Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kusafirisha Chakula Moto Kutoka Nyumbani Hadi Ofisini Huko Mumbai

Kusafirisha Chakula Moto Kutoka Nyumbani Hadi Ofisini Huko Mumbai

Kusafirisha Chakula Moto Kutoka Nyumbani Hadi Ofisini Huko Mumbai

UNATOKA nyumbani kila siku saa kumi na moja asubuhi kwenda kazini. Wakati wa mchana unatamani sana kula chakula moto kilichotayarishwa vizuri nyumbani. Maelfu ya watu wanaofanya kazi huko Mumbai, India, hula chakula cha aina hiyo kinachosafirishwa kutoka nyumbani na dabbawala. *

Kutambua Nafasi ya Biashara

Kufikia mwisho wa karne ya 19, jiji la Mumbai, ambalo wakati huo lilikuwa likiitwa Bombay, lilikuwa kituo cha kibiashara kilichokuwa kikipanuka kikiwa na wafanyabiashara Waingereza na Wahindi waliokuwa wakisafiri mbali kwenda ofisini. Mfumo wa usafiri haukutegemeka na kulikuwa na mikahawa michache tu. Watu walitamani sana kula chakula kilichopikwa nyumbani kwa hiyo watumishi waliajiriwa kazi ya kubeba chakula hicho kutoka nyumbani kwa mwajiri hadi ofisini. Mfanyabiashara mmoja aliona hiyo ingekuwa biashara nzuri kwa hiyo, akawaajiri vijana kusafirisha chakula kwa ukawaida kutoka nyumbani hadi ofisini. Kuanzia hapo, biashara hiyo kubwa ikaanza.

Bado watu wanapenda kula chakula kilichopikwa nyumbani. Kwa kweli, ingawa sasa kuna mikahawa mingi zaidi, bado chakula kilichopikwa nyumbani ni cha bei nafuu na kinapendwa na wengi. Isitoshe, watu wengi wana matatizo ya afya na lazima wale vyakula maalumu. Wengine ni wafuasi wa dini zilizo na vizuizi kuhusu vyakula fulani. Kwa mfano, watu fulani hawali vitunguu nao wengine huepuka kula vitunguu saumu. Vingi kati ya vitu hivyo hutiwa katika vyakula vya mkahawa, kwa hiyo chakula kilichopikwa nyumbani husaidia kuondoa matatizo hayo kuhusu vyakula.

Huduma Yenye Kutegemeka Sana

Njia iliyotumiwa zamani haijabadilika sana, ingawa chakula kingi zaidi kinasafirishwa. Siku hizi, zaidi ya wanaume 5,000, kutia ndani wanawake wachache, wanasafirisha zaidi ya vyakula 200,000 kwa siku kutoka nyumbani hadi kwenye ofisi zilizo katika eneo la mjini lililo na zaidi ya watu milioni 20. Dabbawala hupeleka chakula hicho katika eneo lenye umbali wa kilomita 60, wengine wakitembea—labda wakivuta mkokoteni uliobeba vyakula vya watu 30 au 40—huku wengine wakitumia baiskeli au treni. Iwe watatumia njia gani, wao humfikishia mwenyewe chakula chake kwa wakati unaofaa. Inasemekana kwamba wanafanya kazi hiyo kwa usahihi wa hali ya juu hivi kwamba wanaweza kukosea mara 1 tu kati ya mara milioni 16! Wanafaulu jinsi gani kudumisha usahihi wa hali ya juu hivyo?

Katika mwaka wa 1956, dabbawala waliandikishwa kuwa shirika la kutoa msaada, na wakawa na kamati kuu na maofisa wengine. Vikundi vya wafanyakazi huwa na msimamizi, nao hufanya kazi kivyao. Hata hivyo, wote wanashirikiana na wana hisa katika shirika hilo nao wanadai kwamba muundo huo wa shirika lao ndio hufanya kazi yao ifanikiwe. Hata hawajawahi kuwa na mgomo tangu walipoanza kutoa huduma hiyo miaka 100 iliyopita.

Dabbawala hubeba vitambulisho na wanaweza kutambuliwa kwa urahisi kwa sababu wao huvalia shati jeupe, suruali isiyobana, na kofia nyeupe. Wakipatikana bila kofia, iwapo wanachelewa au kukosa kazi bila sababu nzuri, au wakipatikana wakinywa kileo wakati wa kazi, wanaweza kupigwa faini.

