Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utawala wa Malkia Elizabeth wa Kwanza—Ulikuwa Wenye Ufanisi?

Utawala wa Malkia Elizabeth wa Kwanza—Ulikuwa Wenye Ufanisi?

 Utawala wa Malkia Elizabeth wa Kwanza—Ulikuwa Wenye Ufanisi?

ALIKUWA mashuhuri sana katika enzi zake. Waandishi wa vitabu, washairi, waandikaji wa michezo ya kuigiza, na watengenezaji wa filamu wa kisasa wameendeleza umashuhuri wake. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na vitabu na maonyesho mengi kumhusu. Kura ya maoni iliyofanywa ulimwenguni pote ilionyesha kwamba alionwa kuwa miongoni mwa watu kumi mashuhuri zaidi nchini Uingereza. Huyo ni nani? Ni Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza.

Kwa nini mtawala huyo aliyejulikana kama Malkia Bikira na Malkia Mwema Bess ambalo ni ufupisho wa jina Elizabeth, aliwasisimua watu kwa muda mrefu? Je, kweli utawala wake ulikuwa wenye ufanisi?

Anarithi Matatizo Mengi

Elizabeth Tudor alizaliwa mwaka wa 1533, na baba yake, Mfalme Henry wa Nane hakufurahia kuzaliwa kwake kwani alitaka sana mrithi wa kiume. Mama ya Elizabeth, Anne Boleyn, ambaye alikuwa mke wa pili wa Henry, alikosa kumzalia mtoto wa kiume. Henry aliamuru akatwe kichwa kwa kile ambacho wengi walitaja kuwa mashtaka ya uwongo. Wakati huo Elizabeth alikuwa na umri wa miaka miwili tu.

Kufikia wakati huo, Henry alikuwa amevunja uhusiano wowote na papa huko Roma na akajitawaza kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikana. Henry alipokufa mwaka wa 1547, washauri wa kidini wa mwana wake, Edward wa Sita, walijaribu kufanya Uingereza iwe nchi ya Kiprotestanti. Edward alikufa baada ya kutawala kwa miaka sita tu, na taifa hilo likageukia tena Ukatoliki wakati wa utawala mfupi uliojaa umwagaji wa damu wa Mary wa Kwanza, ambaye alikuwa dada wa kambo wa Elizabeth. * Elizabeth alipoanza kutawala mwaka wa 1558 akiwa na umri wa miaka 25, Uingereza ilikuwa imefilisika na ilikumbwa na mizozo ya kidini. Ilikuwa imepoteza maeneo ya Ufaransa yaliyokuwa chini ya utawala wake na Hispania ilikuwa tisho kubwa.

Alipoanza kutawala, Elizabeth alitafuta washauri wanaofaa, na baadhi yao walikuwa naye kwa karibu kipindi chote cha miaka 44 cha utawala wake. Tatizo la kwanza aliloshughulikia ni dini. Kama inavyosemwa kwenye Tovuti ya Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Vyombo vya Baharini, malkia huyo alichagua “kurudisha yale Marekebisho ya Kidini na kujenga Kanisa Anglikana ambalo halikuwa la Kikatoliki wala la Kiprotestanti.” Badala ya kuwa kiongozi mkuu, alikuwa gavana mkuu ili kuwatuliza watu ambao hawangekubali mwanamke awe kiongozi wa kanisa. Kisha, bunge likapitisha Sheria ya Ufanano ambayo ilianzisha mafundisho na mazoea ya Kanisa Anglikana, ingawa bado walifuata sherehe fulani za Kikatoliki. Msimamo huo wa kutounga mkono upande wowote haukuwapendeza Wakatoliki wengi au Waprotestanti sugu walioitwa Wapuriti.

Elizabeth alikabili tatizo lingine. Angepataje ushikamanifu na heshima kutoka kwa taifa ambalo bado lilikuwa likiteseka kutokana na matokeo ya utawala mbaya wa Mary wa Kwanza? Aliamua kutumia jinsia yake vizuri. Mwanahistoria  Christopher Haigh anaeleza hivi: “Akikalia kiti cha Ufalme, Elizabeth alionekana kuwa Malkia Bikira; Kanisa lilimwona kuwa mama, wakuu walimwona kuwa shangazi, madiwani wake, walimwona kuwa mke mwenye chokochoko, na kwa watumishi wake, alikuwa mwanamke aliye na ulimi mtamu.” Lengo lake kuu lilikuwa kuwasadikisha raia zake kwamba anawapenda. Nao raia walimpenda.

