Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Plovdiv—Jiji la Kisasa Lenye Mambo ya Kale

Plovdiv—Jiji la Kisasa Lenye Mambo ya Kale

 Plovdiv—Jiji la Kisasa Lenye Mambo ya Kale

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BULGARIA

PLOVDIV ni jiji la zamani kuliko Roma, Karthage, na Constantinople. Watu 350,000 hivi wanaishi katika jiji hilo lililojengwa juu ya vilima saba kusini ya kati nchini Bulgaria.

Unapotembea kwenye barabara zake za kale, utaona mambo yanayoonyesha kwamba nyakati za kale jiji hilo lilikuwa lenye utukufu na msukosuko. Unaweza kuona majengo ya Wathrasi ambao waliogopwa sana walioishi mamia ya miaka kabla ya Wakati wa Kawaida, na pia utaona nguzo za Wagiriki, majumba ya maonyesho ya Waroma, na minara ya Waturuki.

‘Jiji Maridadi Zaidi Kati ya Yote’

Vitu vilivyochimbuliwa ndani ya jiji hilo na katika maeneo ya karibu yanaonyesha kwamba watu walianza kuishi huko muda mrefu kabla ya mwaka wa 1000 K.W.K. Mwanahistoria Mroma, Ammianus Marcellinus aliandika kwamba kabla ya karne ya nne K.W.K., ngome ya Wathrasi iliyoitwa Eumolpias ilikuwepo mahali jiji la kisasa la Plovdiv lipo. Katika mwaka wa 342 K.W.K., Eumolpias ilishindwa na Philip wa Pili wa Makedonia, baba ya Aleksanda Mkuu. Philip alibadili jina la jiji hilo kuwa Philippopolis.

Waroma walipoteka jiji hilo mnamo 46 W.K., waliliita Trimontium na wakalifanya kuwa mji mkuu wa Thrasi. Waroma walitaka sana kulidhibiti jiji hilo kwa kuwa lilikuwa kando ya Via Diagonalis iliyokuwa makutano ya barabara muhimu  ya eneo la Balkani. Waroma walijenga uwanja wa michezo, uwanja-duara wa maonyesho (ona picha juu), bafu nyingi sana, na majengo mengine mengi ya Kiroma.

Lucian wa Samosata alifafanua uzuri wa asili wa jiji hilo, ambalo lilijengwa katikati ya vilima vitatu chini ya Milima ya Rhodope. (Ona sanduku  “Jiji Lenye Vilima Saba,” kwenye ukurasa wa 18.) Lilikuwa karibu na Mto Maritsa, na uwanda wa Thrasi wenye rutuba ulikuwa mbele yake. Lucian aliandika kwamba Trimontium lilikuwa “jiji bora na maridadi zaidi kati ya yote!”

Baada ya kuanguka kwa Roma katika kile kilichoitwa Enzi za Giza, Waslavi waliishi katika eneo hilo. Katika karne chache zilizofuata, wapiganaji watakatifu walipora jiji hilo mara nne tofauti. Kisha, katika karne ya 14, badiliko la kisiasa lilitukia wakati jiji hilo lilipoanguka mikononi mwa Waturuki. Walibadili jina la jiji hilo kuwa Philibé na wakamiliki jiji hilo hadi 1878. Msikiti wa Jumaia ukiwa na mnara na saa inayotumia kivuli huwakumbusha watu kuhusu kipindi hicho.

Urusi iliposhinda Uturuki mnamo 1878, jina la jiji hilo lilibadilishwa na badala ya kuitwa Philibé likaitwa Plovdiv. Jiji hilo lilianza kusitawi kiuchumi katika mwaka wa 1892 wakati ambapo lilikuwa na maonyesho ya kibiashara. Kuanzia wakati huo, Plovdiv likawa kituo kikuu cha  biashara huko Bulgaria. Wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Wanazi walidhibiti jiji hilo kwa muda lakini wakatimuliwa na Wasovieti mnamo 1944. Kisha mnamo 1989, Muungano wa Sovieti ulipoanguka, kwa mara nyingine tena Plovdiv liliacha kumilikiwa na milki hiyo yenye nguvu. Huenda wamiliki wa kale wa Plovdiv walikuwa wanyoofu; lakini kama utawala mwingine wa wanadamu, utawala wao ulikuwa na matatizo yanayosababishwa na kutokamilika.

Habari Njema Zafika Plovdiv

Katika mwaka wa 1938, shirika linaloitwa Nabludatelna Kula (Watch Tower) lilianzishwa na kuandikishwa katika eneo hilo. Lilichapisha na kugawa Biblia na vichapo vya Biblia nchini Bulgaria. Licha ya jitihada za serikali ya Ukomunisti za kuwakandamiza, Mashahidi wa Yehova waliendelea kuwahubiria watu wa Plovdiv habari njema za ufalme mkamilifu wa kimbingu unaokuja. (Mathayo 24:14) Watu wachache walianza kuitikia ujumbe huo. Sasa kuna watu zaidi ya 200 huko Plovdiv ambao wamechukua msimamo upande wa Yehova, nao wako katika makutaniko mawili ya Mashahidi wa Yehova.

Wengi kati ya Mashahidi hao ni Wabulgaria. Lakini kati yao kuna watu wengi kutoka mataifa mengine mengi, kama vile historia ya jiji hilo inavyoonyesha kwamba lilikaliwa na watu kutoka mataifa mbalimbali. Kuna Waingereza, Waitaliano, Wakanada, Wamarekani, Wamoldova, na Wapolandi. Wao wote huwaambia majirani wao kuhusu taraja la kutawaliwa na serikali kamilifu. Wakati huo, wakazi wa Plovdiv na watu ulimwenguni pote watafurahia usalama, “kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, wala hakutakuwa na mtu yeyote anayewatetemesha.”—Mika 4:4.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

“JIJI LENYE VILIMA SABA”

  Inaweza kuwa vigumu kwa mtu anayetembelea Plovdiv leo kuona vilima vyake saba maarufu, au tepe, kama vinavyojulikana. Miaka mia moja iliyopita, kilima kimoja, Markovo Tepe, kilibomolewa ili jiji hilo lipanuliwe. Vilima sita vimebaki ili kutoa ushuhuda kimyakimya wa historia ya Plovdiv.

Mtalii yeyote anaweza kuona vilima vitatu waziwazi: Bunardjik Tepe, Djendem Tepe, na Sahat Tepe, ambacho kiliitwa Sahat na Waturuki kwa sababu ya mnara wa saa uliojengwa juu yake. Trimontium, jina ambalo Waroma waliita jiji la Plovdiv, lina vilima vingine vitatu: Djambaz Tepe, ambacho ndicho kilima kipana na kirefu zaidi; Taksim Tepe; na Nebet Tepe, ambacho katika Kituruki kinamaanisha “Kilima cha Ulinzi.”

Unapotembea kupitia Trimontium unaweza kuona historia yote ya Plovdiv, kuanzia magofu ya kale na kuta za Philippopolis kufikia jumba la maonyesho la Waroma ambalo bado linatumika. Pia unaweza kufurahia kuona nyumba zilizohifadhiwa vizuri za enzi ya Kuchochea Utaifa nchini Bulgaria zilizo kwenye barabara nyembamba zilizojengwa kwa mawe.

[Hisani]

© Caro/Andreas Bastian

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BULGARIA

SOFIA

Plovdiv

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Top: © Wojtek Buss/age fotostock; bottom: David Ewing/Insadco Photography/age fotostock