Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kukuza Okidi—Jinsi Subira Huvuta Heri

Kukuza Okidi—Jinsi Subira Huvuta Heri

 Kukuza Okidi—Jinsi Subira Huvuta Heri

MTU anaweza kuwa mraibu wa kukuza okidi. Watu fulani wanaopenda okidi hutumia saa nyingi sana wakijifunza majina ya Kilatini ya okidi wanazopenda ili waweze kuyatamka kwa njia inayofaa. Kwa nini watu wanavutiwa sana na okidi?

Kuna okidi nyingi na za aina mbalimbali. Aina 25,000 hivi zimegunduliwa mwituni na mashirika fulani yanayoshughulika na mimea husema kuna zaidi ya okidi 100,000 zilizotokezwa na wanadamu! Kusema eti ‘zimetokezwa na wanadamu’ hakumaanishi eti wataalamu wa maua wameumba maua mapya kutokana na udongo, maji, na hewa. Badala yake, maua hayo huchavushwa kimakusudi na wanadamu.

Okidi za mwituni na zile zinazochavushwa na wanadamu zina ukubwa mbalimbali. Kuna okidi ndogo sana ambazo mtu anaweza kuziona vizuri kwa kutumia kioo cha kuongeza ukubwa, na nyingine ni kubwa hivi kwamba zinaweza kukuzwa ndani ya chungu na kuweka kando ya dirisha. Okidi moja inayokua katika msitu wa mvua wa Indonesia inaweza kuwa na uzito wa zaidi ya kilogramu 500!

Okidi huwa za rangi na maumbo mbalimbali. Nyingine hufanana sana na nyuki, nondo, au ndege, na nyingine zilizo na maumbo ambayo hujawahi kuona tena zinavutia sana, na hasa zinawavutia wakuzaji. Kwa miaka mingi, ni matajiri tu walioweza kuwa na mimea hii maridadi, lakini sasa hata wasio matajiri wanaweza kupata okidi. Soma kuhusu okidi hizo maridadi.

Wanaokuza Okidi Waongezeka Sana

Kwa karne nyingi, watu wamependezwa na okidi lakini ni katika miaka ya hivi karibuni tu ndipo wakuzaji wamejifunza njia zinazofaa za kuzizalisha. Okidi iliyochavushwa na wanadamu ilichanua maua kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1856. Hata hivyo, badala ya kufurahisha, mara nyingi watu walichoshwa na kazi ya kukuza maua hayo yenye kuvutia lakini yanayohitaji utunzaji wa hali ya juu.

Mbegu za okidi ni ndogo—nyingine ni ndogo kama vumbi. Ilikuwa vigumu sana kutunza mbegu hizo ndogo, na bado ni vigumu kufanya  hivyo, lakini tatizo kubwa ni kuzifanya zikue. Kwa makumi ya miaka, wakuzaji walijaribu vifaa na hali tofauti-tofauti ili watambue ni chini ya hali gani mbegu za okidi zinaweza kuchipuka. Mnamo 1922, Dakt. Lewis Knudson, mwanasayansi katika Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani, aligundua kwamba mbegu zinapotiwa katika mchanganyiko wa maji, sukari, na agaa (umajimaji fulani kama jeli unaotolewa kwenye magugu-maji), mbegu hizo zilichipuka na kukua vizuri. Baada ya muda mfupi, watu wengi walikuwa wakitokeza okidi kwa wingi. Bado watu wengi wanapenda kukuza okidi na sasa kuna aina nyingi za okidi zinazochavushwa na wanadamu kila mwaka ambazo hatujapata kuona.

Lakini muda mrefu kabla ya wanadamu kuzikuza, okidi zilikua mwituni. Aina mpya za okidi hutokezwaje katika mazingira yake ya asili?

Okidi za Mwituni

Okidi mbili au zaidi za jamii yenye uhusiano wa karibu zinapokuwa katika eneo moja, kuna uwezekano mkubwa kwamba zitatokeza aina mpya ya kiasili. Huko mwituni, wadudu na viumbe wengine ndio wachavushaji. Wanapotafuta nekta kwenye okidi, chavua kutoka kwenye mmea mmoja hukwama mwilini na kuchavusha mimea watakayogusa baada ya hapo. Kwa sababu hiyo, okidi hizo zilizochavushwa hutungishwa. Kwa sababu hiyo, zinatokeza maganda ya mbegu.

Baada ya muda, maganda hayo hukomaa, yanapasuka, na kumwaga maelfu, huenda hata mamilioni ya mbegu. Mbegu hizo huanguka chini, nyingine nyingi hubebwa na upepo. Ni vigumu sana kwa mbegu hizo kuendelea kukua na chache sana hukomaa. Mbali na okidi zinazotokea kiasili mwituni, wanadamu wametokeza aina mpya za okidi. Wamefanya hivyo jinsi gani?

