Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Makadamia—Kokwa Tamu za Australia

Makadamia—Kokwa Tamu za Australia

Makadamia—Kokwa Tamu za Australia

MTAALAMU wa mimea Walter Hill alimtazama mfanyakazi wake mvulana kwa wasiwasi. Mvulana huyo alikuwa amekula kokwa za mti uliokuwa tu umegunduliwa katika misitu ya mvua ya kusini-mashariki ya Queensland, Australia. Hill alikuwa amesikia kwamba kokwa hizo zilikuwa na sumu. Lakini mvulana huyo hakuwa mgonjwa wala hakufa. Badala yake, alisema kwamba zilikuwa tamu. Kwa hiyo, Hill akala kokwa moja na akalifurahia. Muda mfupi baada ya hapo akaanza kuwasambazia marafiki na wataalamu wa mimea ulimwenguni pote miche ya makadamia. *

Leo, miaka 150 hivi baadaye, watu ulimwenguni pote wanafurahia sana kula kokwa za makadamia. Jarida Chronica Horticulturae linaeleza hivi: “Makadamia inasemekana kuwa kokwa bora zaidi ulimwenguni kwa sababu ya ladha yake ya kipekee, na rangi ya malai.” Si ajabu kwamba kokwa za makadamia ndizo huletea Australia faida kubwa zaidi!

Kokwa Lenye Ganda Gumu

Miti ya makadamia ya kijani kibichi inakua kwa wingi kwenye pwani ya mashariki ya Australia. Aina mbili kati ya tisa za miti hiyo hutokeza kokwa zinazoweza kuliwa, na zina ganda gumu la nje lenye nyuzinyuzi; ganda la mviringo lenye rangi ya kahawia, na mbegu ndogo yenye rangi ya malai.

Hata hivyo, si rahisi kuvunja ganda hilo la nje. * Wenyeji wa Asili wa Australia walitumia mawe kulivunja. John Waldron aliyekuwa mkulima wa miti ya kokwa alitumia nyundo na fuawe. Akitumia vifaa hivyo katika kipindi cha zaidi ya miaka 50, alipasua maganda zaidi ya milioni nane. Je, mashini zingesaidia katika kazi hiyo? Miundo ya mapema haikupendwa kwa kuwa iliharibu kokwa lililokuwa ndani. Hata hivyo, baada ya muda mashini bora zaidi zilibuniwa.

Tatizo lingine lilikuwa kuzalisha. Kokwa zilipopandwa kutoka kwenye miti mizuri mara nyingi zilitokeza kokwa za hali ya chini. Jitihada za kupandikiza hazikufaulu. Wakikabiliwa na matatizo hayo, ukuzaji wa kibiashara haukufaulu, hadi wakulima wa Hawaii walipokabiliana na tatizo hilo. Wao walifaulu. Kwa sababu hiyo, walianza kusambaza asilimia 90 ya kokwa za makadamia ulimwenguni. Si ajabu kwamba kokwa hizo zilianza kuitwa kokwa za Hawaii.

Kisha katika miaka ya 1960, wakulima Waaustralia “wakaanza kukazia fikira ukuzaji wa makadamia kwa ajili ya biashara,” wakitumia mbinu zilizogunduliwa huko Hawaii. Kwa sababu hiyo, biashara ikaanza kukua hivi kwamba sasa Australia inatokeza asilimia 50 hivi ya kokwa za makadamia ulimwenguni. Makadamia pia hukuzwa Afrika, Asia, na Amerika ya Kati.

Kutembelea Shamba la Australia

Mwandishi wa Amkeni! alimtembelea Andrew, aliye na shamba la makadamia karibu na mji wa Lismore, New South Wales. “Tunakuza aina mbalimbali za makadamia baada ya kila mstari, ili miti hiyo iweze kuchavushana,” akaeleza Andrew. Mwandishi wa Amkeni! alielezwa kwamba asilimia 80 ya mamilioni ya miti inayokuzwa nchini Australia ni miti iliyochaguliwa na wakuzaji wa Hawaii. Hata hivyo, wakuzaji wa miti hiyo nchini Australia wanatumia chembe kutoka kwenye makadamia zinazokua mwituni ili kuboresha miti ya kienyeji.

