Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Wizara ya Mambo ya Kidini ya Serbia imekubali ombi la Mashahidi wa Yehova la kuandikishwa kwa shirika lao la kisheria. Kulingana na rekodi za serikali, Mashahidi wa Yehova wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika nchi hiyo tangu mwaka wa 1930.

Inakadiriwa kwamba asilimia 95 ya muziki uliopakuliwa kutoka kwenye Intaneti ulimwenguni pote katika mwaka 2009, ulipakuliwa kinyume cha sheria.—TIME, MAREKANI.

Matetemeko ya Nchi ‘Yalisababisha Vifo Vingi Zaidi’

“Matetemeko ya nchi ndiyo yaliyosababisha vifo vingi zaidi katika miaka kumi iliyopita,” linasema shirika la Umoja wa Mataifa la Mbinu za Kimataifa za Kupunguza Misiba, huko Geneva, Uswisi. Kati ya watu waliokufa kwa sababu ya misiba katika kipindi hicho, asilimia 60 waliuawa na matetemeko ya nchi. Msiba huo wa asili unaendelea kuwa hatari kubwa, unapozingatia kwamba 8 kati ya majiji 10 yenye watu wengi ulimwenguni pote yako katika maeneo yanayoweza kukumbwa na matetemeko ya nchi kwa sababu ya nyufa zilizo chini ya dunia. Katika miaka kumi iliyopita, watu zaidi ya 780,000 wamekufa katika matukio 3,852 yaliyoorodheshwa kuwa misiba.

Kazi Hatari

“Katika mwaka wa 2009, jumla ya waandishi wa habari 110 waliuawa wakiwa kazini, hilo likifanya mwaka jana kuwa ndio mwaka hatari zaidi katika miaka kumi iliyopita” kwa waandishi wa habari, inasema Taasisi ya Kimataifa ya Uandishi wa Habari, huko Vienna, Austria. Katika maeneo yenye vita kama vile Afghanistan, Iraki, Pakistan, na Somalia, “waandishi wa habari wameuawa kimakusudi” katika miaka ya hivi karibuni, inasema ripoti hiyo. Hilo limefanya kuwe na habari chache kuhusu maeneo hayo na hivyo ‘watu hawajui kinachoendelea katika maeneo hayo.’ Katika miaka kumi iliyopita, Iraki ndio nchi iliyokuwa hatari zaidi kwa waandishi wa habari, ikifuatiwa na Filipino, Kolombia, Mexico, na kisha Urusi.

Bidhaa za Bei ya Chini Zinapunguza Uhalifu

Huenda “kupatikana kwa wingi kwa bidhaa za kielektroniki za bei ya chini” kukafanya wezi nchini Uingereza wakose kazi, kulingana na ripoti moja ya shirika la habari la Reuters huko Uingereza, likimnukuu James Treadwell, mkufunzi wa mambo ya uhalifu katika Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza. Kwa mfano, mashini za kucheza DVD zinauzwa kwa bei ya chini sana hivi kwamba haziwezi kuuzwa tena kwa faida. “Hakuna haja ya kuziiba,” anasema Treadwell. Hata hivyo, kupunguzwa kwa bei ya bidhaa hakujakomesha uhalifu. Badala yake, wezi sasa wanawapora watu bidhaa za bei ya juu na zinazoweza kuuzwa kwa urahisi ‘kama vile simu za mkononi na iPod ambazo watu hubeba.’ Wezi waliokuwa wakivunja nyumba sasa wameanza kuwavamia watu njiani.