwasili. Madaktari hao walifanya upasuaji 53 na wakawatibu maelfu ya watu. Wideline, Shahidi mwenye umri wa miaka 23, alifika Port-au-Prince siku moja kabla ya tetemeko hilo. Mkono wake wa kulia ulivunjwa-vunjwa wakati wa tetemeko hilo na ukalazimika kukatwa katika hospitali. Baadaye watu wake wa ukoo walimpeleka kwenye hospitali iliyokuwa mwendo wa saa saba kutoka nyumbani kwao huko Port-de-Paix. Lakini hali ya Wideline iliendelea kudhoofika nao wafanyakazi wa hospitali hiyo wakamwacha afe.

Kikundi hicho cha Mashahidi waliokuwa wakishughulikia matibabu kiliposikia kuhusu hali yake, walisafiri kutoka Port-au-Prince ili wamtibu Wideline na kumsafirisha hadi mji mkuu ili apate matibabu zaidi. Wagonjwa wengine walipoona kwamba ndugu zake wa kiroho walikuwa wamekuja kumchukua, walipiga makofi. Kwa msaada wa familia na kutaniko lake, sasa Wideline anajaribu kuzoea hali zake mpya.

Katika Jamhuri ya Dominika, Mashahidi wa Yehova walikodi nyumba ambazo zingetumika kama mahali pa kufanya mazoezi kwa wagonjwa waliopelekwa huko. Nyumba hizo zilishughulikiwa na Mashahidi waliojitolea kwa zamu—madaktari, wauguzi, madaktari wa kunyoosha viungo, na wengine. Waliwatunza wagonjwa kwa uchangamfu walipokuwa wakipata nafuu.

Kuwaeleza Wengine Kuhusu Imani, Tumaini, na Upendo

Ni majumba 6 tu yaliyoharibika kati ya Majumba 56 ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova nchini Haiti yaliyokuwa katika eneo la tetemeko hilo. Mashahidi wengi walioathiriwa na tetemeko hilo waliishi katika majumba hayo ambayo hayakuwa yameharibiwa au katika maeneo mengine yaliyokuwa wazi. Mashahidi hao, ambao tayari walikuwa wamezoea kukutana pamoja, walijipanga kama wanavyofanya kwa ajili ya makusanyiko yao.

“Tulidumisha mpango wa kawaida wa kutaniko wa programu za kiroho,” akaeleza Jean-Claude, mwangalizi wa Mashahidi wa Yehova wa eneo hilo, “na kuwatia nguvu vijana na wazee.” Matokeo yalikuwa nini? “Ninafurahi sana kuwaona Mashahidi wa Yehova wakiendelea kuhubiri,” akasema mwanamume mmoja. “Ikiwa hatungewaona, basi tungehisi kwamba mambo ni mabaya zaidi.”

Mashahidi waliwafariji sana watu. “Karibu kila mtu tunayemkuta anaamini kwamba tetemeko hilo lilikuwa adhabu kutoka kwa Mungu,” anaeleza Shahidi mmoja. “Tunawahakikishia kwamba tetemeko hilo lilikuwa tu msiba wa asili na haukusababishwa na Mungu. Tunawaonyesha Mwanzo 18:25. Hapo Abrahamu anasema kwamba ni jambo lisilowaziwa kwa Mungu kuwaharibu watu wazuri pamoja na wabaya. Pia tunawaonyesha Luka 21:11. Katika mstari huo Yesu alitabiri kwamba wakati huu kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi, na tunawaeleza kwamba hivi karibuni atawafufua wapendwa wetu waliokufa na kuondoa kuteseka kote. Watu wengi wanashukuru sana tunapowaeleza mambo hayo.” *

Bado kuna hali ngumu. “Msiba wa kwanza ulikuwa tetemeko la nchi. Sasa lazima tukabiliane na athari zake,” akasema Jean-Emmanuel, daktari ambaye ni Shahidi. “Mbali na hatari ya kulipuka kwa magonjwa mengi katika kambi zilizojaa, zisizo safi, na zilizojaa maji ya mvua, kuna matatizo ya kihisia ambayo yamefungiwa moyoni lakini hayawezi kuondoka.”

Majuma kadhaa baada ya tetemeko hilo, Shahidi mmoja alikuja kwenye kliniki akilalamika anaumwa na kichwa kwa kuendelea na hawezi kulala, ambayo ni matatizo ya kawaida baada ya msiba kutokea. “Je, uligongwa na kitu kichwani?” muuguzi mmoja Shahidi akamwuliza. “Hapana,” akajibu bila hisia zozote. “Mke wangu ambaye tulioana miaka 17 iliyopita alikufa. Lakini tulitazamia mambo kama hayo. Yesu alisema yangetukia.”

Akitambua kiini cha tatizo lake, muuguzi huyo akamwambia: “Lakini umepoteza mwenzi wako wa maisha. Hilo si jambo dogo! Hakuna ubaya kuhuzunika na kulia. Yesu alilia wakati rafiki yake Lazaro alipokufa.” Aliposema hivyo, mwanamume huyo aliangua kilio.

