Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

▪ Chaza aliyevuliwa kutoka kwa sakafu ya Bahari ya Atlantiki Kaskazini ametajwa kuwa “mnyama aliyeishi kwa muda mrefu zaidi.” Wanasayansi walipohesabu mikunjo katika koa lake, walikadiria kwamba chaza huyo alikuwa na umri wa miaka 405.—SUNDAY TIMES, UINGEREZA.

▪ “Uchumi unapozorota, hata watu walio matajiri sana huathiriwa sana. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hilo waulize madaktari wao wa akili.”—THE NEW YORK TIMES, MAREKANI.

TV Inaathiri Mwenendo Kuhusu Ngono

“Kuna uthibitisho wa kutosha kuonyesha kwamba ikiwa vijana watatazama vipindi vya televisheni vinavyoonyesha ngono, mwenendo na mtazamo wao kuhusu ngono utaathiriwa,” inasema ripoti iliyochapishwa katika jarida Pediatrics. Kulingana na uchunguzi mmoja, vijana wanaotazama sana vipindi hivyo “wana uwezekano maradufu wa kupata mimba” kuliko wale ambao hawavitazami sana. Huenda sababu moja ikawa kwamba televisheni hufanya vijana wafikiri kwamba ngono haina madhara, kwa kuwa mimba na magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono hayaonyeshwi waziwazi. Bila shaka, si televisheni peke yake inayoathiri mwenendo wa vijana kuhusu ngono. Wachunguzi wamedokeza kwamba magazeti, Intaneti, na muziki imeathiri maoni yao kuhusu ngono.

Watu Wanaambukizwa Ukoma

Watu elfu tatu nchini Marekani wanatibiwa ukoma, ambao pia huitwa ugonjwa wa Hansen. Visa 150 hivi hugunduliwa kila mwaka. Wagonjwa wengi wametoka nchi nyingine. Hata hivyo, kulingana na Programu ya Kitaifa ya Ugonjwa wa Ukoma huko Baton Rouge, Louisiana, “kila mwaka wenyeji 30 hivi wa Louisiana kusini na wa Texas kwenye pwani ya Marekani inayopakana na Ghuba ya Mexico wanaambukizwa ukoma. Wenyeji hao wamezaliwa Marekani na hawajawahi kutembelea nchi ambazo watu wengi wanaugua ukoma,” linasema Shirika la Marekani la Magonjwa ya Kitropiki na Maambukizo. Wachunguzi bado hawaelewi jinsi ugonjwa huo unavyoenea. Ukigunduliwa mapema, ukoma unaweza kutibiwa kabisa. Hata hivyo, ukiisha kukita mizizi, madhara kwenye mfumo wa neva hayawezi kurekebishwa.

Wizi wa Silaha Zenye Mnururisho

“Uwezekano wa magaidi kupata silaha za nyuklia au zile zenye mnururisho bado ni tisho kubwa,” anasema Mohamed ElBaradei, msimamizi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomu. “Visa vinavyoripotiwa kwa Shirika hilo kuhusiana na wizi au kupotea kwa silaha za nyuklia au zile zenye mnururisho ni vingi sana—karibu visa 250 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka wa 2008 peke yake. Jambo lenye kuhangaisha pia ni kwamba silaha nyingi zilizopotea hazipatikani tena.” Hawajui ikiwa hali hiyo inasababishwa na uhitaji mkubwa wa silaha zenye mnururisho au ikiwa nchi wanachama wanaripoti kwa usahihi zaidi silaha zilizopotea.

Kigae Chenye Maandishi ya Kale Kimepatikana Israel

Wataalamu wa vitu vya kale wa Israel walichimbua kigae chenye maandishi ya kale ambacho huenda kiliandikwa miaka 1,000 kabla ya Vitabu vya Kukunjwa vya Bahari ya Chumvi. Maandishi hayo ambayo ni mistari mitano iliyoandikwa kwa wino kwenye kigae, yaligunduliwa kwenye machimbo ya ngome ya Yuda ya karne ya 10 K.W.K. huko Khirbet Qeiyafa, Israel. Maandishi hayo bado hayajafasiriwa kikamili, lakini yanaonekana kuwa hati ya kisheria iliyoandikwa na mwandishi stadi na yanaonyesha “shina la maneno ‘hakimu,’ ‘mtumwa’ na ‘mfalme,’” inasema taarifa ya Chuo Kikuu cha Hebrew huko Jerusalem iliyotolewa katika vyombo vya habari.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]

Gabi Laron/Institute of Archaeology/Hebrew University © Yosef Garfinkel