Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ustadi wa Kutayarisha Kahawa ya Spreso

Ustadi wa Kutayarisha Kahawa ya Spreso

 Ustadi wa Kutayarisha Kahawa ya Spreso

Kahawa imekuwa moja kati ya vinywaji vinavyopendwa zaidi ulimwenguni kwa kuwa watu wanakunywa vikombe bilioni kadhaa vya kahawa kila mwaka.

KWA wanywaji fulani wa kahawa, spreso ni “kahawa murua sana,” linasema jarida Scientific American, “kwa kuwa inatayarishwa kwa njia ya pekee inayotokeza vizuri ladha yake.” Inatayarishwa kwa kupitisha kwa nguvu mvuke au maji moto kwenye kahawa iliyosagwa hadi ikawa laini kabisa.

Mtaalamu mmoja wa kutayarisha kahawa alimwambia hivi mwandishi wa Amkeni!: “Watu wanaofurahia kunywa spreso iliyotayarishwa kwenye mikahawa wanataka kuitengeneza nyumbani kwao.” Kwa sasa kuna mashini za kutengenezea spreso nyumbani. Kwa sababu hiyo, watu wengi zaidi wanakunywa spreso iliyotengenezewa nyumbani.

Je, wewe ni mnywaji wa kahawa? Je, ungependa kujifunza kupika spreso? Unahitaji kufanya nini ili kutayarisha kikombe murua cha kahawa? Mwandishi wa Amkeni! aliwauliza swali hilo John na baba yake, Gerardo ambao ni magwiji wa kukaanga kahawa, wanaoishi huko Sydney, Australia.

Kupata Mchanganyiko Unaofaa

Ndani ya kiwanda cha kukaanga kahawa cha John na Gerardo, kuna magunia mengi ya buni za kahawa kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. “Mimi huchanganya buni mbalimbali kulingana na maagizo fulani ya upishi yaliyochaguliwa kwa uangalifu,” anasema John. “Kila aina ya buni ina ladha yake na mwishowe huchangia kuwa na mchanganyiko wa ladha mbalimbali. Inachukua muda kupata ladha unayotaka. Kwa kweli, nilifanya majaribio mengi kwa miezi sita ili kupata ladha bora zaidi ya spreso.” Si ajabu kwamba magwiji wa kukaanga kahawa hawamruhusu mtu yeyote apate maagizo yao ya upishi!

Gerardo anasimamia kukaangwa kwa kahawa, jambo linalohitaji mtu azoezwe sana, kwa kuwa kukaanga kunabadili sana muundo wa kikemikali wa buni za kahawa na kutokeza gesi 500 hivi. Buni zinapoingizwa ndani ya chombo cha kukaangia, yaani, pipa linalopashwa joto kwa gesi, zinakuwa moto sana na kutoa sauti fulani wakati maji na kaboni dioksidi zinapochemka na kutoka na kisha buni zinapanuka. Kupanuka huko kunavunja kuta za chembe ndani ya buni na kutokeza mafuta yenye harufu nzuri. Harufu na ladha ya spreso inategemea mafuta hayo. Mtu anakuwa gwiji anapopata ustadi wa kukaanga buni, yaani, anapotambua wakati wa kuongeza moto na anapaswa kuzikaanga kwa muda gani.

Kwa wakati unaofaa kabisa, Gerardo anamwaga buni moto za rangi ya kahawia ndani ya kikapu cha chuma na kuzipulizia hewa baridi ili zisikaangike kupita kiasi. “Ladha ya kahawa inakuwa bora siku moja au mbili baada ya buni kukaangwa,” anasema John. Wakati huo, mafuta yanayotokeza ladha huwa yako tayari kutolewa kwenye buni.

