Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wanyama Wakubwa wa Baharini

Wanyama Wakubwa wa Baharini

 Wanyama Wakubwa wa Baharini

Mnyama mkubwa anaibuka kutoka baharini, ananyakua mashua nzima, na kuivuta pamoja na mabaharia chini ya maji. Hadithi kama hizo zimesimuliwa kwa miaka mingi sana. Lakini je, wanyama hao wakubwa ni halisi?

MNAMO 2007 ngisi anayeitwa colossal alishikwa bila kukusudia na wavuvi katika Bahari ya Ross karibu na Antaktika. Alikuwa na urefu wa mita 10 hivi, kutia na minyiri yake, na alikuwa na uzito wa karibu kilogramu 500! Wanasayansi wanaamini kwamba aina hiyo ya ngisi wanaweza kuwa wakubwa hata zaidi.

Mnyama mwingine mkubwa kama huyo anaitwa ngisi-jitu ambaye ana mwili wenye umbo la kombora, macho yenye ukubwa wa kichwa cha mwanadamu, mdomo kama wa kasuku wenye nguvu za kukata nyaya za chuma, mikono minane yenye mashimo ya kufyonza, na minyiri miwili mirefu ya kuvuta chakula hadi mdomoni. Akiwa majini anaweza kusonga kwa mwendo wa kilomita 30 kwa saa, na hata anaweza kujirusha hewani!

Katika karne iliyopita inasemekana kwamba wanyama hao wakubwa walionekana  mara zisizozidi 50, na hawajawahi kufanyiwa uchunguzi wakiwa baharini.

Nyangumi Wakubwa wa Baharini

Hata hivyo, ngisi-jitu na yule anayeitwa colossal ni chakula cha mnyama mwingine mkubwa zaidi, yule nyangumi anayeitwa sperm, anayeweza kukua kufikia urefu wa mita 20 hivi na uzito wa tani 50. Jino lake moja lina uzito wa gramu 900! Nyangumi wa aina hiyo wamepatikana wakiwa wamekufa wakiwa na visehemu vya ngisi-jitu tumboni. Nyangumi hao walikuwa na majeraha ya mviringo yaliyosababishwa na mashimo ya kufyonza ya ngisi huyo, kuonyesha kwamba alipigana kwa ujasiri kabla ya kuliwa. Mnamo 1965, kikundi cha wavuvi wa nyangumi kutoka Sovieti alidai kuwa alijionea vita kati ya ngisi-jitu na nyangumi huyo mwenye uzito wa tani 40. Hakuna aliyepona katika vita hivyo. Nyangumi aliyenyongwa alipatikana akielea baharini akiwa na kichwa cha ngisi huyo tumboni mwake.

Ingawa ngisi-jitu na nyangumi huyo anayeitwa sperm ni wakubwa sana, nyangumi wa rangi ya bluu-kijivu, ambaye ndiye mnyama mkubwa zaidi kati ya wanyama wanaonyonyesha, anawazidi kwa ukubwa. Nyangumi wa kike wa aina hiyo mwenye urefu wa mita 33 aliyevuliwa huko Antaktika ndiye nyangumi mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa. Nyangumi wa rangi ya bluu-kijivu anaweza kuwa na uzito wa tani 150 hivi. Uzito wa ulimi wake peke yake ni sawa na uzito wa tembo aliyekomaa! Hebu wazia—nyangumi huyo huzaa mtoto mwenye uzito wa tani tatu na urefu wa mita 7 hadi 8! Kwa sababu ya kuvuliwa sana na wavuvi wa nyangumi, nyangumi huyo karibu atoweke katika miaka ya 1960 na leo amewekwa katika orodha ya wanyama walio katika hatari kubwa ya kutoweka.

Wanyama Wakali na Wapole

Kwa sababu ya meno yake 3,000, huenda papa mweupe akawa ndiye samaki mla nyama mwenye kutisha zaidi. Papa mweupe mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa alikuwa na urefu wa mita 7 na uzito wa kilogramu 3,200. Papa huyo ana uwezo mkubwa ajabu wa kunusa, kwani anaweza kunusa tone moja tu la damu linapochanganywa katika maji ya lita 100!

Samaki mkubwa zaidi ni papa nyangumi mwenye urefu wa mita 7.5 hivi. Hata hivyo, wengine wanaweza kuwa na urefu mara mbili ya huo. Mdomo wake unaweza kupanuka kwa mita 1.4 na hivyo anaweza kummeza mwanadamu kwa urahisi. Lakini badala ya kuwa mwindaji hatari wa wanyama wengine wakubwa wa baharini, samaki huyu mkubwa hula mimea ya baharini na samaki wadogo.

Likizungumza kuhusu simulizi la Biblia la nabii Yona aliyemezwa na samaki mkubwa, gazeti National Geographic lilisema kwamba “umeng’enyaji wa ajabu  wa papa nyangumi hufanya tuamini hadithi kama ile ya Yona.” Papa nyangumi “huondoa tumboni kwa njia isiyodhuru vitu vikubwa wanavyomeza ambavyo haviwezi kumeng’enywa.”—Yona 1:17; 2:10.

Jitu Linalopenda Kujificha

Kiumbe mwingine mkubwa wa baharini ni pweza mkubwa, ambaye anaweza kukua na kufikia uzito wa kilogramu 250 hivi. Wakati mmoja aliitwa samaki-ibilisi, kwa kuwa ilidhaniwa anaweza kuzamisha meli. Hata hivyo, pweza huyo hujificha sana kwenye sakafu ya bahari katika mashimo na nyufa. Mikono yake minane ina urefu wa mita 10 hivi, na pweza ndiye mnyama aliye na ubongo mkubwa zaidi kati ya wanyama wote wasio na uti wa mgongo. Kwa kweli, pweza wana akili nyingi sana na wanaweza kujifunza kufanya mambo ya ajabu kama vile kufumbua mafumbo na kufungua vifuniko vya chupa!

Kama tu ngisi-jitu, pweza mkubwa anaweza kujificha kwa kubadili rangi, anaweza kujirusha juu kwa nguvu, na anaweza kuepuka hatari kwa kutoa wingu kubwa la rangi. Pweza anaweza hata kutoka majini kwa muda mfupi ili atafute chakula kwenye nchi kavu!

Viumbe hao wa baharini hulisifu sana jina la Muumba wao, Yehova. Ndiyo sababu mtunga-zaburi wa Biblia aliimba hivi: “Msifuni Yehova kutoka duniani, enyi wanyama wakubwa wa baharini, nanyi vilindi vyote vya maji.”—Zaburi 148:7.

[Mchoro katika ukurasa wa 17]

WANAWEZA KUWA WAKUBWA KADIRI GANI?

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Papa mweupe

Pweza mkubwa

Papa nyangumi

Ngisi-jitu*

Ngisi anayeitwa colossal*

*ukubwa unaokadiriwa

Nyangumi anayeitwa sperm

Nyangumi wa bluu-kijivu

futi 100 90 80 70 60 50 40 30 20 10 0

mita 30 25 20 15 10 5 0

[Picha katika ukurasa wa 15]

Papa mweupe

[Picha katika ukurasa wa 15]

Pweza mkubwa

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Nyangumi anayeitwa “sperm”

[Picha katika ukurasa wa 16]

Papa nyangumi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyangumi wa rangi ya bluu-kijivu na mtoto wake

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Shark: ©Steve Drogin/SeaPics.com; drawing: Getty Images; octopus: ©Brandon Cole

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Sperm whale: ©Brandon Cole; blue whales: ©Phillip Colla/SeaPics.com; whale shark: ©Steve Drogin/SeaPics.com