Kati ya zaidi ya Mashahidi 10,000 katika eneo hilo, 154 walikufa katika tetemeko hilo. Inakadiriwa kwamba zaidi ya asilimia 92 ya wakazi wa Port-au-Prince wamepoteza mtu mmoja au zaidi wa familia katika msiba huo. Ili kuwasaidia watu hao wanaoomboleza, Mashahidi wa Yehova wamewatembelea tena na tena watu ambao wameathiriwa kimwili na kihisia, na kuwapa nafasi ya kumweleza mtu wanayemtumaini hisia zao. Mashahidi waliokuwa wakiomboleza tayari walijua kuhusu ahadi ya Biblia ya ufufuo na dunia paradiso, lakini pia walihitaji kuwaeleza Wakristo wenzao wenye hisia-mwenzi jinsi wanavyohisi na kuambiwa maneno yenye huruma na yenye kutia moyo.

Kukabiliana na Hali Sasa na Wakati Ujao

Mtume Paulo aliandika hivi: “Inabaki imani, tumaini, upendo, hayo matatu; lakini lililo kubwa zaidi kati ya hayo ni upendo.” (1 Wakorintho 13:13) Sifa hizo zinawawezesha Mashahidi wengi wa Haiti kukabiliana na hali za sasa, kuwatia moyo wengine, na kutazamia wakati ujao bila woga. Imani ya kweli, umoja, na upendo unaonekana wazi katika jitihada ya kimataifa ya kutoa msaada inayoendelea. “Sijawahi kujionea upendo mwingi sana kama huo,” akasema Petra, daktari ambaye ni Shahidi aliyetoka Ujerumani kwenda kusaidia. “Nimelia sana, lakini nimelia zaidi kwa shangwe badala ya uchungu.”

Jarida The Wall Street Journal lilisema kuwa tetemeko la Haiti la mwaka wa 2010 ndio “msiba wa asili uliosababisha uharibifu mkubwa zaidi kuwahi kutukia katika nchi moja.” Hata hivyo, tangu lilipotukia, ulimwengu umekumbwa na misiba mingine, ya asili na ile iliyosababishwa na wanadamu. Je, kuna wakati itakapokwisha? Mashahidi wa Yehova nchini Haiti na ulimwenguni pote wana uhakika kwamba hivi karibuni sana Mungu atatimiza ahadi hii ya Biblia: “Atafuta kila chozi kutoka katika macho yao, na kifo hakitakuwapo tena, wala maombolezo wala kilio wala maumivu hayatakuwapo tena. Mambo ya zamani yamepitilia mbali.”—Ufunuo 21:4.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 31 Ona sura ya 11, “Kwa Nini Mungu Anawaacha Watu Wateseke?,” katika kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Blabu katika ukurasa wa 15]

“Singeweza kumwacha Ralphendy hapo ndani afe”

[Blabu katika ukurasa wa 19]

“Ninafurahi sana kuwaona Mashahidi wa Yehova wakiendelea kuhubiri”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

KUWAJENGEA MAKAO WALIOATHIRIWA

Katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya tetemeko hilo, Mashahidi wa Yehova ambao ni wahandisi wa majengo ya umma walianza kukagua nyumba ambazo ni salama ili familia zirudi ndani. Wengi kati ya wale waliopoteza nyumba zao walihitaji makao ya muda kabla ya kupata tena nyumba za kudumu.

“Kwa kuiga kile ambacho mashirika ya kimataifa ya kutoa msaada yamefanya, tulijenga nyumba zisizogharimu pesa nyingi, zinazoweza kujengwa kwa urahisi, na zenye ukubwa kama ule ambao watu wengi walikuwa wakiishi kabla ya tetemeko hilo,” anaeleza John, mfanyakazi wa ofisi ya tawi nchini Haiti. “Nyumba hizo zinaandaa kinga kutokana na mvua na upepo, bila kuhatarisha familia iwapo tetemeko lingine litatokea.” Majuma matatu tu baada ya tetemeko hilo, wajitoleaji wa Haiti na wa kimataifa walianza kujenga nyumba hizo za muda.

Watu barabarani walishangilia malori yalipopita yakiwa yamebeba sehemu zilizokuwa zimetayarishwa za nyumba hizo. Ofisa mmoja wa forodha wa Haiti, alipokuwa akiidhinisha kuingizwa nchini kwa vifaa hivyo vya ujenzi, alisema hivi: “Mashahidi wa Yehova walikuwa kati ya watu wa kwanza kuvuka mpaka ili kuwasaidia watu. Hawazungumzi tu kuhusu kutoa msaada, wao hutenda.” Miezi michache baada ya tetemeko hilo, tayari nyumba 1,500 zilikuwa zimejengwa na Mashahidi kwa ajili ya wale waliokuwa wamepoteza makao yao.

[Ramani katika ukurasa wa 14]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

HAITI

PORT-AU-PRINCE

Léogâne

Chanzo cha tetemeko

Jacmel

JAMHURI YA DOMINIKA

[Picha katika ukurasa wa 16]

Marla

[Picha katika ukurasa wa 16]

Islande

[Picha katika ukurasa wa 16]

Wideline

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kikundi cha Mashahidi wa Yehova wa Haiti wakienda kuwafariji watu walioathiriwa na tetemeko hilo

[Picha katika ukurasa wa 18]

Daktari akimtibu mvulana katika kliniki iliyoanzishwa na Mashahidi wa Yehova