Mbinu ya Kutayarisha Kahawa

“Kati ya mbinu zote za kutayarisha kahawa, spreso ndiyo mbinu rahisi zaidi lakini wakati uleule ngumu zaidi,” anaeleza John. Ili mtu atayarishe spreso nzuri zaidi anahitaji kufanya mambo matatu kwa usawaziko kabisa: kusaga buni (1), kushindilia kahawa iliyosagwa ndani ya kikapu cha kuchujia kilicho ndani ya mashini ya kupika kahawa (2), na kumwaga kahawa yenyewe (3). “Ni muhimu sana kusaga kahawa kwa njia inayofaa,” anasema John. “Kahawa ikisagwa kidogo, spreso itakuwa majimaji sana. Ikisagwa sana, kahawa itakuwa na ladha chungu na iliyounguzwa. Katika visa vyote, spreso inapomwagwa, povu linalotanda juu yake litaonyesha ikiwa mafuta yaliyo  ndani ya buni yametolewa kwa njia inayofaa.”

Baada ya kusaga buni chache, John anatumia kifaa fulani kuzishindilia ndani ya kikapu cha kuchujia na hivyo zinakuwa laini. Kisha anaingiza kikapu ndani ya mashini na kuiwasha. Kahawa moto inaanza kutoka. Mara moja, John anagundua kwamba buni hazikusagwa vya kutosha. “Mara nyingi unahitaji kujaribu mara kadhaa ili utayarishe spreso nzuri zaidi,” anasema. “Hebu tujaribu tena tukitumia buni zilizosagwa sana. Pia, tutashindilia buni zaidi ili kahawa itoke polepole.”

John anafanya marekebisho hayo na kuwasha mashini tena. Kahawa yenye povu nzito sasa inatoka ikiwa na uzito unaofanana na wa asali yenye joto. Harufu nzuri inapotanda hewani, tabasamu la John linaonyesha kwamba hiyo kahawa ni murua. “Ni muhimu sana tuache kumimina kahawa wakati rangi yake nzito inapoanza kuisha,” anasema. Hiyo inachukua muda usiozidi sekunde 30. “Ukiendelea kumwaga kahawa zaidi,” anasema, “unapata kahawa yenye ladha chungu na kafeini nyingi zaidi.”

“Nafikiri tumetayarisha spreso bora zaidi,” anasema John, akitazama povu nzito, laini, na iliyoshikana kabisa. “Je, ungependa kikombe cha kahawa?”

Watu fulani wanaopenda sana kahawa halisi, hawapendi kuongeza chochote isipokuwa tu labda sukari kidogo. Hata hivyo, wengine huongeza maziwa moto ili kutokeza cappuccino, latte, au aina nyingine za spreso. “Leo, zaidi ya asilimia 90 ya kahawa inayouzwa ni ile iliyochanganywa na maziwa,” linasema gazeti Fresh Cup Magazine. *

Kuwa na mazungumzo mazuri huku mkifurahia kunywa chai au kahawa, ikitegemea unapenda kunywa nini, ni moja kati ya mambo yanayofurahisha zaidi maishani. “Vinywaji vyenye ladha nzuri vinawaunganisha watu,” anasema John. “Huenda hilo ndilo jambo linalopendeza zaidi kuhusu vinywaji hivyo!”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 15 Ikiwa unajiuliza ikiwa Mkristo anapaswa kuepuka kahawa na chai kwa sababu vinywaji hivyo vina dawa ya kafeini inayoweza kutokeza uraibu, huenda ukapenda kusoma makala ya “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Aprili 15, 2007 (15/4/2007).

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

KUNUNUA NA KUHIFADHI KAHAWA

“Kahawa iliyokaangwa huanza kupoteza ladha baada ya juma moja, kahawa iliyosagwa hupoteza ladha baada ya saa moja, na kahawa iliyochemshwa hupoteza ladha baada ya dakika chache,” kinasema kitabu fulani cha kununua kahawa. Hivyo, ukitaka kujinunulia buni, ni vizuri kuzinunua kwa kiasi kidogo na kuzihifadhi mahali penye giza na pasipo na unyevu. Lakini usizitie ndani ya friji, kwa kuwa zinaweza kufyonza unyevunyevu na kupoteza ladha. Na sikuzote chemsha kahawa baada tu ya kuisaga.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Photo 3: Images courtesy of Sunbeam Corporation, Australia