Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jicho la Nondo

Jicho la Nondo

 Je, Ni Kazi ya Ubuni?

Jicho la Nondo

● Nondo wengi huruka hasa usiku. Ingawa viumbe fulani wanaotembea usiku huonekana macho yao yanapong’aa kwa sababu ya kumulikwa na nuru, macho ya nondo hayang’ai kwa kuwa konea yake haing’ai inapomulikwa.

Fikiria hili: Jicho la nondo lina konea ya ajabu. Imefanyizwa kwa vinundu vidogo sana vilivyopangwa katika maumbo yenye pembe sita. Vinundu hivyo “ni vidogo kuliko mawimbi ya nuru,” anasema Peng Jiang, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Florida, Marekani. Maumbo na ukubwa wa vinundu hivyo huwezesha jicho la nondo kunasa nuru kutoka kwenye mawimbi na kutoka pembe mbalimbali. Vinundu hivyo vidogo vina kimo cha nanomita 200 hadi 300. Kwa kulinganisha, inakadiriwa kwamba upana wa unywele wa mwanadamu ni nanomita 80,000 hivi!

Mainjinia wanatarajia kwamba kuelewa konea ya nondo vizuri zaidi kutawasaidia kuboresha ubuni wa balbu zinazotumika sehemu mbalimbali kama vile katika mabango ya matangazo. Ubuni wa jicho la nondo unaweza pia kutumiwa katika kunasa nishati ya jua. Vifaa vya silikoni vinavyotumiwa sasa kunasa nishati ya jua vinaweza kupoteza asilimia 35 ya nuru. Hata hivyo, kwa kufuata ubuni wa vinundu vya jicho la nondo, Jiang na wataalamu wenzake walitokeza kifaa cha silikoni kilichopoteza asilimia 3 tu ya nuru. “Tunaweza kujifunza mambo mengi sana kutokana na vitu hivyo vya asili,” anasema Jiang.

Una maoni gani? Je, konea ya jicho la nondo isiyong’aa inapomulikwa ilijitokeza yenyewe? Au ilibuniwa?

[Picha katika ukurasa wa 30]

Jicho la nondo lina konea ya ajabu ambayo imefanyizwa kwa vinundu vidogo sana vilivyopangwa katika maumbo yenye pembe sita

[Picha katika ukurasa wa 30]

Kifaa cha silikoni kisichopoteza nuru nyingi kinachotumiwa kunasa nishati ya jua

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]

Moth eye close-up: Courtesy of Dartmouth Electron Microscope Facility; silicon close-up: Courtesy Peng Jiang