Bunge lilitaka sana Elizabeth aolewe na kuwa na mrithi Mprotestanti. Wanaume mmojammoja wa familia za kifalme walikuja kumposa. Elizabeth angejifanya kuwa anapendezwa nao na kufanya mapatano ya ndoa yachukue miezi au hata miaka kadhaa na kisha akatae posa yao wakati ambapo angepata faida ya kisiasa.

Kwa kuwa Elizabeth hakujihusisha sana na dini, njama nyingi zilipangwa dhidi yake. Tisho kuu lilitoka kwa binamu yake Mkatoliki, Mary Stuart, ambaye nchi za Kikatoliki huko Ulaya zilimwona kuwa mrithi halali wa Mary wa Kwanza. Tisho hilo lilizidi mwaka wa 1568 Mary alipolazimika kung’atuka mamlakani huko Scotland na kukimbilia Uingereza. Ingawa alipewa kifungo cha nyumbani, punde si punde Wakatoliki walipanga njama ya kumtumia kumwondoa malkia Mprotestanti mamlakani, lakini Elizabeth alikataa katakata kumwua mtawala mwenzake. Mnamo 1570, Papa Pius wa Tano alitoa amri ya kumtenga Elizabeth na kuwaweka huru raia zake wasimtii. Papa aliyefuata, Gregory wa Kumi na Tatu alipanua amri hiyo kwa kutangaza kwamba haingekuwa dhambi kuishambulia Uingereza na kumwondoa kwa nguvu malkia kutoka mamlakani. Elizabeth alilazimika kuchukua hatua wakati njama ya Anthony Babington ya kumwua Elizabeth ilipogunduliwa ambayo Mary alihusishwa nayo. Mwishowe ilibidi Elizabeth afanye uamuzi kumhusu Mary, na kwa kushinikizwa na bunge, hatimaye aliamuru Mary auawe mwaka wa 1587. Nchi za Kikatoliki barani Ulaya zilikasirishwa sana na hilo, hasa Mfalme Philip wa Pili wa Hispania.

Mbinu Jasiri ya Philip

Philip, ambaye wakati huo ndiye aliyekuwa mtawala mwenye nguvu zaidi Ulaya, alijaribu kufanya Uingereza iwe nchi ya Kikatoliki kwa kumposa Elizabeth alipokuwa malkia, lakini Elizabeth akakataa. Kwa miaka mingi, maharamia wa Uingereza walikuwa wakipora meli na bandari za Hispania na kuingilia maeneo ambayo yalikuwa chini ya udhibiti wake wa kikoloni. Pia Philip aliudhika sana Elizabeth alipounga mkono jitihada za Uholanzi za kupigania uhuru dhidi ya utawala wa Hispania. Kuuawa kwa Mary kulimfanya Philip kuchukua hatua. Akichochewa na papa, Philip alipanga kutumia manowari zaidi ya 130 za Hispania. Manowari hizo zingesafiri hadi Uholanzi na kuchukua jeshi kubwa la wanajeshi wa nchi kavu na kisha kuvuka Mlango-Bahari wa Uingereza na kushambulia Uingereza. Kabla ya manowari hizo kukusanywa pamoja, wapelelezi wa Uingereza waligundua njama hiyo. Elizabeth alimtuma Sir Francis Drake akiwa na meli 30 kwenye bandari ya Hispania ya Cádiz, ambapo waliharibu manowari kadhaa za Hispania na hivyo kuchelewesha shambulio la manowari za Hispania kwa mwaka mmoja.

Hatimaye manowari za Hispania zilipoondoka bandarini mnamo 1588, jeshi la majini la Uingereza lilikuwa tayari. Licha ya kushambuliwa, manowari za Hispania zilifika kwenye Mlango-Bahari  wa Uingereza bila kuharibiwa sana na zikatia nanga kwenye bandari ya Calais huko Ufaransa. Usiku uliofuata, Waingereza walituma meli nane zilizojaa mabomu na vitu vinavyoweza kulipuka. Kwa woga, meli za Hispania zilitawanyika, na baada ya mapigano makali, upepo uliovuma kutoka kusini-magharibi ulizisukuma meli hizo kutoka Uingereza hadi Scotland iliyokuwa upande wa kaskazini. Dhoruba huko Scotland na kutoka pwani ya magharibi ya Ireland iliharibu nusu ya meli za Hispania, na zile zilizobaki zilijikokota na kurudi Hispania.

