Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi ya Kutibu Ugonjwa wa Kushuka Moyo

Jinsi ya Kutibu Ugonjwa wa Kushuka Moyo

 Jinsi ya Kutibu Ugonjwa wa Kushuka Moyo

“MIMI na mume wangu tumetafuta matibabu, tukabadili mtindo wetu wa maisha, na kujitahidi kuwa na ratiba inayonifaa,” anasema Ruth, ambaye ameugua ugonjwa wa kushuka moyo kwa miaka mingi. “Sasa inaonekana tumepata dawa inayonifaa na ninahisi nafuu. Lakini wakati nilipohisi hakuna chochote kinachoweza kunisaidia, mume wangu na marafiki walinionyesha upendo nyakati zote na hivyo kunisaidia nisikate tamaa.”

Kama vile kisa cha Ruth kinavyoonyesha, watu wanaougua ugonjwa wa kushuka moyo sana wanahitaji msaada kutia ndani matibabu yoyote yanayofaa. Ni hatari kupuuza ugonjwa huo kwa sababu mara nyingine ukikosa kutibiwa mtu anaweza kufa. Miaka elfu mbili hivi iliyopita, Yesu Kristo alisema kwamba watu wenye ujuzi wa kitiba wanaweza kumsaidia mtu aliposema “wale walio wagonjwa wanamhitaji [tabibu].” (Marko 2:17) Ukweli ni kwamba matabibu wanaweza kuwasaidia sana wagonjwa walioshuka moyo. *

Mapendekezo Yanayoweza Kusaidia

Kuna matibabu mbalimbali kwa ajili ya ugonjwa wa kushuka moyo ikitegemea dalili na kiwango cha ugonjwa. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 5,  “Aina Mbalimbali za Ugonjwa wa Kushuka Moyo.”) Watu fulani wanaweza kutibiwa na daktari wa kawaida, lakini wengine wanahitaji usaidizi wa wataalamu. Huenda daktari akampa mgonjwa dawa za  kutuliza akili au akapendekeza matibabu mengine. Wengine wamepata matokeo mazuri kwa kutumia mitishamba, kubadili vyakula, au kufanya mazoezi.

Mambo Yanayosababisha Matatizo

1. Marafiki wenye nia nzuri ambao hawana ujuzi mwingi au hawana ujuzi wowote wa mambo ya kitiba wanaweza kujaribu kukufanya ukubali matibabu fulani na ukatae mengine. Huenda pia wakakuamulia ikiwa utatumia mitishamba, dawa ulizoandikiwa na daktari, au kukukataza usitumie chochote.

Fikiria hili: Hakikisha kwamba mashauri yoyote unayokubali yanatoka kwa chanzo kinachotegemeka. Mwishowe wewe ndiye utakayejiamulia baada ya kupata habari kamili.

2. Kuvunjika moyo kunaweza kufanya wagonjwa waache matibabu waliyochagua kwa sababu hawapati nafuu au matibabu hayo yanawadhuru kwa njia fulani.

Fikiria hili: “Mipango huvunjika mahali ambapo hapana mazungumzo ya siri, lakini katika wingi wa washauri mambo hutimizwa.” (Methali 15:22) Huenda matibabu yoyote yakawa na matokeo mazuri kukiwa na mawasiliano mazuri kati ya daktari na mgonjwa. Mweleze waziwazi daktari mahangaiko na dalili zako, na umuulize ikiwa unahitaji kubadili matibabu au uvumilie kwa muda kabla ya kuanza kupata matokeo mazuri.

3. Kujitumaini kupita kiasi kunaweza kuwafanya wagonjwa waache matibabu yao ghafula baada ya majuma machache tu kwa sababu wanahisi nafuu. Wanaweza kusahau jinsi  ugonjwa huo ulivyowadhoofisha kabla ya wao kuanza kupata matibabu hayo.

Fikiria hili: Kuacha matibabu ghafula bila kuambiwa na daktari kunaweza kuwa na matokeo mabaya na hata kuhatarisha uhai wako.

Ingawa Biblia si kitabu kinachozungumzia mambo ya kitiba, Yehova Mungu, Mtungaji wa Biblia ndiye Muumba wetu. Makala inayofuata itachunguza faraja na mwongozo ambao Neno la Mungu linawapa wale walioshuka moyo na pia wale wanaowatunza.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote hususa. Kila mtu anapaswa kuchunguza matibabu mbalimbali kabla ya kufanya uamuzi wake.

 [Sanduku katika ukurasa wa 5]

AINA MBALIMBALI ZA UGONJWA WA KUSHUKA MOYO

Matibabu yanayofaa yanategemea mtu anaugua aina gani ya ugonjwa wa kushuka moyo.

Ugonjwa wa kushuka moyo sana una dalili ambazo zinaweza kudumu kwa miezi sita au zaidi usipotibiwa na zinaathiri sana maisha ya mgonjwa.

Ugonjwa wa kubadilika-badilika kwa hisia. Wagonjwa wanaweza kusisimka sana kwa muda mrefu na ghafula washuke moyo sana.—Ona makala “Kuishi na Ugonjwa wa Kihisia,” katika Amkeni! la Januari 8, 2004 (8/1/2004).

Ugonjwa wa kushuka moyo kidogo haudhoofishi kama ugonjwa wa kushuka moyo sana lakini dalili zake humzuia mgonjwa asiweze kuendelea na shughuli zake za kawaida. Pia watu wanaougua ugonjwa huo wanaweza kushuka moyo sana kwa vipindi vifupi.

Ugonjwa wa kushuka moyo baada ya kujifungua huwapata wanawake wengi na huathiri sana hisia.—Ona makala “Kuelewa Mshuko wa Moyo Baada ya Kujifungua” katika Amkeni! la Juni 8, 2003, (8/6/2003).

Ugonjwa wa kushuka moyo katika majira fulani hasa unatokea katika majira ya kupukutika kwa majani na majira ya baridi kali kwa sababu ya ukosefu wa mwangaza wa jua. Kwa kawaida ugonjwa huo huisha katika majira ya kuchipua na majira ya kiangazi.