Tulipotazama miti yenye majani mengi, tuliona mamia ya kokwa zikining’inia kama mipira midogo. Kokwa hizo hukomaa baada ya miezi sita na kuanguka chini. Tuligundua kwamba kokwa kadhaa zilizoanguka zilikuwa na matundu. Andrew anasema: “Panya wanaweza kutafuna na kutoboa ganda kwa sekunde nane tu. Pia nguruwe-mwitu hupenda sana kokwa za makadamia.” Tunaposonga mbele, Andrew anapiga teke kokwa ambalo nusu yake ilikuwa imezikwa udongoni. “Hapo nimeokoa senti tatu [za Australia],” ananiambia huku akitabasamu. Wakulima wengi huvuna kokwa zao kwa kutumia mashini fulani ya pekee iliyo na pipa na vidole vifupi vya plastiki ambavyo huokota kokwa zilizoanguka. Ganda la nje la kokwa hizo huminywa kisha kokwa zinatenganishwa zikiwa shambani, halafu zinapelekwa kiwandani ambako ganda la ndani huvunjwa. Baada ya hapo kokwa zinakaguliwa na kusafirishwa kwa wanunuzi.

Yenye Ladha na Afya

Tunapomaliza matembezi yetu, tunakula kokwa kadhaa na kufurahia ladha yake tamu. Je, kokwa za makadamia zina faida kwa afya? Kiwango cha mafuta katika kokwa hizo (sehemu kubwa ni mafuta yasiyoganda, au mafuta mazuri) “ni zaidi ya asilimia 72, na hicho ndicho kiwango kikubwa zaidi cha mafuta katika kokwa yoyote,” linasema jarida fulani la serikali kuhusu kokwa za makadamia. Kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni, kula kiasi kinachofaa cha makadamia kunaweza kupunguza kolesteroli inayodhuru na mafuta yanayoitwa triglyceride na kupunguza tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu.

Watu hufurahia kula chokoleti, biskuti, au aiskrimu iliyotengenezwa kwa makadamia. Wengine hufurahia kula kokwa hizo zikiwa zimekaangwa, zikiwa zimetiwa chumvi, au moja kwa moja kutoka kwenye ganda lake. Vyovyote vile, watu wengi wanafurahia sana kula kokwa hizo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Miaka mingi mapema, wavumbuzi Cunningham (1828) na Leichhardt (1843) walikusanya kokwa za makadamia, lakini zilihifadhiwa bila kuchunguzwa. Mnamo 1857, Ferdinand von Mueller, mtaalamu wa mimea huko Melbourne aliyefanya kazi pamoja na Hill, alizitia katika jenasi ya Macadamia, jina la rafiki yake wa karibu Dakt. John Macadam.

^ fu. 6 Maganda ya makadamia ni magumu sana hivi kwamba yanatumika kulainisha vitu viwandani.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

MAGANDA YANATUMIWA KUTOKEZA UMEME

Maganda magumu ya makadamia yanaweza kutumiwa kama tu makaa ya mawe. Kwa sababu hiyo, kampuni fulani ya Australia inatumia maganda hayo kutokeza umeme kwa ajili ya kiwanda cha kokwa hizo na kwa ajili ya kusambaza umeme sehemu nyingine. Kiwanda hicho ndicho cha kwanza nchini Australia kujaribu mbinu ya kuzalisha umeme kwa kutumia takataka, na huenda kikatokeza umeme zaidi wakulima wanapoendelea kupeleka maganda yao huko.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Wakulima nchini Australia wanapanda mamia ya maelfu ya miti kila mwaka

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

All photos pages 22 and 23: Australian Macadamia Society