Utawala Wenye Ufanisi Waanza

Elizabeth alipoanza kutawala, Uingereza haikuwa ikimiliki maeneo yoyote ng’ambo. Tofauti na hilo, Hispania ilikuwa ikipata mali nyingi kutoka kwa maeneo yake mengi huko Amerika ya Kaskazini, ya Kati, na ya Kusini. Uingereza pia ilitaka kumiliki baadhi ya maeneo hayo. Kwa hiyo, wafanyabiashara wajasiri walisafiri baharini wakitafuta umashuhuri, mali, na njia mpya ambazo zingetumiwa na wafanyabiashara kwenda China na Mashariki ya Mbali. Sir Francis Drake akawa nahodha wa kwanza kuendesha meli yake mwenyewe kuzunguka ulimwengu, akipora meli za Hispania zenye hazina akielekea pwani ya magharibi ya Amerika ya Kusini na Kaskazini. Ili kuzuia udhibiti wa Hispania wa maeneo hayo, Sir Walter Raleigh alianzisha mpango wa kutafuta koloni huko Pwani ya Mashariki ya Amerika Kaskazini. Aliliita eneo alilotwaa, Virginia, kwa heshima ya Malkia Bikira wa Uingereza. Ingawa jitihada za kufanya maeneo ya Amerika ya Kusini na Kaskazini kuwa koloni hazikufanikiwa, zilifanya Uingereza ianze kupendezwa na maeneo hayo. Wakati manowari zenye nguvu za Hispania ziliposhindwa, Uingereza ikawa ndiyo nchi yenye meli nyingi ulimwenguni na Elizabeth aliunga mkono mipango mipya ya kufanya biashara na nchi za kusini-mashariki ya Asia. Msingi ulikuwa umewekwa kwa ajili ya Milki ya Uingereza ambayo ingeenea duniani pote. *

Huko Uingereza, elimu ilikaziwa sana. Shule mpya zilifunguliwa na hilo liliwapa nafsi wanafunzi wengi kujifunza kusoma na kuandika. Hamu ya kusoma pamoja na maendeleo katika uchapishaji ulitokeza wasomi wengi. Hicho kilikuwa kipindi cha William Shakespeare na waandishi wengine mashuhuri wa michezo ya kuigiza. Watu wengi walifurika kwenye majumba mapya ya maonyesho ili kutazama michezo ya kuigiza. Washairi waliandika mashairi kwa ustadi na watungaji walitunga nyimbo mpya. Wasanii stadi walichora picha ndogo za malkia na watumishi wake. Tafsiri mpya za Biblia ziliwekwa kanisani na nyumbani. Lakini utawala huo wenye ufanisi haukudumu.

Miaka ya Mwisho ya Utawala wa Elizabeth

Miaka ya mwishomwisho ya utawala wa Elizabeth ilijaa matatizo chungu nzima. Kwa kuwa aliishi muda mrefu zaidi kuliko washauri wake, aliwapa watu wachache aliowachagua mapendeleo na hilo lilizusha fujo kati ya watumishi wake na kulikuwa na jaribio la kumpindua ambalo halikufanikiwa. Kwa mara nyingine tena, ufalme wake uligawanyika kidini. Wakatoliki walikataa kuhudhuria ibada ya Waprotestanti, nao waliteswa vikali. Kufikia mwisho wa utawala wake, watu 200 hivi kutia ndani makasisi na watu wa kawaida walikuwa  wameuawa. Wapuriti walifungwa gerezani na wakauawa pia. Uasi dhidi ya utawala wa Uingereza ulitokea huko Ireland, na vita kati ya Uingereza na Hispania viliendelea. Misimu minne ya mavuno mabaya yalisababisha ukosefu wa kazi na uhalifu, na watu walifanya vurugu kwa sababu ya bei ya juu ya chakula. Umashuhuri wa Elizabeth ulikuwa umepungua. Waingereza hawakumpenda tena Malkia Bikira wao.

Mwishowe Elizabeth alikata tamaa ya kuishi na akiwa mtawala wa mwisho wa ukoo wa Tudor, alikufa Machi 24, 1603. Watu walishtuka walipopata habari za kifo chake, lakini kufikia jioni hiyo walikuwa wakisherehekea kwa mioto mikubwa na karamu barabarani kutawazwa kwa mtawala mpya. Hatimaye walikuwa na mfalme—James wa Sita wa Scotland, ambaye alikuwa Mprotestanti na mwana wa Mary Stuart. Mtawala huyo ambaye aliitwa James wa Kwanza wa Uingereza, alitimiza kile ambacho Elizabeth alishindwa kutimiza—aliunganisha falme hizo mbili chini ya mtawala mmoja. Hata hivyo, matumaini ambayo watu walikuwa nayo yalididimia upesi na wakaanza kutamani utawala wa Malkia Mwema Bess.

