Gesi ya Asili—Nishati Inayotumiwa Nyumbani
Gesi ya Asili—Nishati Inayotumiwa Nyumbani
GESI YA ASILI hufanyiza zaidi ya asilimia 20 ya nishati yote inayotumiwa ulimwenguni pote. Gesi ya asili hutolewa wapi? Ni safi kadiri gani? Na ni kiasi gani kinachosalia?
Wanasayansi wengi wanaamini kwamba zamani sana gesi za asili zilifanyizwa kutokana na mabaki ya mimea na wanyama waliooza, kutia ndani mimea na wanyama wadogo wa baharini. Kulingana na nadharia hiyo, baada ya muda mrefu, vijidudu pamoja na shinikizo lililotokezwa na mabaki hayo na joto kutoka chini ardhini, yalibadili vitu hivyo vilivyooza kuwa nishati ya asili, yaani, makaa ya mawe, gesi, na mafuta. Baada ya muda, gesi nyingi ilifyonzwa katika miamba, na kuhifadhiwa ikiwa imefungiwa chini ya tabaka la mwamba usioweza kupenywa. Baadhi ya hifadhi hizo za gesi ni kubwa zikiwa na lita trilioni nyingi sana za gesi. Hifadhi hizo za gesi hupatikana jinsi gani?
Kutafuta Gesi ya Asili
Setilaiti zinazotambua vitu vilivyofichwa, mifumo ya kupokea habari kutoka kwenye setilaiti, mifumo ya kuchunguza matetemeko ya nchi, na kompyuta zimesaidia sana katika kazi ya kutafuta gesi ya asili. Mifumo ya kuchunguza matetemeko ya nchi hutumiwa kuchunguza sauti inayotoka katika miamba ardhini, na hivyo kuwasaidia wanasayansi kufahamu kilicho chini yake. Kwa kawaida sauti hizo hutokezwa na watu wanaotafuta gesi hizo kwa kutumia baruti au vitetemeshi vilivyounganishwa kwenye malori ya pekee. Mawimbi yanayotokezwa hufika kwenye tabaka la juu la dunia na kurudishwa kwenye vifaa vinavyopima mawimbi hayo, navyo vinawasaidia wanasayansi kuona kwa kutumia kompyuta jinsi miamba ilivyofanyizwa. Picha wanazopata zinawasaidia kutambua mahali ambapo kuna hifadhi za gesi.
Gesi inapotafutwa baharini, mawimbi hutokezwa na bunduki za pekee zinazorusha hewa, mvuke, au maji ndani ya bahari. Shinikizo linalotokezwa huingia kwenye sakafu ya bahari na kurudishwa kupitia vifaa vya kunasa mawimbi ya sauti
chini ya maji vilivyounganishwa kwenye waya mrefu uliounganishwa upande wa nyuma wa meli ya kufanyia uchunguzi. Watafiti wanachunguza habari hizo na kufanyiza picha kupitia kompyuta.Kabla ya pesa za kuchimbua gesi zitolewe, lazima ithibitishwe kwamba eneo fulani lina gesi ya kutosha. Kwa hiyo, wanajiolojia lazima wahakikishe kwamba kuna shinikizo na kiasi cha kutosha cha gesi ndani ya hifadhi. Shinikizo hilo linaweza kupimwa kwa usahihi kwa kutumia geji. Hata hivyo, ni vigumu zaidi kupima kiasi cha gesi. Njia moja ni kupima shinikizo mara ya kwanza, kuachilia kiasi fulani cha gesi, kisha kuipima kwa mara ya pili. Ikiwa shinikizo hilo litashuka kidogo itaonyesha kuwa kuna gesi nyingi hapo; likishuka sana, itaonyesha kuna gesi kidogo.
Kutayarisha Gesi kwa Ajili ya Matumizi
Baada ya kutolewa, gesi ya asili husafirishwa kwa mabomba hadi kwenye vituo vya kusafishia ili kemikali zisizohitajika ziondolewe, kama vile kaboni dioksidi, hidrojeni salfaidi, kutia ndani mvuke, unaoweza kufanya mabomba yawe na kutu. Gesi ya asili hugeuzwa kuwa umajimaji katika viwango vya chini kabisa vya joto ili kuondoa nitrojeni inayoweza kushika moto na kutenganisha heli, butani, ethani, na propani. Mwishowe kinachotokezwa ni methani safi, ambayo ni gesi isiyo na rangi, harufu, na inaweza kushika moto upesi. Kwa sababu methani inatokezwa kwa njia ya asili, inaitwa gesi ya asili.
Ili gesi ya asili iweze kutumiwa nyumbani, watengenezaji huongeza kiasi kidogo cha vitu vyenye salfa vilivyo na harufu kali ili inapoanza kuvuja itambulike kwa urahisi na kuzuiwa kabla ya mlipuko kutokea. Isitoshe, gesi ya asili ni safi zaidi kuliko nishati nyingine za asili, kama vile makaa ya mawe na mafuta.
Ili gesi isafirishwe kwa urahisi, gesi fulani ya asili hugandishwa kwa viwango vya chini sana vya joto na kugeuzwa kuwa majimaji. Kwa kawaida, butani na propani hufanywa kuwa gesi majimaji ya petroli (LPG), ambayo hutumiwa na watu kupikia. LPG hutumiwa pia kama nishati ya kuendesha mabasi, matrekta, malori, na magari mengine. Butani na propani zimetumika kutokeza vitu vya kemikali kama vile plastiki, viyeyushaji, nyuzi zilizotengenezwa viwandani, na vitu vingine.
Nishati Inayoweza Kwisha
Kama tu nishati zote za asili, gesi ya asili inaweza kwisha. Kulingana na makadirio, ni asilimia 45 hivi tu ya gesi ambayo haijagunduliwa. Iwapo makadirio hayo ni sahihi basi huenda gesi hiyo ikatosha mahitaji ya miaka 60 tu kwa kulinganisha kiwango kinachotumika leo. Lakini katika nchi nyingi, utumizi wa nishati unaongezeka, kwa hiyo huenda makadirio ya sasa yasiwe sahihi.
Kwa kweli, njia ambayo nchi fulani zinajitahidi kujiimarisha kiviwanda inaweza kumfanya mtu afikiri kwamba mali za asili za dunia haziwezi kwisha. Ni kweli kwamba kuna nishati inayotokezwa na nyuklia, na pia jua na upepo. Lakini je, vyanzo hivyo vitatosheleza uhitaji wa nishati unaozidi kuongezeka? Na je, vitatumika bila kudhuru mazingira? Tutajua kadiri wakati unavyopita.
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Baada ya kuchimbuliwa, gesi ya asili husafirishwa kwa mabomba hadi kwenye kituo cha kusafishia ambako inashughulikiwa na kusambazwa kwenye nyumba na sehemu za biashara
[Mchoro]
Kisima cha gesi
Kituo cha kusafishia
Kampuni ya gesi
[Picha katika ukurasa wa 13]
Vifaa maalumu hutumiwa kutokeza mawimbi ya sauti yanayorudishwa kwenye mashini za kupima
[Picha katika ukurasa wa 13]
Wanajiolojia wanachunguza picha zilizotokezwa na mawimbi ya sauti
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]
Top: © Lloyd Sutton/Alamy; bottom: © Chris Pearsall/Alamy