Kazi ya Kila Siku ya Dabbawala

Saa 2:30 asubuhi, mtu katika nyumba ya mteja, labda mke wake, ametayarisha chakula cha mchana na kukipakia ndani ya dabba. Dabba hizo huwa na makopo kadhaa ambayo huingiana moja juu ya nyingine na kuunganishwa kwa kutumia vishikio vya chuma. Dabbawala atakusanya makopo katika eneo moja, atayapakia juu ya baiskeli au mkokoteni wake, na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye kituo cha gari-moshi ambako atakutana na wengine katika kikundi chake. Wakiwa huko wanapanga makopo hayo kulingana na mahali yanapopaswa kufikishwa, kama tu wapeleka barua wanavyofanya.

Kila dabba huwa na herufi, namba, na rangi zinazoonyesha eneo ambalo chakula hicho kimetoka, kituo cha karibu cha gari-moshi, kituo ambacho kinapelekwa, jina la jengo, na namba ya orofa. Dabba zinazopaswa kupelekwa katika eneo moja huwekwa pamoja na kutiwa kwenye viunzi vya mbao vinavyoweza kubeba dabba 48 hivi. Treni inapofika, makopo hayo hutiwa katika eneo la pekee karibu na chumba cha dereva. Kisha, treni hiyo inapofika kwenye kituo kikuu, makopo hayo hupangwa tena na kusafirishwa hadi kwenye kituo cha mwisho. Makopo hayo hutenganishwa na mteja hufikishiwa chakula chake kwa baiskeli au mkokoteni.

Njia hizo za kusafirisha chakula zinafaa zaidi na pia hazigharimu pesa nyingi. Isitoshe, dabbawala hasumbuliwi na msongamano wa magari kwa kuwa anapita kando ya barabara au katikati ya magari. Kwa sababu hiyo, chakula hufikishwa kwenye ofisi inayofaa kufikia saa 6:30 mchana. Kisha, kati ya saa 7:15 na 8:00 alasiri, baada ya dabbawala kula chakula chake cha mchana, anakusanya makopo yote matupu na kuyarudisha nyumbani kwa mteja ambako mtu wa familia atayaosha na kuyatayarisha kwa ajili ya siku inayofuata. Kuanzia mwanzo hadi mwisho, kazi hiyo yote hufanywa haraka na kwa njia inayofaa, kama tu mbio za kupokezana!

Kazi ya Hali ya Chini Inayosifiwa Sana

Kazi ya dabbawala inasifiwa sana. Mashirika mengine yamechunguza mfumo wao wa usafirishaji, ili watumie mbinu hizo katika biashara zao. Sinema zimetokezwa kuwahusu dabbawala. Gazeti Forbes Global Magazine liliwapa cheti kinachoitwa Six Sigma kwa sababu ya usahihi wao wa hali ya juu. Wametajwa katika kitabu The Guinness Book of World Records na katika majarida ya utafiti ya Shule ya Biashara ya Harvard huko Marekani. Dabbawala wametembelewa na watu mashuhuri, kutia ndani mshiriki wa familia ya kifalme ya Uingereza ambaye alivutiwa sana na kazi yao hivi kwamba akawakaribisha baadhi yao wahudhurie harusi yake huko Uingereza.

Siku hizi dabbawala wanatumia kompyuta na simu za mkononi kuchukua maagizo na kuweka rekodi. Lakini njia yao ya usafirishaji haijabadilika. Wakati wa chakula cha mchana unapokaribia, wafanyakazi wengi wa ofisini huko Mumbai hufurahi kujua kwamba chakula moto kilichopikwa nyumbani kitaletwa hapohapo kazini—bila kuchelewa!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Dabba linamaanisha “kopo”; wala linamaanisha mtu anayefanya kazi hiyo. Neno hili huandikwa kwa njia mbalimbali.

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kupakia “dabba” kwenye treni

[Picha katika ukurasa wa 11]

“Dabba” lina makopo kadhaa yanayopangwa moja juu ya nyingine ili yabebwe na kusafirishwa kwa urahisi

[Picha katika ukurasa wa 12]

Makampuni mengi yamechunguza na kutumia mbinu bora ya kusafirisha bidhaa ya “dabbawala”