Je, Kweli Utawala Wake Ulikuwa Wenye Ufanisi?

Wanahistoria wa kale walimsifu sana Elizabeth. Miaka michache baada ya kifo chake, William Camden alisema kwamba utawala wake ulikuwa wenye ufanisi na maendeleo, na malkia aliwachochea raia zake watimize mambo makuu. Kwa muda mrefu, hakuna mtu yeyote aliyetilia shaka maoni hayo. Elizabeth alizidi kupata umashuhuri mwishoni mwa karne ya 19 alipotajwa kuwa mwanzilishi wa Milki ya Uingereza, ambayo wakati huo ilikuwa imeenea robo ya dunia.

Wanahistoria fulani wa kisasa hawauoni utawala wa Elizabeth kuwa wenye ufanisi. Kitabu The Oxford Illustrated History of Britain kinasema hivi: “Sifa ambazo Elizabeth alipata baada ya kifo chake zilitiliwa chumvi zinapolinganishwa na mambo ambayo alitimiza. Propaganda zake, . . . kuishi kwake muda mrefu, kutawala kwake wakati ambapo Uingereza ilikuwa na wasomi wengi kama vile Shakespeare, na ushindi dhidi ya manowari za Hispania, kumetufumba macho tumsifu na kupuuza kwamba alifanya Uingereza izorote na kuwa nchi isiyoweza kutawalika.” Haigh, ambaye alinukuliwa hapo awali, anaeleza ni kwa nini wanahistoria fulani walitoa maoni hayo: “Mnamo 1603, Elizabeth alionekana kuwa bi-kizee mpumbavu, kwa kuwa wanaume walitaka mfalme wa ukoo wa Stuart. Kufikia 1630, wakati ambapo wafalme wa ukoo wa Stuart waliwakatisha tamaa, watu walianza kumwona Elizabeth kuwa mtawala anayefaa badala ya wafalme hao wa ukoo wa Stuart.”

Hakuna shaka kwamba Elizabeth alikuwa mwanamke wa pekee katika ulimwengu uliotawaliwa na wanaume. Elizabeth alikuwa na uhusiano mzuri na watu kwa sababu alikuwa mwenye akili na thabiti, na alisaidiwa na mawaziri wake ambao waliandika kwa ustadi hotuba zake, wakapanga ziara zake, wakamchagulia mavazi, na picha alizopigwa ili kuendeleza utawala wake na ufanisi uliotokea kwa sababu ya utawala huo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Ona makala “Sasa Wakiri Kutovumiliana Kidini,” katika Amkeni! la Aprili 8, 2000 (8/4/2000), ukurasa wa 12-14.

[Blabu katika ukurasa wa 22]

“Sifa ambazo Elizabeth alipata baada ya kifo chake zilitiliwa chumvi zinapolinganishwa na mambo ambayo alitimiza”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 22]

JOHN DEE NA MILKI YA UINGEREZA

  Elizabeth alimwita John Dee (1527-1608/9) mwanafalsafa wake. John Dee alikuwa mwanahisabati, mwanajiografia, na mwastronomia mwenye kuheshimika, ambaye pia alijihusisha na unajimu na uchawi. Alimshauri malkia kuhusu siku iliyofaa zaidi kutawazwa kwake na alifanya ufundi wake wa kiuchawi katika jumba la malkia. Inasemekana kuwa yeye ndiye aliyetunga usemi “Milki ya Uingereza,” naye alimchochea Elizabeth ajione kuwa malkia wa milki ya wakati ujao ambayo ingeanzishwa kwa kudhibiti bahari na kufanya maeneo mapya kuwa koloni zake. Ili kutimiza hilo, aliwafunza wavumbuzi kuhusu usafiri wa baharini, hasa jinsi ya kutafuta njia ya Kaskazini-Mashariki na Kaskazini-Magharibi kuelekea nchi za Mashariki, na aliunga mkono mipango ya kufanya bara la Amerika Kaskazini kuwa koloni ya Uingereza.

[Hisani]

Photograph taken by courtesy of the British Museum

[Picha katika ukurasa wa 20, 21]

A. Meli zilizojaa mabomu na vitu vinavyoweza kulipuka zilitumwa kushambulia manowari za Hispania B. Sir Francis Drake C. Malkia Elizabeth D. Jumba la Michezo ya Kuigiza la Globe E. William Shakespeare

[Hisani]

A: From the book The History of Protestantism (Vol. III); B: ORONOZ; C: From the book Heroes of the Reformation; D: From the book The Comprehensive History of England (Vol. II); E: Encyclopædia Britannica/11th Edition (1911)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

© The Bridgeman Art Library International