Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wazazi Waaminifu na Wenye Ushirikiano

Wazazi Waaminifu na Wenye Ushirikiano

 Wazazi Waaminifu na Wenye Ushirikiano

▪ Uwanda wa juu nchini Afrika Kusini uko karibu kuganda. Nikiwa ndani ya ofisi yangu kwenye orofa ya tatu, ninatazama mti usio na majani ukiyumbayumba kwa sababu ya upepo mkali wa majira ya baridi kali. Katika mti mwingine, njiwa fulani anapasha joto makinda yake ya siku tatu.

Kabla ya kutaga mayai, njiwa wa kiume na wa kike walishirikiana kujenga kiota, wa kiume alileta vijiti na wa kike alijenga. Walijenga kiota kizuri kwa sababu pepo kali za majira ya baridi kali hazijawahi kukiangusha, ingawa kiota hicho kimetumiwa mara mbili kutaga na kulea makinda. Njiwa wa kike alilalia mayai usiku; wa kiume akayalalia mchana. Baada ya majuma mawili, mayai hayo yalianguliwa. Kabla ya majuma mengine mawili kwisha, makinda hayo yatakuwa makubwa vya kutosha kuruka.

Sikiliza! Unasikia sauti hiyo laini inayosikika kama kicheko? Njiwa wa kike, akiwa amebeba chakula katika koo kwa ajili ya makinda yake yenye njaa, anatangaza kwamba amerudi na yuko tayari kubadilishana zamu na mwenzi wake. Hata baada ya makinda kuweza kuruka, wazazi wote wawili wataendelea kuyalisha hadi yatakapoweza kujitegemea.

Mimi hustaajabia jinsi ndege hao wanavyoshirikiana na kutunzana, jambo linalopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Mambo hayo hunifanya nikumbuke maneno ya Zaburi 86:8: “Hakuna yeyote aliye kama wewe . . . , Ee Yehova, wala hakuna kazi zozote kama zako.”

Katika Neno lake, Biblia Takatifu, Yehova Mungu amewapa wazazi wa kibinadamu mwongozo unaotegemeka kama mwongozo wa kisilika aliowapa njiwa. Kwa mfano, Biblia inawasihi akina mama “wawapende watoto wao.” (Tito 2:4) Inawaambia hivi akina baba: “Msiwe mkiwakasirisha watoto wenu, bali endeleeni kuwalea katika nidhamu na mwongozo wa akilini wa Yehova.” (Waefeso 6:4; 1 Timotheo 5:8) Kwa kweli, wazazi wanaofanya mambo hayo ni wenye thamani sana machoni pa Mungu.