Jinsi Okidi Huchavushwa

Okidi ya aina mpya huwa na sifa kutoka kwa kila okidi iliyoifanyiza. Kwa sababu hiyo,  yule anayeikuza huamua kwanza ni ua la aina gani analotaka kutokeza. Huenda akawa anataka ua lenye rangi au mistari au madoadoa fulani. Huenda akawa anataka kuunganisha sifa hizo katika mmea wenye maua madogo au makubwa. Huenda pia akawa anataka ua lenye harufu fulani. Akiwa na mambo hayo akilini, mpandaji hutafuta okidi mbili ambazo zitatokeza okidi nyingine yenye sifa hizo anazotaka. Kwa mfano, mkuzaji okidi anaweza kuchagua kutumia okidi inayoitwa golden slipper (Paphiopedilum armeniacum). Okidi hiyo iligunduliwa huko China mnamo 1979. Mara nyingi okidi iliyochavushwa na okidi hiyo hutokeza maua yenye rangi ya manjano, na baadhi yake ni maridadi ajabu.

Mpandaji anapopata mimea miwili ambayo atatumia, anatoa chavua yote kutoka kwenye okidi yenye ganda la mbegu ambayo itatiwa chavua. Kisha akitumia kijiti kidogo au kitu kama hicho, mpandaji anatoa chavua kutoka kwenye okidi yenye mbegu na kuzipaka kwenye shina la okidi yenye ganda la mbegu. Anabandika majina ya okidi alizotumia kuchavusha okidi hiyo pamoja na tarehe yake.

Lazima Uwe na Subira

Ikiwa okidi hiyo itatungishwa, jambo fulani la ajabu hutukia katika ua lenye ganda la mbegu. Ua hilo hutokeza mirija kama nyuzi ambayo ni sehemu ya ua inayoitwa ovari. Ovari hiyo hupanuka na kufanyiza ganda la mbegu. Humo ndani, mamia ya maelfu ya mbegu ndogo sana hufanyizwa, kila moja ikiwa imeunganishwa na mrija mmoja wa chavua. Inaweza kuchukua miezi kadhaa au zaidi ya mwaka ili ganda la mbegu liive. Wakati huo, mpandaji hukusanya mbegu hizo kutoka kwenye ganda la mbegu. Anazitia ndani ya chupa iliyosafishwa vizuri iliyo na agaa na virutubisho. Mbegu hizo zinapoota, okidi ndogondogo sana zitatokea kama nyasi.

Baada ya miezi michache, mpandaji anatoa miche hiyo kutoka kwenye chupa na kuipanda karibu-karibu ndani ya chungu kikubwa. Anatunza sana miche hiyo, akiimwagilia maji mara nyingi ili isikauke. Baada ya muda, mpandaji hupanda okidi hizo kwenye chungu kimoja-kimoja. Wakati huu ndipo anapohitaji kuwa na subira sana. Okidi zinaweza kuchukua miaka kadhaa au zaidi ya miaka kumi kuchanua maua.

Wazia furaha ya mpandaji anapoona okidi aliyokuza ikichanua! Ikiwa okidi iliyokua ni ya aina mpya kabisa, mpandaji anaweza kuipa jina analotaka. Okidi zote zitakazokuzwa kutoka kwa okidi hiyo zitaitwa kwa jina hilo.

Nyakati nyingine, mpandaji hutokeza okidi ambayo huwasisimua watu wanaopenda kukuza okidi. Anaweza kupewa tuzo nyingi, na mimea hiyo maridadi itauzwa kwa bei ghali sana. Lakini hata ikiwa atapata pesa nyingi kadiri gani, jambo lenye kufurahisha zaidi kwa mpandaji ni kuona okidi alizochavusha zikichanua.

Kwa hiyo, sasa unajua kwamba ilichukua wakati na subira nyingi kutokeza okidi maridadi unazopenda. Lakini kwa kweli, kazi ambayo wanadamu hufanya kutokeza okidi ni rahisi ikilinganishwa na kazi ya Muumba mkuu wa kila kitu kilicho hai, Yehova. Chembe za urithi ambazo ametia ndani ya kila mmea hufanya ichanue maua yenye kupendeza sana. Sisi ni watazamaji tu wa upendo wake ambao unaonekena katika okidi mbalimbali maridadi zenye kupendeza. Maneno ambayo mtunga-zaburi Daudi alisema ni ya kweli: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”—Zaburi 104:24.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Okidi ya “Beallara”

[Picha katika ukurasa wa 17]

Okidi ya “Doritaenopsis”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Okidi ya “Brassidium”